Skip to main content

WATU WENYE ULEMAVU MAKOMBENI WATAKA ELIMU KUANZISHA USHIRIKA





NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WATU wenye ulemavu shehia ya Makombeni wilaya ya Mkoani Pemba, wamesema wana hamu ya kutaka kuanzisha vikundi vya ushirika, ingawa changamoto ni taaluma ndogo ya kuendesha vikundi hivyo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi shehiani hapo, walisema wamekuwa na hamu ya kutaka kujikusanya, ili kufikia ndoto zao kupitia vikundi vya ushirika, ingawa changamoto ni elimu ndogo ya uanzishwaji wa vikundi.

Walisema, wamekuwa wakigubikwa na umaskini wa kipato, ambao wanaamini kama wengekuwa na uwezo kielimu wa kuanzisha vikundi, wengekuwa na hali nzuri kimaisha.

Mmoja kati ya watu hao wenye ulemavu wa ualibino Mbuke Ramadhan Mussa, alisema wamekuwa hawajui wapi pakuanzia ili hadi kufikia kuwa na kikundi cha ushirika.

Alieleza kuwa, hawaelewi kuwa sheha anaweza kuwa chanzo cha wao kuanzisha vikundi vya ushirika, bali wapo kwenye makaazi wakiwa hawajui la kufanya.

‘’Ni kweli sisi watu wenye ulemavu wa shehia ya Mkoambeni, tunahitaji kupata uwelewa wa kuanzisha vikundi vya ushirika, ili tuwe kama wenzetu katika kukuza pato lao,’’alieleza.

Kwa upande wake Mayasa Makame Chumu mwenye ulemavu wa viungo, alisema inawezekana hali ngumu waliyonayo inatokana na kukosa elimu ya kutojikusanya pamoja.

‘’Naamini kama tutapewa mtaalamu wa kutupatia elimu ya uanzishwaji wa vikundi, umaskini wa kipato kwetu utakuwa ndoto,’’alieleza.

Hata hivyo Mwajuma Khamis Juma na mwenzake Omar Kombo Kheir, waliziomba taasisi za watu wenye ulemavu kuwafikia shehia kwao, ili kukaa nao na kuwaelekeza.

‘’Tunaambiwa kuwa kuna haki zetu kupitia sheria na mikataba mbali mbali, sasa zitekelezwe kwa wahusika kufika shehiani kwetu ili watupe elimu,’’walishauri.

Mapema sheha wa shehia ya Makombeni Mwashum Makame Haji, aliwataka watu hao wenye ulemavu kujikusanya pamoja, na kisha kuwasili ofisini kwake.







Alieleza kuwa, kama wameshakuwa tayari kwa ajili ya kuanzisha vikundi vya ushirika wa aina yoyote, wafike kwake ili kisha kuwatafutia mtaalamu husika.

‘’Hata hapa Makombeni wapo watu ambao wana uwezo mzuri wa kuwaelimisha, sasa wajipange na kisha waje ili tuwakabidhi na kuwaelekeza aina ya ushirika na jumuia zilivyo,’’alieleza.

Katika hatua nyingine sheha huyo aliwataka viongozi wa jumuiya na vyama vya ushirika vilivyomo shehiani mwake, kuwashirikiana kwa karibu na watu wenye ulemavu.

Afisa wa watu wenye ulemavu mkoa wa kusini Pemba, ambae anakimu wilaya ya Mkoani, Mussa Seif Mussa amekiri kuwepo kwa shida hiyo, na kuahidi kufika shehiani humo.

Alieleza, hawakuwa na taarifa hiyo kwa siku zote, ingawa sasa baada ya kupokea malalamiko hayo, watajipanga ili kwenda Makombeni kukutana na watu hao.

‘’Hili ni jukumu letu la msingi la kuwapitia wenzetu wenye ulemavu ili kujua changamoto na utendaji wa shughuli zao mbali mbali,’’alieleza.

Hata hivyo Afisa huyo aliwataka watu hao wenye ulemavu wa shehia ya Makombeni, kuendelea kufuatilia vyombo vya habari, ili kujua namna ya kuanzisha vikundi hivyo.

Mratibu wa baraza la taifa la watu wenye ulemavu Mashavu Juma Mabrouk, alisema atafuatilia kwa karibu watu hao, ili kujua changamoto zao.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilipata mkopo wa shilingi bilioni 230, ambapo wizara ya Uwezeshaji ilipata shilingi bilioni 31, kwa ajili ya wajasiriamali.

Katibu Mtendaji wa baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar Ussi Khamis Debe, alisema fedha za mikopo zimekuwa na changamoto kuombwa na vikundi vya watu wenye ulemavu.

‘’Kwa mfano tumefanikiwa kuanzisha vikundi 90 vya watu wenye ulemavu kwa Unguja na Pemba, lakini ni vikundi 12 pekee vilivyopata na vyengine vilishindwa njiani,’’alieleza.

                    Mwisho       

Comments