NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na
Mifugo Zanzibar Shamata Shaame Khamis, amewaagiza wakulima wa ndizi wilaya ya
Mkoani, kuepukana na vishoka wa biashara hiyo, na badala yake walitumie soko
jipya la Mtambile, ili kupata bei kubwa.
Waziri Shamata aliyasema hayo jana, mara baada ya
ufunguzi wa soko la mboga na matunda la Mtambile wilaya ya Mkoani, ikiwa ni
sehemu za shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964.
Alisema, kuanzia sasa waachane na wanunuzi wa ndizi
wanaowalalia kibei, na badala yake sasa walitumie soko hilo, ili kuzipandisha
thamani ndizi zao.
Alieleza kuwa, ndani ya soko hilo mtakuwa na mnada maalum
wa mazao mbali mbali, ikiwemo ndizi, muhogo, matikti, nyanya, chungwa na ndimu,
hivyo ni wajibu kwa wakulima hao, kulitumia soko hilo.
Waziri Shamata, alisema kwa muda mrefu, wakulima walikuwa
wanalaliwa kibei na wachuuzi wanaosafirisha bidhaa hiyo nje ya kisiwa cha
Pemba, kwa kueleza kuwa kunaanguko la bei.
‘’Niwatake wakulima wa ndizi, sasa iwe basi kulaliwa bei
na njooni hapa ndani ya soko jipya, na muuze bidhaa hiyo na mtapata bei, maana
patakuwa na ushindani wa bei,’’alieleza.
Hata hivyo Waziri huyo, aliliagiza baraza la mji wa
Mkoani, kutenga bajeti maalum, kwa ajili ya matengenezo madogo madogo ya soko
hilo hapo baadae.
‘’Leo (jana) tumelifungua soko hili, linang’ara na
linapendeza, sasa ni wajibu kwa Baraza la mji Mkoani, kuanzia sasa kujiwekea
bajeti maalum, kwa ajili ya matengenezo,’’alifafanua.
Aidha amewataka wafanyabiashara wote na hasa wale waliokuwa
wakianyabiashara zao pembezoni mwa barabara, sasa kuhamia ndani ya soko hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo wa Umwagiliaji,
Maliasili, na Mifugo, alisema kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,
yamewakomboa wananchi kiuchumi.
Alisema kuwa, kabla ya kufanyika kwa Mapinduzi hayo,
wananchi wa Zanzibar, hawakuwa na nafasi ya kulima na kuuza kwa bidhaa zao kwa
thamani, jambo lililowazidishia unyonge.
‘’Tukiwa ndani ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, lazima
tuwakumbuke waasisiwa wa taifa hili, akiwemo rais wa kwanza wa Zanzibar,
marehemu Abied Amani Karume na mwenzake kwa kujitolea,’’alisema.
Hivyo amewataka wananchi, kuendelea kuiunga mkono serikali
ya awamu ya nane, ambayo inaendelea kutekeleza dhana ya mapinduzi daima kwa
vitendo, kwa kujenga miradi mikubwa ya maendeleo.
Kwa upande wake, Katibu mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa, serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Issa Mahafudhi, alisema ujenzi
wa soko hilo, ni utekeleza wa ahadi ya Rais wa Zanzibar, wakati alipokutana na
wajasiriamali.
Hata hivyo alisema, mji wa Mtambile umekuwa na ongezeko
la watu kila mwaka, na sasa kuchukua nafasi ya tatu kwa idad
‘’Hivyo uwepo wa soko hili, limeandana na mahitaji ya
wananchi kwa muda mrefu na hasa suala la changamoto, iliyopo ya wafanyabiashara
kuendesha shughuli zao pembezoni mwa barabara,’’alifafanua.
Mkuu wa Mkoa wa kusini
Pemba, Mattar Zahor Massoud, alisema serikali inampango wa kujenga soko jingine
kama hilo, katika eneo shehia ya Kengeja, ili kukidhi mahitaji ya
wajasiriamali.
Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, alisema
yalifanyika kwa lengo la kuwapa heshima wazalendo wa taifa hili, ikiwemo kujitambua
kiutu na kiuchumi.
‘’Leo tukiadhimisha miaka 60, kila mmoja ni shuhuda kuwa,
ameyapata matunda ya mapinduzi, iwe kwenye sekta ya elimu, afya, barabara, maji
safi na salama,’’alifafanua.
Soko hilo la matunda na mboga la Mtambile inavyo vikuta
40, milango 13 ya maduka, ambapo ujenzi wake ulianza mwishoni mwa mwaka 2022,
na kumalizika mwezi Julai mwaka huu.
Ujenzi huo umepitia hatua tatu, ikiwemo ukataji mlima,
ujenzi wa soko lenyewe na uweka saruji chini nje ya soko hilo, lenye vyoo
vinane, kikiwemo cha watu wenye ulemavu.
Aidha ujenzi huo, umegharimu zaidi ya shilingi milioni 5.88
ambapo ni fedha zinazotokana na makusanyo ya baraza la mji Mkoani, kupitia
serikali kuu.
Shamra shamra hizo za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar
zitaendelea tena kesho, eneo la Makangale ambapo Waziri wa Biashara na
Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban atalifungua tangi la maji safi
na salama.
Mwisho
Comments
Post a Comment