NA MARYAM SALUM, PEMBA@@@@
“AMA kweli subira ni kitu cha kheir,
mwenye kusubiri hakosi”
“Kejeli, maneno mabaya, machafu, matusi ya nguoni yote
sikujali… nahakikisha nafikia lengo langu”,.
Hayo maneno
ya kijana mashuhuri anaesaka uongozi kila pembe aliejulikana kwa jila la Saada
Saleh mkaazi wa Chwale Wilaya ya Wete Pemba.
Anasimulia
kuwa, maneno hayo na kejeli za watu hayakuwa yakimridhisha, ingawa kwa vile alikuwa
na msimamo wa kutafuta basi hawakuweza kupata nafasi ya kumvunja moyo.
“Lakini niliwashindwa na wamebaki vinywa wazi,
yasiyoniridhi nilipitia kwa muda mrefu bila kugombana wala kulipiza kisasi nao
hadi nilipofikia”, anasema.
Majirani,
marafiki wa karibu na hata kwa baadhi ya ndugu wa familia walikuwa wanasema mengi,
lengo lao ni kuona hafikii kwenye malengo yake ya kuwa kiongozi.
Saada aliamini misemo mbali mbali ya kiswahili
kwamba… subra ni ngao, na pia nia njema hairogwi na ndipo alipokaza buti kuona
anapamba na adui zake kuhakikisha anafikia malengo.
Alijitolea kwenye
masuala mbali mbali ya kimaendeleo, ikiwemo vikundi vya maendeleo vya kuweka na
kukopa, jumuiya binafsi, hadi jumuia za Chama cha Mapinduzi.
Hapo ndipo sasa
alipoanza mchakato wa kugombea nafasi za uongozi kama kijana, ingawa haikua
rahisi kwa mara ya kwanza kufanikiwa.
Saada alipambana
na hali hiyo bila kukata tamaa, mwisho wa siku kuona kwamba anayafikia malengo
aliyoyakusudia ingawa sio rahisi kutokana changamoto alizokua akizipata.
Miongoni mwa
changamoto zenyewe ni pamoja na kukosa ushirikiano kwa baadhi ya watu wake wa
karibu, hasa kwenye familia, marafiki kumdharau.
Aliitwa majina
mabaya, hasa pale anapotoka kwenda kwenye shughuli zake na kusema kuwa, hana
anachokifuata isipokua uhuni, ingawa yapo mengi yamesemwa, lakini msimamo wake
ndio njia pekee iliomsaidia.
Anaeleza kuwa
changamoto zote hizo alizokumbana nazo kama kijana wa kike, zimeweza kumfungulia
milango na kufika pale anapopataka.
Saada ni msichana
mdogo lakini amepitia changamoto mbali mbali akiwa kwenye shughuli zake za
maendeleo, ingawa zilimfanya awe jasiri zaidi, mahiri, ukakamavu na kujiamini.
“Nilipitia
changamoto nyingi, lakini kutokana na subra niliyonayo sikutetereka, kwani
nilihakikisha nafikia malengo yangu, ili niondokane na utegemezi kwa wazazi
wangu, kama walivyo vijana wengine”, anasema.
HISTORIA YAKE
Saada alizaliwa
Oktoba 24 mwaka 1997 katika hospitali ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba na
alisoma elimu yake ya msingi na sekondari katika skuli ya Chwale Madenjani
kuanzia mwaka 2003 hadi kumaliza kidato cha nne mwaka 2013.
Mwaka 2017 alijiunga
na chuo cha Zanzibar College of Business Education katika fani ya manunuzi na
magavi kwa ngazi ya cheti na aliendelea na Diploma mwaka 2018 na kumaliza mwaka
2019.
HARAKATI ZAKE ZA
KUGOMBEA
Mwaka 2016 aligombea
nafasi ya Makamo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wete ambapo alishinda kwa
kupata kura 31 dhidi mwenzake aliepata kura zisizozidi tano (5) kati ya kura 37
zilizopigwa.
Mwaka 2018 pia
Saada aligombea nafasi ya Uenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa kike Pemba, Female
Youth Organiasation (PFYO) inayosimamiwa na Shirika la Action Aid na kuibuka
mshindi.
Kwa vile
subira ni ngao, kama kijana asiekata tamaa ya maendeleo, ilipofika mwaka 2020, alichukua
fomu ya kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo lake la Kojani, ingawa alikosa.
“Sijakata
tamaa, nitaendelea kupambana na itakapofika mwaka 2025 nitaingia tena jimboni
kuusaka uongozi”, anaeleza Saada.
Anafahamisha kuwa, kutokana na vijana wenzake wakike
na jamii iliyomzunguka katika jimbo lake kukosa uelewa kuhusu umuhimu wa wanawake
kwenye uongozi, basi hawakumpigia kura hata moja.
“Waliona
kama wananikomoa lakini hawajui kwamba mwanamke ndie mwenye huruma na anaeweza kuwatetea
zaidi kuliko wanaume lakini hiyo ni miongoni mwa changamoto, hivyo nitaigeuza
kuwa fursa kwangu”, anaeleza.
Anafahamisha kuwa, kukosa ubunge kwake haikua mwisho
wa kugombea nafasi nyengine, bali ilimuongezea kasi, ari na nguvu mpya kwani
baada ya hapo aligombea nafasi ya Uenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya ya Wete
na kupata kura 17 kwenye kura 46.
Hivyo hakukata
tamaa ambapo mwaka 2022 pia aligombea nafasi nyengine ya Uenyekiti wa UVCCM
Wilaya na nikafanikiwa kuibuka mshindi.
“Mwaka 2022
niligombea Uwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Wete hapo sasa ndipo nilipoamini
kwamba ‘subira huleta k heri’ kwa kujinyakulia ushindi kwa kupata kura
68 kwenye kura 113 huku mgombea wa pili akipata kura 35”, anaeleza.
Ndani ya Jumuia
ya Vijana wa kike ya ‘PFYO’ iliyopo Wete anafanya Miradi mbali mbali ya
kimaendeleo kama kujiinua kiuchumi yeye na vijana wenzake.
Ambapo aliufanya
kwa kushirikiana na Shirika la Action Aid mwaka 2017 hadi 2020 African Charter
on Democracy Election and Good Governance.
Saada hakukata
tamaa licha ya kuwa ni mtoto wa kike aliepambana
zaidi kuhakikisha maelengo yake anayafikia, hakujali changamoto za hapa na
pale.
“Hapa
nilipofikia bado sijafika tamati kwenye uongozi, huu ni mwanzo tu nitahakikisha
napambana zaidi kwenye suala la maendeleo kwa kufikia mbali zaidi, mimi na
vijana wenzangu,”anasema.
CHANGAMOTO
Miongoni mwa
changamoto ni kupewa majina mabaya, kufikiriwa maovu kwa lengo la kumkatishwa tamaa asifikie
malengo.
“Wengine
walimfikiria kwamba atakuja kuolewa na kuondoka, wengine wakasema siwezi
kuongoza kutokana na jinsia yangu kuwa ni mwanamke,’’anakumbuka.
Changamoto
nyinge ambayo anasema iko katika mfumo dume, ni wanaume kumzonga zonga, kila
eneo analoweka nia ya kugombea, ingawa kwa vile alishajua ilikuwa kazi rahisi.
MAFANIKIO
Kwake anaona
faida kubwa hadi sasa ni kupata marafiki wengi zaidi kwenye maeneo tofauti
Zanzibar, Dares-Salaam na Mikoa mengine jirani, pia kujijengea uewelewa zaidi
katika uongozi.
Kupamba na
changamoto na kujua mbinu za kisasa za kuzitatua, ambazo nyingi anasema
alizitumia kama fursa.
‘’Mtu
akikwamba uongozi ni uhuni, kwangu najiongeza uwa nisiwe muhuni, nikiambia
viongozi waongo, najipanga ili kuwabadilisha mtazamo, na nimefanikiwa kwa
kiasi,’’anasema.
Anajigamba
kuwa amekuwa mwenyeji ndani ya Chama chake cha Mapinduzi CCM pamoja na serikali,
kwa kule kujuana na viongozi mbali mbali.
Sambamba na
hayo Saada anaeleza kuwa, nafasi aliyonayo sasa si kwa nguvu zake pekee, bali
ni jitihada zake na nguvu kubwa zaidi
kutoka kwa vijana wenzake na viongozi wengine chama na Serikali kwa ujumla.
Akitoa
nasaha kwa vijana wenzake hasa wanawake waliopata kuchaguliwa kwenye uongozi, anasema
wasijione wamepata kwa ujanja wao ikawa ndio chanzo cha kufanya mambo kwa
maslahi yake mtu binafsi.
“Tusisahau
tulipokua tunaomba kura, tulikua na maneno ya busara, yenye hekma, wanyenyekevu
kwa wenzetu, hivyo utaratibu huo uwe endelevu hadi baada ya uongozi”,
anafafanua.
Aliwataka wanawake
wengine ambao hawajaingia kwenye uongozi kwa kuhofia, nafasi zipo nyingi za
uongozi kwenye chama, tawi na katika jamii.
MAMA MZAZI WA SAADA
Mpaji Shaame
Massoud ambae ni mama mzazi wa Saada anaeleza kuwa, Saada ni mtoto wake wa pili
kati ya watoto wake tisa aliokirimiwa na Mungu.
“Saada ni
mtoto wangu wa pili na anajipambania sana kuhakikisha analeta mafanikio katika
jamii yake, hivyo hakujali changamoto alizokumbana nazo,” alisema.
Mama huyo
alitoa nasaha zake kwa kijana wake kuwa, aendelee kupiga moyo konde na afanye
kazi zake kwa weledi, kujiamini ili kuhakikisha jamii inapata maendeleo.
Ali Juma
Ali, Suleiman Massoud Shaame na Hadia Omar Haji wakaazi wa Chwale Wilaya ya
Wete walisema kuwa, Saada ni msichana wanaemfahamu tangu utotoni mwake kwamba,
ni mcheshi, mchangamfu kwa wenzake na anayependa kutafuta.
“Tunamjua kuwa,
ni mkarimu, mtafutaji, mpambanaji na pia hapendi kukata tamaa mapema katika
suala la kutafuta maendeleo na hata familia yake ni nzuri”, alieleza.
Hivyo
walimtaka kuongoza nafasi yake ipasavyo, ili kukiletea maendeleo chama husika
na kujali nguvu za vijana wenzake ambao walimpatia ridhaa hiyo kwa maendeleo na
sio majungu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment