NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
CHUO cha Utawala wa Umma Zanzibar ‘IPA’ tawi
la Pemba, kimewakumbusha waalimu, wa skuli za wilaya ya Chake chake, kuendelea
kuwa kioo, kwa kuwa na maadili mema ndani ya jamii.
Ushauri huo umetolewa Disemba 18, 2023 na Mkuu wa chuo hicho
tawi la Pemba, Juma Haji Juma, wakati akiwasilisha mada ya maadili kwa watumishi
wa umma, kwenye mafunzo ya uthibitisho wa kazi, kwa waalimu hao, mafunzo yaliyofanyika
skuli ya sekondari Madungu wilayani humo.
Alisema, jamii inategemea na kusoma kila
kitu kutoka kwa Mwalimu, hivyo ni wajibu wake, hilo kulijua na kuhakikisha anaendelea
kung’ara ndani ya jamii, kwa kujipamba na maadili mema.
Alieleza kuwa, miongozo ya sheria na kanunu
za kiutumishi, zipo kwa ajili ya kutoa muongozo zaidi, lakini Mwalimu mwenyewe
analazimika kuongeza wigo, wa kujipamba na tabia njema.
‘’Mwalimu ndio kila kitu ndani ya jamii,
kuanzia kivazi, aina ya maeneo anayokaa kuzungumza, matumizi ya lugha na hata namna
anavyoilinda nchi yake, kwa maneno mazuri,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa tawi la ‘IPA’
Pemba, Juma Haji Juma, alisema eneo jingine kwa waalimu wanatakiwa kuhakikisha
wanaishi nalo, ni dhana ya uzalendo kwa taifa lao.
Akifungua mafunzo hayo, Mratibu Idara ya Utumishi na Uendeshaji kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Harith Bakar Waziri, alisema wizara haitaki kuona, kuwa kuna mtumishi anatimiza miaka miwili, pasi na kupata mafunzo ya uthibitisho wa kazi.
Alifafanua, ndani ya awamu hii ya serikali
ya awamu ya nane, Wizara imepewa kipaumbele cha aina yake, ikiwemo kuwezeshwa
kufanya mafunzo hayo.
‘’Mafunzo haya mkimaliza yatawapa haki
mbali mbali, ikiwemo ya likizo, safari kikazi kwani ni sehemu ya uthibitisho wa
kazi, kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Mratibu huyo,
alisema mafunzo hayo yataendeshwa Pemba nzima, kwa waalimu wote ambao
wameajiriwa hivi karibuni, ili kuweka sawa matakwa ya kisheria.
Akiwasilisha mada ya dhana ya muwamko wa
kustaafu salama kwa watumishi wa umma, mtendaji kutoka ‘IPA’ Ali Issa Matlubu,
alisema mada hiyo ni mpya kwa watumishi wapya.
Alieleza kuwa, IPA iliona iwaletee mada
hiyo watumishi hao wapya, ili wafahamu kuwa, mara baada ya kuajiriwa kitendo
kinachofuata ni kustaafu, iwe kwa lazima, hiari au sheria.
Hata hivyo amesema, tafiti mbali mbali zinaonesha kuwa 70, kila wastaafu 100 wanakosa matayarisho muhimu ya kuelekea kustaafu, jambo linalosababisha magonjwa na hatimae vifo.
Mafunzo hayo ya siku mbili, mada nane
zitafundishwa ikiwemo uzalendo, sheria ya Afya na Usalama kazini, sheria ya
Utumishi wa umma, Maadili ya watumishi, sheria ya Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na
Uhujumu wa uchumi ‘ZAECA’ pamoja na dhana ya kustaafu kwa salama.
Mwisho
Comments
Post a Comment