HABIBA ZARALI, PEMBA
LICHA ya sheria ya elimu Zanzibar nambari
6 ya mwaka 1982 kufanyiwa marekebisho ya mwaka 1993, ili kuimarisha upatikanaji
wa elimu bora, lakini bado inaliliwa.
Sheria hiyo
ambayo inaonekana kukosa mashiko ya kuwadhibiti wazazi na walezi kikamilifu wasioshughulikia
watoto wasiokwenda skuli, au wanaokatisha masomo kwa kuwaozesha waume.
Baadhi ya
vifungu hivyo ni kile cha 20 (1) na 22 cha sheria ya elimu Zanzibar, kwa
kumuozesha mtoto ambae bado mwanafunzi.
Ambapo hapo
mzazi atakuwa ni mkosa na akitiwa hatiani adhabu zake kwa kosa la kwanza
anatakiwa kulipa faini isiyopunguwa shilingi 1,500 na isiyozidi 3,000.
Kosa la pili
katika sheria hiyo ni faini isiyopunguwa 3,000 na isiyozidi 5,500 ambapo kosa
la tatu atalipa faini isiyopunguwa 5,500 na isiyozidi 10,000 au kifungo
kisichozidi miezi sita au vyote viwili.
Pamoja na
sheria hii kuwa haimkatazi mwanafunzi kuoa au kuolewa kabla ya kukamilisha
elimu ya lazima, lakini kifungu cha 20 (3) kinaeleza kuwa hakuna mwanafunzi
anaesoma elimu ya lazima kuoa au kuolewa, kabla ya kukamilisha elimu hiyo.
Sheria
ikafafanua kuwa, na ikitokezea imefungwa ndoa wakati ikiwa bado ni mwanafunzi, mwanafunzi
huyo lazima afukuzwe masomoni.
WADAU/WANAHARAKATI WA ELIMU
WANASEMAJE?
Wanaharakati
na wadau mbali mbali wa elimu, wametoa kilio chao juu ya sheria hiyo ya elimu,
huku wakisema ni vizuri sheria hiyo kurekebishwa.
Mwenyekiti
wa Bodi skuli ya sekondari ya Mohamed Juma Pindua Hamdu Hassan Mohamed, anasema
sheria hiyo imeshapitwa na wakati na inahitaji kurekebishwa.
Anasema
sheria hiyo inaonekana kuwapa kiburi wazazi kwa kuwakatisha masomo watoto wao,
na kuwaozesha mapema, jambo ambalo ni kuwakosesha haki yao ya msingi.
“Sheria hii
kwa wakati ule basi ilikuwa inafaa, maana nakumbuka nilikuwa napokea mshahara
680 na ulikuwa ukitosha, lakini leo hii haina thamani kutokana na wakati uliopo,”anaeleza.
Mwanaharakati
wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji Tatu Abdalla Mselem anasema kutokana
na faini kuwa ndogo, inamfanya mzazi kutoona thamani ya kumuachia mtoto wake
kuendelea na elimu na badala yake kumuozesha mapema.
Anasema katika kifungu cha sheria hiyo ambacho
hakimkatazi mwanafunzi kuoa au kuolewa kabla ya kukamilisha elimu ya lazima, wazazi hutumia fursa hiyo na
kuwaozesha watoto mapema, kabla ya
kumaliza skuli.
“Kitendo cha
kuwaozesha watoto mapema ni kuwadhalilisha, kwani wanakosa haki zao za msingi za
kupata elimu,”anaeleza.
Mwanaharakati
Sifuni Ali Haji anasema kuwa faini hiyo ya mzazi anayotozwa ni ndogo mno, na
ndio maana ndoa kwa wanafunzi, zimekuwa zikiongezeka.
Anasema
faini ya shilingi 1,500 ni ndogo hivyo kunahitajika kukaliwa kitako na
kuangaliwa upya kwa kina ili kuweza kuifanyiwa marekebisho kulingana na wakati uliopo.
“Sheria hii
ipitiwe na ifanyiwe marekebisho katika vifungu vyote, ambavyo haviendani na
wakati tulionao,’’ anashauri.
WAALIMU
Msaidizi
mwalimu Mkuu skuli ya sekondari Uweleni Khamis Mohamed Ussi, anasema kutokana
na adhabu kuwa ndogo, imepelekea wazazi na walezi kukosa woga na kuwaozesha
watoto wao wakiwa bado wako masomoni.
Anasema
ingekuwa sheria ni kali na madhubuti yenye kwenda na wakati, na hatuwa
zikachukuliwa dhidi ya wazazi wanaowaozesha watoto wao, wimbi hilo lingepungua.
“Hivi sasa wapo baadhi ya wazazi hufanya
ujanja wa kufanya harusi sehemu nyengine kwa kuficha wasijulikane kwa lengo la
kujificha,’’anasema.
Mwalimu mkuu
skuli ya Mahuduthi Siti Sleyyum anasema marekebisho ya sheria hiyo yanahitajika
kwani wazazi wanaichukulia nafasi hiyo na wanajiamini kwa kuwa haina ukali
wowote.
“Sheria hiyo
inamkanganyiko, kwani haikutamka wazi hasa pale ilipoeleza kuwa, haimkatazi
mwanafunzi kuowa au kuolewa kabla ya kukamilisha elimu ya lazima,’’anaeleza.
Anasema ni
vyema sheria hiyo ingetamka wazi na kwenda moja kwa moja tu kuwa mwanafunzi
asiolewe badala ya ilivyozunguka zunguka.
Mwalimu Siti
Mohamed wa skuli ya Mtambile anasema wazazi ni lazima wapewe elimu, juu ya
athari ya ndoa za mapema, ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ambayo ndio
itakayoweza kuwasaidia katika maisha yao.
Anasema mbali
na kuwepo kwa mapungufu hayo ya sheria lakini wanafunzi na wao wanapaswa
kujielewa, ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
Mratibu wa Chama
chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar Ofisi ya Pemba
Fat-hiya Mussa Said, anasema kutokana na faini kuwa ndogo, ndio maana wazazi
huwakatisha watoto wao.
Aliitaka
serikali kupitia wizara ya elimu kuifanyia marekebisho ya haraka sheria hiyo
ili adhabu kali iweze kutolewa kwa wazazi watakaowaozesha watoto wao ambao bado
hawajamaliza masomo.
KIONGOZI WA DINI
Mmoja kati
ya viongozi wa dini ya kiislamu Wilaya ya Chake chake ambae hakutaka jina lake
litajwe anasema inaweza kuwa ni vigumu kwa wananchi kuona kuwa ni kosa kumuozesha mtoto ambae bado hajamaliza masomo
kwa vile haiendani na imani zao.
“Ingawa dini
ya kiislamu haijamkataza mtu kutafuta elimu, lakini wazanzibari ambao wengi wao
wanafuata imani ya dini hiyo, wanaamini mtoto ni yule ambae hajabaleghe na sio
vyenginevyo,’’alisema.
WIZARA YA ELIMU
Ofisa Mdhamini
wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, anasema sheria
hiyo imepitwa na wakati, na bado ina vifungu vinahitaji marekebisho.
Akizungumzia
kuhusiana na kesi za ndoa za utotoni anasema zinafanywa kwa usiri mkubwa bila
ya kuripotiwa na huzigunduwa pale mwanafunzi wakiwa wameshaolewa.
Hata hivyo
anasema licha ya changamoto hiyo, lakini wizara kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii madhara ya ndoa za utotoni.
Mwanasheria
wa Serikali Ali Amour Makame anasema wakati ilipotungwa sheria hiyo kiwango cha
adhabu kilichowekwa kilikua kikubwa, ingawa kwa sasa ni ndogo.
Lengo la
sheria hiyo ni kumlinda mtoto kumaliza elimu ya msingi na sio vyenginevyo,
ingawa wapo baadhi ya wazazi hufuata sheria ya dini ya mtoto anapokuwa baleghe
tu na kumuozesha.
WAZAZI/WAELZI
Mmoja kati
ya wazazi Amina Khamis wa Mkoani, ameitaka jamii kushirikiana kwa pamoja,
katika kutokomeza ndoa hizo, ili watoto waweze kupata elimu ambayo itaweza kuwasaidia katika maisha yao.
Ali Sharif
wa Chake chake, anasema ni vyema wazazi wapewe elimu juu ya athari ya ndoa za
utotoni, ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ambayo ndio itakayoweza
kuwasaidia hapo baadae.
Anasema
mbali na kuwepo kwa mapungufu hayo ya sheria lakini ni jukumu la wanafunzi
kujielewa ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
WANAFUNZI
Mwanafunzi Aisha Ali wa skuli ya sekondari Uweleni,
anasema baadhi ya wazazi na walezi huwalazimisha kufunga ndoa watoto, ambao
bado wanahitaji kupata elimu hasa ya lazima.
Wapo badhi ya wazazi wamekuwa wakiwaozesha watoto kwa
kisingizio cha tamaa za kupata kipato kupitia mahari wanayopewa.
Mwanafunzi
Abdul Juma wa skuli ya Kengeja, anasema wamekuwa wakifanya hivyo bila YA kujali
athari anazoweza kuzipata mtoto anayeolewa akiwa mwanafunzi.
mwisho
Comments
Post a Comment