NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAZIRI wa Nchi, Ofis ya Rais, Kazi, Uchumi na
Uwekezaji Zanzibar, Mudrik Ramadhan
Soroga, amesema miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar, imemletea heshima mzanzibari,
kwa kupata haki zake bila ya ubaguzi, ikilinganishwa na kabla ya mwaka 1964.
Alisema, kwa sasa kila mmoja anapata haki ya kuwasilisha
lalamiko lake, katika vyombo vya sheria na kupokelewa kwa heshima na kisha
kusikilizwa na uamuzi kutolewa kwa haki.
Waziri Soraga, aliyasema hayo leo Disemba 22, 2023 mara baada ya uwekaji
wa jiwe la msingi la kituo cha Polisi cha wilaya ya Mkoani cha daraja ‘B’ ikiwa
ni sehemu za shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964.
Alisema, sasa mzanzibari anatembea kifua mbele, akijua kuwa
inapotokezea kubinywa kwa haki zake, anapopakukimbilia na kufungua mashauri,
ambayo yanaendeshwa kwa haki kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Alieleza kuwa, waasisi wa taifa hili walipigania haki za
wazalendo na mwendo huo unaendelezwa hadi leo ndani ya serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo ujenzi wa vituo vya
kisasa vya Polisi.
‘’Niwaambie kuwa, ujenzi huu wa kituo cha Polisi Mkoani,
ni sehemu ya matunda ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambayo msingi wake
mkuu ni Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,’’alifafanua.
Akizungumzia Mapinduzi hayo, Waziri Soroga, alisema
yameleta tija kwa wananchi wa Zanzibar, kwani kabla ya hapo utu, heshima, hadhi
ya mzalendo haikuwa ikitambulika.
Alieleza kuwa, kilichokuwa kikijitokeza kwa wazazi wa
wakati huo, ni madhila, kufanyishwa kazi ngumu zenye malipo duni na ambayo
hayakujali utu wao.
Alifahamisha kuwa, suala la kukosa haki, elimu, matibabu
na huduma nyingine muhimu kwa wakati huo, lilikuwa jambo la kawaida, hali ambayo
wapinga dhulma iliwauma.
‘’Leo tunafuraha kubwa mno, baada ya waasisi wa taifa
hili, kufanya mbinu za kimapinduzi, mkoloni ameshaondoka na sasa kila mmoja
ananeemeka na matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,’’alieleza.
Akizungumzia uwepo wa kituo hicho cha Polisi daraja ‘B’ Waziri
huyo, ameliomba Jeshi la Polisi iwe chachu ya kufanyakazi kwa bidii na kutoa
huduma bora bila ya upendeleo kwa wananchi.
Alieleza kuwa, kituo hicho kikazae matunda ya kutokomeza
majanga yaliomo ndani jamii, ikiwa ni pamoja na vitendo vya ukatili na
udhalilishaji wa wanawake na watoto, dawa za kulevya na ulevi.
Aidha amewakumbusha kuendelea kukitunza, kukilinda na
kukienzi, ili kiwafae kizazi cha sasa na kijacho, kwani gharama za ujenzi wa kituo
hicho ni kodi za wananchi.
Mapema Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Abdalla
Hussein Mussa, alisema kituo hicho kimewapa ari na kasi zaidi ya utendaji kazi,
hasa kwa vile kinahuduma zote muhimu.
Alieleza kuwa, kituo cha kisasa chenye vyumba 31,
ikijumuisha chumba kwa ajili ya mkuu wa kituo, mkuu wa Polisi wilaya, mkuu wa upelelzi
wa makosa ya jinai, vyamba saba kwa ajili ya mahabusu wakiwemo watu mashuhuri,
watoto wa kike na kiume, watu wazima.
Aidha alieleza kuwa mradi wa ujenzi huo umegharimu
shilingi milioni 700, ambapo kati ya fedha hizo, shilingi milioni 580 ni
gharama ya ujenzi na shilingi milioni 120 ni malipo ya fundi.
Alifahamisha kuwa, mradi huo ambao umejengwa na fundi wa
ndani ya jamii, ulianza Mei 11, mwaka huu na kumalizika, Disemba 5 mwaka huu na
tayari kwa ajili ya kuhamiwa.
‘’Ujenzi wa kituo hichi kipya cha Polisi hapa wilaya ya
Mkoani, ni hatua kubwa ya serikali, katika kuwandoshea wananchi na Polisi
changamoto za eneo la kazi, kwani sasa huduma zitatolewa kwa ufanisi,’’alifafanua.
Mapema Katibu mkuu ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera,
Uratibu na Barazala la Wawakilishi Zanzibar Dk. Islam Seif, alisema kwa sasa
kila mmoja ni shuhuda, jinsi Zanzibar ilivyopiga hatua ya maendeleo.
Alieleza kuwa, viongozi wa kitaifa wa Zanzibar,
waliosimamia kufanyika kwa Mapinduzi haya, wamefanyakazi kubwa ya kuwakomboa
wananchi mbali mbali, na kwa sasa kila mmoja anatembea kifua mbele.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud,
alisema serikali bado inayonia ya kujenga vituo vyingine vipya vya Polisi, ili
wananchi wapate huduma bora katika mazingira bora.
Hata hivyo, amewakumbusha Jeshi la Polisi, kuendelea
kufanyakazi kwa bidii na kwa dhana ile ya ile, ya kuwalinda wananchi na mali zao
tena bila ya ubaguzi.
Alisema huu sio wakati tena kwa wananchi, kuendelea kulilalamikia
Jeshi la Polisi kiutendaji, kwani waelewe kuwa, ujenzi wa kituo hicho kipya ni
kodi za wananchi.
Shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zitaendelea
tena asubuhi hii, kwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban
kulifungua tangi la kuhifadhi maji Makaangale, ambapo kesho Waziri huyo, pia
ataweka jiwe la msingi la mradi wa utotoleshaji vifaranga vya matango bahari,
shehia ya Pujini wilaya ya Chake chake.
Mwisho
Comments
Post a Comment