Alianzia nazi, genge, samaki wa
kukaanga, sasa auza nguo
NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
email:: hajipembatoday@gmail.com
‘’MIMI sasa sijioni mwanamke, najiona
kama mwanamme mwenye uwezo mkubwa, ndio maneno ya mwanzo wa mlengwa kaya
maskini Sakina Khamis Mbwana miaka 37, wa kijiji cha Tumbe Mashariki Pemba.
Nilipotaka
kujua kwanini asijifananishe na mwanamke aliyepata mafanikio, kwanza aliagusha
kicheko na kusema, ameshahama kwenye uwanawake kiuwezo, na sasa ni sawa na
mwanamme.
Nilipomng’ang’ania
sababu za kujifananisha na mwanamme, alisema ilishazoeleka na kuaminika kuwa
mwanamke hawezi kwa na mafanikio.
KABLA YA KUFIKIWA NA TASAF
Sakina kwa
bahati mbaya, mwaka 2013 alifiliwa na mume wake, aliyemuachia watoto sita,
wakati huo wakiishi kwenye nyumba ya miti na makuti.
Matunzo ya
watoto hao, anakumbuka kuyapata ndani mwezi mmoja, baada ya kufiliwa na
muumewake, ingawa kuanzia hapo, hakuna tena mchango hata wa kupata majani ya
chai kutoka kwenye familia.
Hadithi
ikawa kwake yeye ni mgagaa na upwa hali ugali mkavu, ingawa baadhi ya siku,
akiukosa hata huo mkavu kula na watoto wake sita mayatima.
Haki ya
elimu kwa watoto, ilikuwa ni ya kusua sua, mara wasimamishwe mara waruhusiwe
kutokana na kutokuwa na uhakika wa mchango hata wa shilingi 100.
Baada ya
kuondokewa na mume wangu, kazi sasa ilikuwa ni kuuza maandazi na maziwa eneo la
soko la samaki Tumbe, ingawa kipato kilikuwa kidogo.
‘’Nikilimaliza
bidhaa hizi, ilikuwa faida haizidi shilingi 4000, wakati ndani nna watoto sita,
wanaohitaji mlo wa asubuhi pekee ni shilingi 6,000 kwa siku,’’anasema.
Alikuwa
akimaliza bidhaa hiyo, miguu yake huelekea baharini kuungana na wenzake, kwenye
kilimo cha mwani ambapo kwa wakati huo, kilo mmoja mkavu ni shilingi 300.
Hata
alipojiunga kwenye kilimo cha mwani, anasema hakumbuki hata siku moja, watoto
wake waliokula wakibakisha chakula kwenye dishi.
‘’Mimi ili
nishibe vyema na watoto wangu, kuanzia asubuhi hadi jioni, ilikuwa nahitaji
shilingi 1,5000 kwa siku, ingawa nilikuwa natimiza shilingi 5000,’’anasimulia.
Sakina hakumbuki
watoto wake kuvaa nguo mpya hata siku za sikukuu, na siku moja baada ya kukosa
cha kuvaa, aliwatembeza watoto wake soko la samaki Tumbe, baada ya kukosa hata
nguo za mtumba.
‘’Wao
hawakujua kwa sababu gani, tunakwenda kutembea sokoni, badala ya eneo letu la
kusherehekea sikukuu, lakini ilitokana na kukosa nguo,’’anasilimulia.
Hakuwa na
ndoto hata siku moja, kupata chakula cha kutosha, kutimiza ada ya skuli ya
watoto wake, au kufikia sikukuu wakavaa nguo za dukani kama wenzao.
BAADA YA UJIO WA TASAF
Sakina
anakiri kuwa, hakuamini alipoitwa na sheha wake, juu ya kurodhesha majina ya
watoto wake, na taarifa nyingine za maisha, akiona kama ni mchezo.
Alikuwa na
hakika kuwa, hakuna mpango wa kunusuru kaya maskini, ambapo anaweza kulipwa fedha
na pasi na kufanya kazi.
‘’Ukishakuwa
na watoto yatima na hali yako ikiwa ya kinyonge, atakuja huyu kukuandika, yule
kukupiga picha na kisha mwisho wa siku, hakuna jambo,’’anakumbuka.
Baada ya
TASAF kuitia roho na kuitwa jina lake kwa ajili ya kupokea, hakuamini moyo,
macho na hisia zake kuwa amepata ruzuku hiyo.
‘’Siku ya
mwanzo nilipokea shilingi 48,000 na nilielezwa ni kwa ajili ya watoto, iwe
katika elimu ya skuli au huduma za afya, na hapo ndio nikaanza
kuamini,’’anasema.
Sakina ambae
yumo kwenye wale walengwa 14, 280 wa Pemba kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2019,
anakumbuka fedha hizo, hakufanya kosa na aliwanunulia vifaa vya elimu watoto
wake.
Kuanzia hapo,
watoto wake ilikuwa hawaendi skuli na sare mbovu, viatu visivyofahamika na
hakuna siku waliyorejeshwa kwa ukosefu wa michango wa skuli.
Alidumu kwa
miezi mitatu kupokea shilingi 48,000, ingawa baada ya kukiuka masharti,
alipokea ruzuku ya shilingi 36,000 kutoka TASAF.
MRADI WA KUKAANGA SAMAKI
‘’Nikiwa napokea shilingi 36,000 sasa nikamua
niende bandirini Tumbe, kununua samaki wa shilingi 10,000 kwa ajili kukukaanga
na na mafuta ya shilingi 200 na baada ya kuuza, nilipata faida ya shilingi
5000,’’anasema.
Mlengwa huyo,
kazi hiyo ilimgia gegoni sawa sawa, na kuanzia mwaka 2000, akawa ananunua
samakini wa shilingi 45,000 hadi shilingi 50,000.
‘’Huku
watoto wangu wakiwa wanakwenda skuli kama kawaida, na biashara yangu iling’aa,
na sasa hadi kufikia kujipatia faida ya shilingi 15,000 kwa siku kutoka ile
shilingi 5000 ya zamani,’’anasema.
GENGE
Hapa, baada
ya kujikusanyia faida hadi kufikia shilingi 50,000 huku akiendelea kuwahudumia
watoto wake sita mayatima, alizaa wazo la kuanzisha genge.
Genge hili
aliamua kuuza bidhaa kama tungule, bilingani, bizari, nazi ingawa halikudumu,
kutokana na kutokuwa na nafasi ya kuwepo nyumbani.
‘’Asubuhi
nafuata samaki sokoni Tumbe, wakati huo huo natakiwa nikafuatilie viungo vya
mchuzi mjini, nikaona siwezi kujigawa, hivyo baada ya muda genge
niliacha,’’anasema.
Fedha
alizoanzia genge na faida anayoendelea kuipata kwenye samaki wa kukaanga, hadi
inalifikia shilingi 20,000 sasa alizaa mradi mwengine.
Ingawa
pembeni ya miradi hii, Sakina alikuwa akiendesha mradi mwengine, wa kununua na
kuuza sabuni za karafuu, akisema mwenyewe kwa ajili ya chai ya watoto.
‘’Nilidumu
nao kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu, lakini huu ulikuwa ni baada ya saa za
kazi, lakini hata navunja kisanduku mlikuwa na shilingi 200,000,’’anasema.
MRADI WA NGUO ZA MITUMBA
Hapa, faida
ya sabuni ya shilingi 200,000 ndio alioanza kununua nguo za mitumba kutoka Kenya,
ambapo alimtuma mtu aliyekuwa kuweko kwa shughuli za uvuvi.
‘’Kwa sasa
nimeshaolewa, na mume wangu alipofika Kenya wakati anataka kurudini mwezi
Disemba mwaka 2021, ndie niliemuagiza na sasa naendelea na biashara hii hapa
kwangu,’’anasema.
Mara ya
kwanza, alipotuma shilingi 200,000 kwa bidhaa hiyo, alijipatia faida ya
shilingi 40,000 na sasa kwa mara ya pili, alituma tena shilingi 400,000 ambapo
hadi mwezi Aprili akiendelea kuuza.
MALENGO YAKE
Tayari
ameshanunua kiwanja kutoka kwa familia, na hapo baadae anajipanga kuanza
ujenzi, ili aondokane na kodi ya mlango kwenye biashara yake.
Kwa sasa anaishi
kwenye maisha ya ubinaadamu na furaha, na hasa baada ya kuwaona watoto wake
wanaendelea na masomo.
KATIBU WA SHEHA
Katibu wa sheha wa shehia ya Tumbe
Mashariki, Makame Hassan Makame, anasema wapo wananchi 20 waliomo kwenye mpango,
ambao sasa wamejiongeza.
Maana shehiani hapo, kati ya wananchi
7,675 waliofikiwa na mpango wa kunusuru kaya maskini walikuwa ni 231, ingawa
kwa sasa wanaoendelea ni 225, akiwemo Fatma Rubea Ali.
Wapo walioanzisha ushirika wa
biashara kilimo cha mboga, ufugaji vikundi vya kuweka na kukopa.
Lakini, akasema ipo miradi kadhaa
ambayo inawalenga jamii wote, kama vile ujenzi wa tuta la kinga maji, ambapo
wakulima zaidi ya 45, wamenufaika.
“Wakulima 45 walishayahama mashaba
yao kwa kuingia maji ya bahari, lakini TASAF ilianzisha mpango wa kujenga tatu
la kukinga maji, na sasa wakulima wamerudi,’’anasema.
Akaiomba TASAF, mara itakapomalizika
mpango huo kwa awamu ya kwanza, bado kwenye shehia yake, anao zaidi ya wanachi 200
wanaohitaji kunusuriwa.
MUUME WA SAKINA
Kwana hakupenda jina lake
lichapishwe, ingawa anasema mke wake sasa anamuona kama mfalme kwenye maisha
yake.
‘’Hata namma ya kumshirikisha kwa
kila jambo langu la maisha, sasa najiona liko juu, maana amekuwa mtunza fedha
na mtumiaji mzuri,’’anasema.
Kwake sasa hana wasi wasi wa huduma
za ndani, maana mke wake amekuwa akitoa zaidi ya asilimu 60 ya kukamilisha
huduma za kila siku.
TASAF
Mratibu wa TASAF Pemba Mussa Said,
anasema wapo walengwa 14, 280 kwa Pemba, ambao wanaendelea kupata fedha za
kunusuriwa na umaskini.
Walengwa hao wapo kwenye shehia 78,
ikiwemo ya Tumbe Mashariki, ambapo tayari shilingi bilioni 14. 4 zimeshwafikia.
Mtu kama Fatma, ndio hasa malengo ya
TASAF ya kumtoa mwananchi katika unyonge, na kumleta kwenye taa, ili nae aishi
maisha mazuri.
“TASAF inaorodhesha ya zaidi ya
walengwa 50,000 kutoka wastani wa walengwa 15 kila shehia, kati ya shehia 78,
ambao wamenzisha miradi ya kujikwamua.
“Mtu kama Fatma wa Tumbe, Amina wa
Mgogoni, Mfaki wa Kwale Gongo na Maryam wa Ukunjwi ambao hatuna shaka, hawawezi
kurudi tena kwenye umaskini mzito, wanafikia 50,000 kwa Pemba yote,’’anaeleza.
Mratibu Mussa anabainisha kuwa, kwa
mwaka 2014 hadi 2015 walengwa hao wa kunusuru kaya maskini, waliibua miradi ya
kijamii 41, idadi iliongozeka mwaka uliofuata, kwa kufikia miradi 84.
Mwaka 2017 hadi mwaka 2018,
walijukuta na miradi mengine ya kijamii 21, inayuhusisha upandaji miti kama
vile Makangale, uazishwaji wa vitalu na ujenzi wa matuta ya kinga maji ya
bahari Ndagoni, Kiwani, Micheweni na Tumbe.
Achia mbali idadi ya watu 50,000
waliojiwekeza wenyewe, vipo vikundi 942 vikizaa walengwa 12,000 vilivyoanzishwa,
kuanzia mwaka 2014 hadi sasa.
WANANCHI WA KAWAIDA
Fatma Hamad Mkandi, wa Tumbe anasema
fedha zilizoekezwa kunusuru kaya maskini, zimetumika vizuri kwa vile matunda
yanaoonekana.
Hassan Haji Omar, anasema
kilichobakia sasa ni tasisi nyingine kuvilea vikundi hivyo, ili walengwa wake
wasirudi tena kwenye umaskini.
‘’Kwetu sisi Sakina tumeshamuona kama
mwanamke mwenye uwezo mkubwa, sasa maana ruzuku ya TASAF aliitumia kama
inavyotakiwa,’’anasema.
Mwisho
Comments
Post a Comment