NA HAJI NASSSOR, PEMBA@@@@
KIJALUBA iSAVE Zanzibar, ni mradi
jumuishi, unaolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi.
Kupitia
mradi huu, watu hao wenye ulemavu wa aina mbali mbali, utawajengea uwezo kuhusu
maisha yao wenyewe na jamii zao, kwa ujumla.
Maana, lengo
kuu hasa la mradi huu wa Kijaluba iSAVE Zanzibar, unaangazia zaidi, kukuza
uwezo wa watu hao, kwa kujenga mitazamo chanya, juu ya ushiriki wao, na
kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato.
Kipato
hicho, hasa kwa aina ya maradi huo ulivyo, ni kupitia katika vikundi vyao vya
kuweka na kukopa ‘saccos’ ambapo kwa baadhi ya maeneo, huitwa vikoba.
MBINU ZA UTEKELEZAJI WA MRADI HUO
Kwa mujibu
wa Msaidizi Afisa Mradi wa kijaluba Mohamed Salim Khamis, anaefanyia kazi zake
Pemba, anasema kwanza ni kuwawezesha watu hao kupata kipato.
‘’Lakini
jengine ni kuwezeshwa, ili wawe na ushiriki kamili katika miradi na maendeleo
ya jamii kwa ujumla, kutokana na mazingira yao,’’anasema.
Mbinu
nyingine aliyoitaja, ambayo mradi utakwenda kushughulika, ili kuhakikisha kundi
la watu wenye ulemavu wanakuza pato lao, ni kuangalia vikwazo vinavyowakatisha
tamaa.
‘’Kwa mfano,
kama jamii wanamitazamo kuwa, watu wenye ulemavu hawawezi, tutoa elimu, au kama
tutagunuda wanatengwa, tutaelezea haki zao kwa jamii yao,’’ anaeleza.
Watu hao
wenye ulemavu kupitia mradi huo wa miaka miwili, wataanzishiwa vikundi vya
kuweka na kukopa (iSAVE groups) na kuviunganisha na taasisi za kifedha.
Kumbe, hapa
baada ya kupewa mbinu za kisasa kwenye vikundi vyao vya kuweka na kukopa, kisha
wataunganishwa na tasisi za kifedha kama benki, ili sasa waweza kuomba mikopo.
Hapa Msaidizi
Afisa Mradi huo wa kijaluba Mohamed Salim Khamis, anafafanua kuwa, pamoja na
yote hayo, kundi hilo litajengewa uwezo kwenye eneo la ujasiriamali.
Walishasema
wahenga kuwa, mgagaa na upwa wala hali ugali mkavu, hapa msemo huu utasadifu,
kwa kundi la watu wenye ulemavu, maana wanagaa gaa kwenye ufukwe wa Kijaluba.
‘’Baada ya
kuanzishiwa vikundi hivyo, na kuwiva kiujasiriamali hapo watakuwa tayari sasa
kuombewa mikopo kwenye tasisi za kifedha kama PBZ, CRDB, NMB na Idara ya
Uwezeshaji,’’anafafanua.
Anasema,
walengwa wakuu wa mradi, ni watu wenye ulemavu wakiwemo watoto, wanawake,
wanaume pamoja na vijana, ambapo watajumuisha angalua asilimia 60.
Akimaanisha
kuwa, kwa mfano kila watu 10 wataokanufaika na mradi huu jumuishi, basi sita
wawe watu wenye ulemavu na wanne wale wasiokuwa na ulemavu.
‘’Kwa hiyo,
wanajamii wa wilaya ya Chake chake kwa Pemba na wilaya ya Kusini kwa Unguja,
ndio ambao watafikiwa na mradi huu, ambapo shehia za wilaya hiyo ni eneo la
majaribio,’’anafafanua.
WATEKELEZAJI MRADI
Hapa Mratibu
wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya
Pemba, Fat-hya Mussa Said, anasema, mradi unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya
shirikisho la Jumuiya za watu wenye ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’ pamoja na
TAMWA-Zanzibar.
Akaeleza
kuwa, kazi yao kubwa katika mradi huu, ni kuhakikisha kila kitakachofanywa
ndani ya mradi, basi jamii nyingine inapata taarifa kwa kule TAMWA, kuwatumia
waandishi wa habari.
‘’TAMWA
tunaguswa na haki za watu wenye ulemavu, na ndio maana tukawa washirika wa
utekelezaji wa mradi huu, ambao unafadhiliwa na Chama cha watu wenye ulemavu
cha Norway ‘NAD’, anafafanua.
Mratibu
huyo, anaona kama jamii ya wilaya ya Chake chake itajali kwa kiasi kikubwa haki
za watu wenye ulemavu, mradi huo utatekelezwa vyema.
Kumbe
anasema, kila mmoja akizijali kwa vitendo haki za ndugu yake mwenye ulemavu,
maana hakuna sheria, kanuni wala sera iliyoandikwa pahala popote, kuwabagua.
‘’Leo wapo makatibu
wakuu watu wenye ulemavu, wapo wakurugenzi, wenyeviti wa taasisi mbali mbali,
ni ishara kuwa wanauwezo mkubwa,’’anasema.
Hili
liliongezewa nguvu na Msaidizi Afisa Mradi huo Mohamed Salim Khamis, akisema
kama jamii haiwakubali watu wenye ulemavu, mradi huo unaweza kuwa mgumu.
‘’Naamini
kwa vile watu wa wilaya ya Chake chake wanajali mno haki za watu wenye ulemavu,
hata utekelezaji wa mradi huu wa Kijaluba, unaweza kuwalaini sana,’’anafafanua.
HATUA ILIYOFIKIWA
Tayari
waalimu wasimamizi wa vikundi vya kuweka na kukopa wameshapewa mbinu za kwenda
kuihamasisha jamii, na hasa kundi la watu wenye ulemavu, kuanzisha vikundi vya
kuweka na kukopa.
Mwalimu wa
mafunzo hayo Bakar Haji Bakar kutoka TAMWA-Pemba, aliwaeleza wasimamizi hao
ngazi ya shehia, wahakikishe, hata kwenye uongozi wa vikundi kipaumbele ni watu
wenye ulemavu.
‘’Kwa mfano
wale viongozi sita wa mwanzo, katika kila kikundi, watu wanne, wawe ni watu wenye
ulemavu, maana pia mradl huu unalenga kutoa fursa za uongozi kwao,’’anasema.
Kumbe mradi
huu utakapotia nanga Disemba 2024, kutoka pale ulipoanza Novemba 2022, watu
wenye ulemavu kwa wilaya ya Chake chake, wewe wameshaiva kiuongozi.
Kupitia
mradi huu wa majaribio, utaona kuna wananchi 1876, wakiwemo wanawake 1,122 na
wanaume 750, kutoka wilaya za Chake chake Pemba na Kuisni Unguja, watanufaika.
Chakuzingatia
tu ni kuwa, kila watu 60, kati ya 100, watakuwa ni wenye ulemavu mchanganyiko,
tena waliomo kwenye shehia za wilaya ya Chake chake kwa Pemba na au wilaya ya
kusini Unguja.
Watu hao,
watawezeshwa kupitia vikundi maalum vitakavyoanzishwa katika kila shehia ya
wilayani humo, ambapo kila kikundi, kitakuwa na wastani wa wanachama kati ya 25
na wasiozidi 30.
Afisa Utawala
kutoka Shirikisho la jumuiya za watu wenye ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’ kisiwani Pemba Aisha
Abdalla Juma, yeye amefurahishwa, na ujio wa mradi huo.
Anaona sasa,
utakwenda kuwaamsha watu wenye ulemavu, juu nafasi yao katika jamii, katika kujikwamua
na umaskini unaowakabili.
‘’Omba omba
sio agizo kwa watu wenye ulemavu, bali wanafanya hivyo kwa kutokujua, na ujio
wa mradi huu tunategemea sasa kundi hili la wenzetu wenye ulemavu, watajiweza
kiuchumi,’’anasema.
Kubwa,
aliigeukia jamii ya wilaya ya Chake chake, kutoa kila aina ya ushirikiano, hasa
katika kuhamasishana juu ya kushirikiana nao, katika kuanzisha vikundi hivyo.
Upande
mwengine Mwezeshaji wa vikundi vya watu wenye ulemavu ‘CRP’ Fatma Abrahman Ali wa
shehia ya Ole wilaya ya Chake chake, anaesimamia vikundi tisa, vyenye wanachama
wastani wa 25 hadi 30 kwa kila kimoja.
Katika
vikundi hivyo, kwa mfano chenye wanachama 30, ni lazima 20 wewe watu wenye
ulemavu, kwani ndio hasa malengo ya mradi husika.
‘’Kwa saa tumemaliza
mafunzo sisi waalimu wasimamizi, kisha tutakwenda kwa jamii, kuihamasisha namna
ya uundaji wa vikundi vya kuweka akiba, ili sasa wapate
kujikomboa,’’alifafanua.
Mwalimu wa
vikundi hivyo kutoka ‘SHIJUWAZA’ Fatma Abdalla Issa, anasema kutokana na
mafunzo waliokwishapatiwa, sasa wako tayari kwenda shehiani.
WALENGWA WA MRADI
Hidaya Mjaka
Ali wa shehia ya Vitongoji wilaya ya Chake chake, mwenye ulemavu wa viungo,
anasema wanausubiri kwa hamu mradi huo.
Nassra Issa
Omar wa shehia ya Wawi, mwenye ulemavu wa uoni, anasema kama mradi huo
utawafikia kwa vitendo, anaamini wimbi la watu wenye ulemavu, kuzitegemea
familia zao, litapungua.
Khamis
Mohamed Nassor wa Gombani, alisema jipya analoliona kwenye mradi huo, ni
kujumuishwa wao na wetu wenye ulemavu, kuanzia uundwaji wa vikundi na uongozi.
‘’Ni kweli
wenzetu wenye ulemavu walikuwa wakiachwa nyuma kwa muda mrefu, lakini sasa ujio
wa mradi huu nao watapa mwanga wa kujitegemea,’’anasema.
Mradi wa
Kijaluba, ni jumuishi unaolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi, kwa
kule kuwajengea uwezo kuhusu maisha yao na jamii zao.
Mradi huo
unatarajiwa, kukuza uwezo wa kundi hilo, samba mba na kujenga mitazamo chanja,
juu ya ushiriki wao, kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato.
Aidha mradi
huo ulioanza mwaka 2022, ukitarajiwa kumalizika mwaka 2024, utakwenda
kushughulikia vikwazo vinavyowarudisha nyuma, watu wenye ulemavu.
Kwa sasa
mradi huu, anatekeleza wilaya ya Kusini Unguja na Chake chake kwa Pemba, kama
eneo la majaribio, ambapo walengwa wakuu ni watu wenye ulemavu wakiwemo vijana,
watoto kwa asilimia 60 na 40 na watu wengine.
MIKATABA NA SHERIA YA WATU WENYE
ULEMAVU
Kwa mfano
kifungu cha 28 (1), (b) cha sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar, nambari 8 ya
mwaka 2022, kinabainisha haki ya kufanyakazi na ajira kwa watu hao.
Nacho kifungu
cha 31, kikasisitiza kuwa ni kosa kuwabagua, kuwadhalilisha, watu wenye ulemavu
kwa sababu ya hali zao.
Mkataba wa
kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, Ibara ya 27, unafafanua kuwa, nchi
zilizoridhia mkataba, zinalazimishwa kutambua haki za kujipatia nafasi za
kumudu maisha yao.
Ibara
ikasisitiza nchi hizo Tanzania ikiwemo, kukuza upatikanaji haki ya kufanyakazi,
ikijumuisha wale waliopata ulemavu wakiwa kazini, pamoja na kukataza ubaguzi.
Mwisho
Comments
Post a Comment