NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JAMII ya wilaya ya Chake chake Pemba, imeshauriwa kuendelea
kusaidiana, katika malezi na makuzi ya awali ya watoto, ili wakuze ubongo wao,
kwa aina ya mazingira wanayoishi.
Hayo
yameelezwa leo Januari 23, mwaka 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kupambana
na Udhalilishaji wilaya ya Chake chake, ambae pia ni Katib Tawala wilaya hiyo,
Suleiman Hamad Suleiman, kwenye siku ya pili ya mafunzo ya siku tano, ya ulinzi
na hifadhi ya mtoto, yanayofanyika ukumbi wa zamani wa TASAF, kwa ufadhili wa
UNICEF.
Alisema,
jamii bado haijaona umuhimu wa kushirikiana baina yao, katika malezi na makuzi
ya awali ya mtoto, jambo ambalo kwa baadhi ya wakati, huwapa msongo wa mawazo watoto
hao.
Alieleza
kuwa, jamii isiishie tu kwenye kuwaangalia wasikumbwe na majanga, bali sasa washirikiane
katika malezi, makuzi ya awali katika maisha yao.
‘’Niiombe
jamii ya wilaya ya Chake chake, wahakikishe wanasaidiana miongoni mwao, katika
malezi, makuzi ya awali ya mtoto, ili wakuze ubongo na kuyatawala mazingira yao,’’alifafanua.
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa kamati ya kupambana na udhalilishaji wilaya
ya Chake chake Suleiman Hamad Suleiman, amwewataka wajumbe wa kamati hiyo, kushirikiana
miongoni mwao wanapofanya kazi zao, za kutetea haki na fursa za watoto.
Akiwasilisha
mada, ya mahitaji katika maendeleo na makuzi ya awali ya mtoto, Katib wa kamati
hiyo Rashid Said Nassor, alisema jamii haielewei kua, mtoto anapokuwa tumboni
mwa mama yake, anasikia kila kitu.
Aidha alieleza
kuwa, wazazi wasiwajibu uongo watoto wao wanapowauliza maswali, kwani huwaharibu
ubongo wao na kukosa uaminifu kwao hapo baadae.
Alifafanua
kuwa, kuanzia mwaka mmoja mtoto, akiwa anapenda kuchora, kuuliza, kutembea kwa
kasi ni nafasi ya wazazi, kuwaachia kufanya hivyo, ili wazidi kujifunza.
Aliongeza
kuwa, kuanzia miaka 13 hadi 18 watoto huchukua nafasi ya kukuza maadili, kufikiria
uhuru wa kujitegemea, kuanzisha majukumu mapya katika jamii, kuwa na hisia ya
utambulisho.
‘’Jingine
katika miaka hiyo ni kuanza kujiamiani, kujifananisha na wakubwa zaidi, jambo
ambalo familia zinapaswa, kuwa makini katika malezi yao yenye maadili,’’alifafanua.
Mjumbe
wa kamati hiyo ambae pia ni Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali wilaya cha Chake
chake, Burhan Khamis Juma, alipinga suala la baadhi ya wazazi, kuwadanganya
waototo wao, ikiwa ni njia ya kuwatuliza.
Nae mjumbe
wa kamati hiyo Nassra Ali Sagafu, alisema njia nyingine ya wazazi wa kiume,
kuwa karibu na watoto wao ni kuwasindikiza wenza wao kliniki.
‘’Mtoto
akimuona baba yake eneo la kliniki au hospitali, inamsadia sana kujenga ukaribu
wa kudumu katika maisha yake,’’alifafanua.
Kwa upande
wake mjumbe kutoka ofisi ya Mufti Pemba, Abdull-taif Abdalla Salim, alisisitiza
kwa wazazi kuacha utamaduni wa kuwasemesha uongo watoto wao, ili kuwanyamazisha,
bali wawaeleze ukweli.
Katika mafunzo hayo ya siku tano, mada kadhaa
zitawasilishwa ikiwemo hifadhi ya mtoto, mikataba ya kitaifa na kikanda ya haki
za mtoto pamoja na mahitaji katika maendeleo ya awali na makuzi ya mtoto. Mwisho
Comments
Post a Comment