Na Salma Lusangi, ZANZIBAR:::
ASILIMIA 17 ya umeme unapotoea Zanzibar kutokana na baadhi ya watu kuunga umeme kinyume na sheria, hali ambayo inapelekea nchi kukosa mapato.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini Shaibu Kaduara alisema wanaotumia umeme kinyume na Sheria ni kosa la jinai na atakaebainika atashtakiwa kwa kosa la kuhujumu uchumi wa Nchi.
Hayo yalisemwa na Waziri huyo wakati aliposhiriki katika zoezi lililopewa jina la ''Kaduara'' ambalo limejikita katika kuwatafuta wananchi wanaojiunganishia nishati ya umeme kinyemela.
Alisema zoezi limebainika wapo wananchi wengi wanaotumiya umeme kinyume na Sheria kwa kujiunganishia majumbani, kitendo ambacho kinatia hasara kwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).
Alisema Wizara yake imeanzisha operesheni hiyo ambayo lengo lake ni kuwafungia mita ya umeme wananchi pamoja na kufanya msako wa kuwatafuta watu wanaojipatia huduma ya nishati kinyume na Sheria zilizowekwa.
Aidha, alisema operesheni imewakamata baadhi ya watu wanaoiba umeme kwa muda mrefu ambapo wamezisimamisha mita ili zishindwe kurikodi matumizi ya umeme. Alisema watu hao hawatakua salama kwasababu Wizara haitamuonea muhali mtu yeyote alibainika na kosa hilo.
''Nimezinduwa operesheni ''Kaduara'' ambayo lengo lake kupambana na watu wanaotumia huduma muhimu ya umeme kinyume na Sheria ambapo tunaweza kuwaita kuwa ni wahujumu wa uchumi''alisema.
Alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ni kuwapatia wananchi huduma ya Maji safi na salama pamoja na huduma ya nishati kwa ajili ya kurahisisha na kuyafikiya maendeleo mjini na vijijini.
Naye fundi Mkaguzi wa ZECO Juma Mussa, alisema wamebaini wapo watu wanaotumia huduma ya umeme kwa kuunganisha umeme moja kwa moja kutoka kwenye waya mkubwa wa shirika hilo huku wengi wamezifungua mita na kutengeneza njia ya wizi na hatimae kuifunga kwa supagluu.
Alisema wateja waliokamatwa watawajibishwa kwa kutozwa faini kwa muda wote waliokuwa wakifanya uhalifu huo.
“Kaduara operesheni”ni zoezi la kufunga mita ya umeme kwa wananchi pamoja na kuwasaka watu wanaojipatia huduma ya nishati kinyume na Sheria. Zoezi hilo lilizinduliwa June, 16 2022 na linaendelea hadi hapo watu watakapoacha tabia ya kuiba umeme.
Mwisho
Comments
Post a Comment