HABIBA ZARALI, PEMBA
KITUO cha Huduma
za Sheria Zanzibar ZLSC, kimeitaka jamii kisiwani Pemba, kuendelea kutoa elimu
ya sheria inayohusiana na utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani, wanayoipata
kupitia kituo hicho, ili kuifanya jamii kuishi kwa usalama na kupata haki zao.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa kituo hicho tawi la
Pemba, Safia Saleh Sultan, katika mkutano wa kutoa elimu ya utatuzi wa migogoro,
uliowashirikisha viongozi wa dini, kisiasa na wahamasishaji jamii kutoka shehia
za Njuguni na Mihogoni Wilaya ya Micheweni.
Alisema elimu inayotolewa kituoni hapo, kupitia makundi
mbalimbali ya jamii kisiwani humo, ni miongoni mwa njia wanazozifanya za
kuhakikisha wanawajengea wananchi uwezo wa kisheria ili waweze kutatuwa
migogoro kwa njia ya amani.
Alieleza kuwa, katika jamii kuna migogoro mingi ikiwemo
ya kesi za madai kama vile ya ardhi, ndoa, matunzo ya watoto, madeni, hivyo ni
vyema wakavitumia vikao vya familia, kuyamaliza.
‘’Kesi kama hizi mnapokimbilia mahakamani, kuna athari
kadhaa, moja wapo ni kupoteza muda, fedha na kuchelewa kupatikana suluhu, kwani
huwezi kufungua kesi siku moja na kukapata hukumu ni lazima ichukuwe muda,’’alifafanua.
Akitoa mada juu ya njia za kutatuwa migogoro kabla ya
kwenda mahakamani, wakili wa watoto wanaokinzana na sheria kutoka kituo hicho Pemba,
Siti Habib Mohamed, alisema njia ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya vikao vya
familia, inafaa zaidi.
Alieleza kuwa, utatuzi wa migogoro unahitaji kuwa na
usikivu mkubwa na kuwasikiliza walalamikaji, ili kuondoa dhana ya uonevu na
kupelekea kubakia kwa mgogoro, jambo ambalo halitoleta tija.
Wakili huyo, aliwafahamisha washiriki hao kuwa, kuelimisha
jamii kuwatumia wasaidizi wa sheria, wanapokumbana na changamoto za kisheria, kwa
kuepusha kupoteza gharama na muda, wakati wa ufuatiliaji wa kesi zao.
Mapema Afisa Ufuatiliaji na tathmini kutoka ‘ZLSC’
Zanzibar Khamis Haroun Hamad, aliwataka wanananchi kuepusha kuzalisha migogoro
yanayotokana na mitazamo, yao yaliyomo moyoni na machoni na badala yake wafuatilie haki zao kwa upana.
Alisema umoja na mashirikiano ni chachu ya kuleta suluhu
ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani na endapo, mtu ataweza kukosea hatuwa
moja tu katika kutatuwa migogoro inaweza kuleta thari kubwa ya vurugu.
Mmoja wa washiriki
hao Mkitu Hassan Mwalimu alikipongeza kituo hicho kwa elimu waliyiopata na
kuahidi kufikisha kwa jamii.
Alieleza kuwa, suala la kutunza amani ni jambo moja
kubwa, kwani inapochafuka, ni vigumu kuirejesha, hivyo suala la elimu hiyo ya
utatuzi wa migogoro ni jambo jema kwao.
Hamad Suleiman Said, aliahidi kuifikisha elimu hiyo
kutokana na umuhimu wake wa kufikia maendeleo ya kweli kuanzia ngazi za familia
hadi taifa.
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ kwa
kushirikiana na the foundation for civil society, kwa sasa wanaendesha mradi wa utatuzi wa
migogoro kwa njia mbadala za amani na haki.
Mwisho
Comments
Post a Comment