NA ZUHURA JUMA, PEMBA @@@@
WATU wenye ulemavu katika kijiji cha Vikinguni shehia ya Ng'ambwa Wilaya ya Chake Chake Pemba wameiomba Serikali kuwawekea dawa zao katika vituo vya afya, ili kuwasaidia katika kupunguza makali ya magonjwa yanayowasumbua.
Walisema kuwa, watu wenye ulemavu hasa wa akili pamoja na wenye kifafa wanahitaji watumie dawa kila siku ili kuimarisha afya zao, ingawa wakati mwengine hawatumii kutokana na kuzikosa dawa hizo ukilinganisha wengi wao hali zao ni duni kimaisha.
Wakizungumza na Zanzibarleo kijijini kwao walisema, dawa hizo ni tatizo katika kituo cha afya cha Vikinguni hali ambayo inawafanya wakanunue, jambo ambalo wakati mwengine wanashindwa kutokana na kukosa fedha.
"Kila siku watu hawa wanahitajia wameze dawa ili afya zao ziweze kuimarika lakini wakati mwengine tunashindwa kuwapa kwani mpaka tununue na hatuna uwezo", waliesema watu wenye ulemavu.
Nassir Suleiman Hamad alisema kuwa, wamekuwa wakipata usumbufu wakati wanapoanguka watu wenye kifafa na wenye ulemavu wa akili na wanapokwenda hospitali hukosa dawa.
"Kila siku tunapokwenda katika kituo cha afya na wagonjwa wetu hao tunaambiwa dawa hakuna, kwa hiyo tunasumbuka sana kwa sababu hatuna uwezo wa kupata dawa kwa kila siku", alieleza baba hiyo.
Kwa upande wake Maryam Ahmed Hemed alisema kuwa, kuna haja kwa Serikali kuwawekea dawa kwenye vituo vya afya ili kuondokana na usumbufu wanaoupata.
"Wakati mwengine tunakwenda hospitali kubwa kuomba dawa na ukiangalia pia ni usumbufu kwa sababu hatuna hata nauli ya kufikia huko, tunaomba tusaidiwe tunateseka", alisema.
Nae Fatma Hamad Khamis alisema kuwa, watu wenye ulemavu wa akili na wa viungo wengi wanaambatana na ugonjwa wa kifafa, hivyo kila siku wanatakiwa kumeza dawa, ingawa wakati mwengine wanashindwa kutokana na kukosa pesa ya kununulia dawa hizo.
"Wasipomeza dawa ni kama yale maradhi tunayapalilia, hivyo tunaomba tuonewe huruma kwa kupatiwa hizi dawa, ili zitusaidie", alieleza mwananchi huyo.
Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal Ali alisema, Wizara ya Afya ina mfumo wake wa kutoa matibabu katika hospitali na vituo vya Afya ngazi kwa ngazi, hivyo watu wenye ulemavu wa akili kliniki na daktari wao yupo katika hospitali ya Wilaya Vitongoji.
"Hivyo pale Vitongoji kwenye mfumo wa kuomba dawa, ikiwa tunazo tunawapatia kwa sababu wao ngazi yao wanaruhusika kutoa dawa hizo na matibabu yake", alifafanua.
Alisema kuwa, Serikali inaangalia makundi yote ingawa inatoa huduma kulingana na uwezo wa sehemu husika katika hospitali na vituo vya Afya kama ilivyo kwa vituo vya kujifungulia kwa mama wajawazito, kwamba huwezi kujifungulia kituo ambacho hakitolewi huduma hiyo, hivyo hivyo kwa watu wenye ulemavu.
Mdahamini huyo alieleza, kwa hivyo na wao matibabu yao ili yawe rahisi kwa kesi hizo, wanashauriwa wafike katika hospitali za Wilaya iliyopo vitongoji au Chake Chake kwa ajili ya kupata huduma hizo katika hali ya ubora.
MWISHO.
Comments
Post a Comment