NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WADAU wa haki jinai kisiwani Pemba, wamesema ili kupunguza matendo
ya ukatili na udhalilishaji, lazima kuwe na kifungu cha sheria, kinachowaadhibu
wazazi na walezi, watakaobainika kuwatorosha watoto wao.
Walisema, wazazi na walezi kwa sasa,
wamekuwa wakiwatorosha watoto wao, iwe wa kike au kiume, mara baada ya
kujitokeza kwa matendo hayo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi, juu ya uwepo wa wimbi kubwa la kufutwa kwa kesi za udhalilishaji,
walisema kwa sasa, kumeibuka mtindo wa baadhi ya wazazi kuwatorosha watoto wao.
Walisema, hayo hujitokeza kwa wazazi wa
upande wa mtoto wa kike, na hasa ikiwa tayari wameshachukua rushwa au
wameshaandaa mipango ya kuwafungisha ndoa.
Mmoja kati ya wanaharakati hao, Dina
Juma kutoka Jumuiya ya PEGAO, alisema wapo wazazi wamekuwa hawapendi kuendelea
na kesi za watoto wao mahakamani, hivyo njia nyepesi ili kuiua kesi hiyo ni
kumtorosha mtoto wake.
‘’Maana wanajua kuwa, mtoto aliyedhalilishwa
huwa ni shahidi nambari moja, hivyo ikiwa ataitwa mahakamani vikao vinne
hajaenda, chatano mara kesi inaweza kuondolewa, na kisha kuwafungisha
ndoa,’’alieleza.
Nae mwanaharakati Tatu Abdalla Msellem,
alisema wazazi wa upande wa mtoto wa kike, hufanya hivyo baada ya kughilibiwa
na upande wa mtuhumiwa, na wengine hufanikiwa.
‘’Kwa mtindo wa sasa, wa wazazi hasa wa
watoto wa kike wa miaka 15 hadi 17 kuwakimbiza watoto wao kwa tamaa ya fedha
ama ndoa, matendo hayo hayataondoka,’’alieleza.
Nae Afisa Mawasiliano wa TAMWA-Zanzibar
ofisi ya Pemba Gaspery Charles, alisema kama hakikuwepo kifungu kizito cha
kuwaadhibu wazazi wenye tabia hiyo, matendo hayo hayatopungua.
‘’Ifike wakati sasa kuwepo na kifungu
cha sheria, ambacho kinataja adhabu kwa wazazi, watakaochangia kesi za watoto
wao kufutwa au kuondolewa mahakamani,’’alishauri.
Nae mwanaharakati Hafidh Abdi Said,
alisema hata wazazi wa vijana wa kiume, wamekuwa wakiwakimbiza, baada ya kuona
wametenda makosa mbali mbali.
‘’Hii tabia inaweza kuondoka, ikiwa sasa
sheria itaweka wazi, kuwa, wazazi au walezi waliochangia kukimbizwa kwa kijana
(mtuhumiwa), ikiwa watawekwa ndani hadi kijana wao arudi,’’alishauri.
Aliyekuwa
Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Tedie Mchomvu, alisema alifanikiwa
kumpata mshitakiwa Khamis Juma Chumu ‘soda’ (76) mkaazi wa Mtoni wilaya ya
Chake chake, aliyembaka mtoto wa miaka 13, baada ya kukimbia na kisha
kushikiliwa kwa watoto wake.
Alisema
mpango huo, unaweza kusaidia kwa wale wazazi na walezi, wenye tabia ya
kuwaficha ama kuwakimbiza watoto wao, iwe wa kike ama kiume, ili wasiendelee na
kesi mble ya vyombo vya sheria.
Wakili
wa kujitegemea Pemba Zahran Mohamed Yussuf, alisema haoni mantiki kwa vyombo
vya ulinzi na usalama, kuwashikiliwa watu wengine kwa kosa mtu mmoja.
‘’Kwa
vile Jeshi la Polisi linajiendesha kwa mujibu wa sheria, lazima liwashikilie
wale ambao wanawatuhumu, lakini sio ndugu na jamaa wa mshtakiwa, huko ni kukiuka
haki za binadamu,’’alieleza.
Mratibu wa Dawati la Jinsia la wanawake na watoto wilaya ya Wete Hassan
Khamis anasema, njia ya kupunguza kwa wibi la kesi hizo, ni sheria kuongezewa
meno.
Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii Pemba Omar Mohamed yeye anasema,
wamekuwa wakikosa ushirikiano kwa watoto hao, wanapofikishwa mahakamani, aidha
ni kuwa wanatishwa na wale wanaowabaka au kuwalinda wapenzi wao.
Aidha wadau hao, walisema kesi nyingi ambazo huishia kufutwa ni
zile ambazo, watoto wa kike wana umri katia ya miaka 15 hadi 17, jambo ambalo
linarejesha nyuma jitihada za kupunguza matendo hayo.
Hakimu wa mahakama maalum ya kupinga udhalilishaji wilaya ya Wete Ali
Abdulrahman Ali, alisema wamekuwa wakiumisha kichwa hasa kesi za watoto wenye
umeri katia ya miaka 15 hadi 17.
“Hatuwezi kumtia hatiani mtuhumiwa kwa ushahidi wa daktari pekee
kwa sababu, cheti cha daktari kinaonesha mtoto kutendewa kitendo (ubakaji) na
sio kujulikana mtuhumiwa”, anafafanua.
Salma Hamad Omar mwenye umri wa miaka 19 mkazi wa Mzambarau Takao
anaeleza, watoto wenye umri huo hukataa kutoa ushahidi kwa sababu, hao
wanaume ni wachumba zao, hivyo wanaona shida kusema wamebakwa.
Mtoto mwe umri wa miaka 17 Maryam Faki Ali mkaazi wa shehia ya
Minungwini anaeleza, watoto wenye umri huo hawapendi kutoa ushahidi kwa sababu
huwa kuna makubaliano baina yake na mwanaume.
Takwimu za jeshi la Polisi wilaya Wete za mwaka 2020 zinaonyesha
kesi 85 za udhalilishaji ziliripotiwa, huku kesi 30 zikiwa ni kesi za
ubakaji zinazohusisha watoto kati ya mika 15 hadi 17.
Kati ya hizo kesi, kesi nne (4) tu ambazo zilitolewa hukumu, huku
17 zikfutwa katika kituo cha Polisi, kesi saba (7) zilifutwa mahakamani na kesi
mbili (2) zikiwa katika upelelezi.
Wakati mwaka 2021, kesi zilizoripotiwa zilikuwa 44, ambapo
kesi 28 zikiwa za watoto wenye umri wa miaka 15 hadi 17, ambapo ni
kesi nne (4) tu zilizotolewa hukumu kama ilikvyokuwa kwa mwaka 2020, huku
kesi 12 zikifutwa Polisi na saba (7) mahakamani na kesi tano (5) upelelezi wake
bado unaendelea.
MWISHO.
Comments
Post a Comment