|
I |
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘’ATAKAYE muua mwenzake, basi naye anyongwe,
na kinga kuwa alikuwa na hasira isifanye kazi, yakifanyika hayo, kujichukulia
sheria mikononi itakoma,’’wanasema wahanga wa matukio hayo.
WAHANGA WANATOA RAI GANI?
Mke ambaye muume wake aliuawa
mwaka 2020 eneo la Micheweni kwa wananchi waliodaiwa kuwa na hasira, anasema
njia pekee ya kuondoa utamaduni wa wananchi kujichukulia sheria mikononi, naye
ni kuuliwa.
Kijana Issa Haji Othman wa
Mwanakwerekwe, anasema njia nyingine ya kukomesha wananchi kujichukulia sheria
mikononi, ni kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Mayasa Haji Mzee wa Chake chake,
anasema ili kukomesha wananchi kujichukulia sheria mikononi, ni wananchi
kuelezwa mifumo ilivyo ya haki jinai.
‘’Wananchi hawaelewi kwa undani,
mifumo ya haki jinai, kuanzia kesi inapokuwa Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka hadi Mahkamani pamoja na haki ya dhamana au rufaa,’’anasema.
VYOMBO VYA KUSIMAMIA HAKI JINAI VINASEMAJE?
Kamanda wa Polisi mkoa wa
kaskazini Pemba Juma Saad Khamis, anashauri, elimu zaidi itolewa ya athari ya
kujichukulia sheria mikononi.
‘’Nadhani wananchi hawajui
madhara ya kujichukulia sheria mikononi, sasa kama wataelewa, inaweza kuwa njia
moja ya kupunguza utamaduni huo,’’anashauri.
Afisa Sheria kutoka Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba Bakar Omar Ali, anasema
wananchi waelimishwe, ni maana na sheria na mifumo yake katika mahakama.
‘’Wananchi wanadhani kama vile
mtuhumiwa hana haki zake, ikiwemo dhamana au kukata rufaa, sasa yanapofanyika
haya pasi na uwelewa, hujichukulia sheria mikononi,’’anaeleza.
Mratibu wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora Pemba Suleiman Salim, anasema ili kupunguza wimbi la
wananchi kujichukulia sheria mikononi, ni kuenezwa kwa elimu ya sheria.
Sheha wa shehia ya Wawi, Sharifa
Waziri Abdalla, anasema vyombo vya ulinzi na usalama, viharakishe upelelezi wa
makosa mbali mbali, ili kupunguza hasira kwa wananchi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar
Hamad Khamis Hamad, anasema njia rahisi ya kupunguza wananchi kujichukulia
sheria mikononi, ni kuwa na kasi ya uendeshaji wa kesi za jinai.
‘’Ile tabia ya wananchi kukataa
kutoa ushahidi isiwepo, majaji na mahakimu wapungze dharura, ili kesi hizo
ziende kwa haraka na haki ipatikane,’’anashauri.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis
Ramadhan Abdalla, anashauri kuwa, kama mifumo ya uendeshaji wa kesi itafumuliwa
na kuwa rahisi zaidi, wananchi watakoma kujichukulia sheria mikononi.
‘’Inawezekana mifumo yetu ya
kuanza upelelezi, utoaji wa ushahidi, kujitetea, kukata rufaa, dhamana na kutia
wakili, pengine wananchi wanaiona ina mizunguruko, yengefumuliwa
kidogo,’’anashauri.
Aliyekuwa Mratibu wa Kituo cha
Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Zanzibar ofisi ya Pemba Safia Saleh Sultan,
anashauri kuwa, kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake, ili kuondoa wananchi
kujichukulia sheria mikononi,’’anashauri.
Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka Ali Amour Makame, anasema wananchi kufika mahakamani
kutoa ushahidi, itasaidia kuondoa changamoto hiyo.
VIONGOZI WA DINI WANASHAURI NINI?
Mratibu wa Ofisi ya Mufti Pemba,
sheikh Said Ahmad Mohamed, anasema, kama waumini watashibisha elimu ya kiroho,
inaweza kusaidia, kuondoa tabia ya kujichukulia sheria mikononi.
‘’Maana uislamu umekataza moja
kwa moja kumwaga damu, sasa kama waumini wa dini ya kiislamu watapewa elimu
hii, inaweza kusaidia jambo hilo,’’anashauri.
Mchungaji Samuel Eliyas Maganga kutoka Kanisa
la Tanzania Assembles of God ‘TAG’, anasema njia ya kuondoa tabia ya
kujichukulia sheria mikononi, ni waumini, kufungwa kimoyo na kiroho.
‘’Sisi viongozi wa dini,
tuwafunge kiimani waumini wetu, tukiwaeleza athari ya kumwaga damu na madhara
ya kuua, ambayo ni kazi halali ya Muumba,’’anashauri.
Mchungaji Benjaman Kissanga,
anasema kama viongozi wa dini watatoa hutuba zenye kukemea tabia hiyo, kila
wanapokutana na waumini wao, inaweza kusaidia.
Sheikh Mohamed Issa Kombo, anasema
waumini wa dini ya kiislamu, kama watapewa elimu ya kumjua Muumba na kazi zake,
kuna uwezekano wa kupungua matendo hayo.
WANAHARAKATI WENGINE WANAONAJE?
Mkurugenzi wa Jumuiaya ya Wasaidizi wa sheria
wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali anasema, ni wananchi
kujenga utamaduni wa kuhudhuria vikao na mikutano wanayowekewa, ili wapate njia
za kushughulikia kesi na malalamiko.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wasioona Pemba ‘ZANAB’ Suleiman Manssour anasema, njia rahisi ya kuondoa tabia
ya wananchi kujichukulia sheria mikononi, ni vyombo vya haki jinai kutenda
haki.
‘’Inatokea familia imeshauliwa
ndugu yao, kisha Hakimu anayeshughulikia kesi hiyo kwa tamaa zake anachukua
rushwa, na mtuhumiwa anaachiwa, hapo ndipo hasira za kujichukulia sheria
mikononi inapotokezea,’’anasema.
Mwakilishi wa Jimbo la Konde
Zawadi Amour Nassor, anasema njia pekee ya kumaliza tabia hiyo, ni wananchi
kujengwa kiuzalendo katika jamii.
Mratibu wa Jumuiya wa ajili ya
watu wenye ulemavu Zanzibar ZAPDD tawi la Pemba Khalfan Amour Mohamed, anasema mifumo
ya haki jinai isipowazingati wananchi wenye kipato cha chini, matendo hayo
yanaweza kuongezeka.
WATAALAMU WA AFYA AKILI WANASHAURI NINI?
Dokta Ali Yussuf, mtaalam wa
saikolojia ya binaadamu, anasema cha kufanya ni vyombo vilivyopewa mamlaka,
kushirikiana na jamii, kwenye utungaji wa sheria.
Jengine anaona ni kwa vyombo vya
kusimamia haki, wasizipindishe sheria, wakifanya hivyo jamii itawaamini na
kutoa taarifa zaidi kwenye matukio hayo.
Daktari mwengine wa saikolojia
Mtumwa Hija Mzale anasema, uwezo wa akili ya mwanadamu, ni kuvumilia kosa la
mwanzo, hivyo la pili, likitokezea hupenda kujichukulia sheria mwenyewe, na sio
vyombo kuzuia makosa.
‘’Saiokolojia ya mwanadamu
haipendi kuona kuna adhabu kali, lakini hakuna mikakati ya kuzuia makosa ya
jinai yasiotokee, hivyo wajibu huo bado upo,’’anashauri.
NINI KIFANYIKE?
Haroub Shein Hassan, anasema
uhuru wa kufanya kila mmoja apendavyo bila ya kuchukuliwa hatua, usiwepo kwani
unaweza kuzaa madhara kwa jamii.
Mayasa Himid Mjaka, wanasema vyombo
vya ulinzi na usalama, viweke mazingira ambayo ni laini na mwafaka kwa watu wa
madaraja yote katika jamii.
Kamisha wa Polisi Zanzibar Hamad
Khamis Hamad, anasema ni wananchi kupewa elimu ya sheria, na hasa ya namna ya
uendeshaji wa kesi za jinai mahakamani.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis
Ramadhan Abdalla, anasema wananchi waekelezwe juu ya haki za mtuhumiwa, mara tu
baada ya kushikiliwa, ikiwemo dhamana na rufaa.
Mratibu wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora Tanzania ofisi ya Pemba Suleiman Salim, anasema
wananchi wakifundishwa manufaa ya kutoa ushahidi mahakamani, matendo hayo
yataondoka.
RIPOTI YA UHALIFU TANZANIA KWA UPANDE WA ZANZIBAR
Ripoti ya uhalifu na makosa ya usalama
barabara ya Jeshi la Polisi Tanzania ya mwaka 2020, inaonesha kuwa wapo
wananchi 124 wameshauawa, kutokana na watu kujichukulia sheria mikononi
visiwani Zanzibar.
Uchunguzi umebainika, hao ni wa
kipindi cha miaka 10, kati ya mwaka 2011 hadi mwaka 2020, kwa mikao mitano
pekee ya Zanzibar.
Kwa idadi ya wananchi hao
waliouawa, kwa tuhma za kufanya uhalifu, ni sawa na kila mwaka, wastani wa watu
13 kuuawa visiwani humo katika kipindi hicho.
Kwa idadi hiyo, ilisababisha
punguzo la watu kutoka milioni 1,303,569 waliohesabiwa kwenye sensa ya mwaka
2012, hadi kufikia watu milioni 1,303,445.
Watu hao waliouawa kwa Zanzibar,
Mkoa wa mjini Mgharibi Unguja, ulioongozwa kwa miaka yote hiyo, na takwimu hizo
haijwahi kushuka.
Imebainika kuwa, mwaka 2011,
Zanzibar kuliripotiwa matukio manne (4), mkoa wa Mjini mgharibi pekee, uliripoti
matukio matatu (3).
Hali hiyo, iliripotiwa kutisha
zaidi katika mwaka 2017, kulikoripotiwa wananchi 26 waliouawa, ambapo kati yao,
18 walikuwa wa mkoa wa Mjini magharibi.
Kwa mwaka huo mikoa mingine ya
iliyoripoti matukio mengi zaidi, ni mkoa wa kusini Unguja, matano (5), kusini
Pemba matatu (3), na mikoa mengine kukiwa hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Mwaka 2019, ulibeba matukio 17, uchunguzi
ukaonesha matukio 12 yalikuwa mkoa wa Mjini magharibi pekee, kusini Pemba
matukio mawili (2) na mikoa mengine kukiwa na idadi sawa na tukio moja moja.
Hata mwaka 2020, mkoa wa Mjini
magharibi, ulikusanya matukio 10, ya mauwaji kwa wananchi kujichukulia sheria
mikononi, kati ya matukio yote 15 yaliyoripotiwa.
NINI CHANZO?
Hafsa
Issa Khamis Ali wa Mwanakwerekwe mkoa wa Mjini magharibi Unguja, anasema,
chanzo ni jamii kukosa maadili, huruma na kukosa utu.
Khadija Mansour Haji wa Kiwajuni wilaya ya Mjini Unguja, ambae mwaka
2019 muume wake alipoteza uhai, kwa kushambuliwa na wananchi wakati wa usiku,
anasema chanzo ni sheria kuwa lege lege za wanaoua.
Mohamed Kassim Othman wa Gulioni
wilaya ya mjini Unguja, anasema chanzo ni jamii kukosa uwelewa, juu ya
kumfikisha katika vyombo vya sheria mtuhumiwa wa aina yoyote.
Kheir Makame Haji wa Chake chake
Pemba, anasema bado jamii haijapata elimu ya athari ya kujichukulia sheria
mikononi, na ndio maana visa hivyo mkaoni humo viko juu.
Mwanakhamis Muhidin Juma wa
Mzingani Mkoani Pemba, anasema mifumo ya haki jinai, kuanzia siku ya kwanza ya
kuripotiwa kwa tukio hadi siku ya hukumu ni shida.
NYARAKA
Katiba ya Zanzibar yam waka 1984,
kifungu cha 13 kimebainisha kuwa ‘kila mtu anayo haki ya kuwa na hifadhi ya
maisha yake kwa mujibu wa sheria’.
Kifungu
hicho kifafanua kuwa, ‘kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata
hifadhi, na ni marufuku kuteswa, kuadhibiwa kinyama au adhabu zinazomdhalilisha’.
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 15 ikafafanua kuwa, ‘kila
mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru’.
Mkataba wa haki za binadamu wa
mwaka 1948 kuanzia ibara yake ya 3 hadi ya 8, imekataza kwa mtu kuteswa,
kuadhibiwa, kwani yuko huru kulindiwa.
Mkataba wa kimataifa wa haki za
kiraia na kisiasa wa mwaka 1966, ambao Tanzania uliuridhia mwaka 1976, Ibara ya
1, umeanisha haki ya kuishi, ukamilifu na usalama wa mtu.
Mwisho
Comments
Post a Comment