NA ZUHURA JABIRI, ZANZIBAR@@@@@
KATIBA
ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 21(2), inatamka wazi kuwa kila raia ana
haki ya kushiriki katika masuala ya uongozi na shughuli za kijamii bila
kuingiliwa.
Aidha, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya
Zanzibar nambari 8 ya mwaka 2022 inalinda haki za watu wenye ulemavu, kushiriki
kikamilifu katika maisha ya jamii, ikiwemo siasa.
Tanzania pia
imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) wa mwaka
2006, hatua inayothibitisha dhamira ya kitaifa ya kuhakikisha wanawake wenye
ulemavu wanapata haki sawa za kisiasa na kiraia.
Hata hivyo,
pamoja na misingi hii imara ya kisheria, uhalisia unaoonekana katika jamii ya
Zanzibar unaonesha picha tofauti kabisa.
Maana sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina jumla ya watu 215,434 wenye ulemavu,
sawa na asilimia 11.4 ya idadi yote ya watu.
Ambapo kati yao,
watu 6,843 wako katika umri wa miaka 15 hadi 65, kundi linalostahiki kushiriki
kikamilifu katika michakato ya kisiasa, ikiwemo kupiga kura na kugombea nafasi
za uongozi.
Licha ya idadi
hii kuwa kubwa, uwakilishi wa wanawake wenye ulemavu katika vyombo vya uamuzi
bado ni mdogo sana.
Kwani kwa sasa,
katika Baraza la Wawakilishi lenye jumla ya wajumbe 76, ni wanawake watatu tu
wenye ulemavu, wanaoshika nafasi.
Akiwemo Mwantatu
Mbaraka Khamis na Aza Januar Joseph wanashika viti maalum kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), huku Anna Athanas Paul akiteuliwa na Rais wa Zanzibar, kutoka
orodha ya watu kumi waliopendekezwa. Tofauti hii kubwa, kati ya idadi ya
wanawake wenye ulemavu na nafasi wanazoshika inaonesha wazi pengo kati ya haki
zilizoandikwa kisheria na utekelezaji wake halisi.
Changamoto
zinazowakabili wanawake wenye ulemavu katika kushiriki siasa ni nyingi na
zinagusa nyanja mbalimbali za maisha yao.
Moja wapo
anasema mwanaharakati za watu wenye ulemavu Pemba Hidaya Mjaka Aki, kuwam ni miundombinu
katika vituo vya kupigia kura, kwani mara nyingi haizingatii mahitaji yao.
Nyingine anataja
kuwa ni ukosefu wa njia panda (ramps), sakafu zisizo rafiki, na umbali mrefu wa
kutembea hufanya baadhi ya wapiga kura wenye ulemavu, kushindwa kufika vituoni.
Anafafanua kuwa, jingine ni changamoto za
mawasiliano, hasa kuhusu kupata taarifa rasmi zikiwemo wakati wa kuchukua fomu,
urejeshaji na masharti makuu.
Omar Haji
Mohamed asieona, anasema changamoto nyingine ni ukosefu wa vifaa vya kura kwa
maandishi ya nukta nundu (braille), vifaa vya sauti, na wakalimani wa lugha ya
alama.
Zaidi ya
changamoto za kimazingira, zipo pia changamoto za kijamii na kiutamaduni,
ikiwemo kutoonekana kama vile wanamchango kwa jamii yao.
Mitazamo hasi
kuhusu uwezo wa wanawake wenye ulemavu bado imeshamiri katika jamii nyingi za
Zanzibar.
Maana wingi
huamini kimakosa kuwa ulemavu ni sawa na kutoweza, hali inayowakatisha tamaa
wanawake wengi wenye ulemavu kuwania nafasi za uongozi.
Vyama vya siasa
navyo mara nyingi huwapuuza wanawake hawa katika michakato ya uteuzi wa
wagombea, wakiwanyima fursa za kushiriki kikamilifu.
Aneleza kuwa, aidha,
upungufu wa rasilimali kama fedha za kampeni, mafunzo ya uongozi, na programu
za ulezi (mentorship) huongeza ugumu wa safari yao ya kisiasa.
Pamoja na
changamoto hizi, zipo dalili za matumaini, maana mwezi Disemba 2024, Zanzibar
ilizindua sera mpya ya jinsia inayolenga kuhakikisha uwakilishi wa wanawake kwa
asilimia 40 katika miundo ya vyama vya siasa.
Huku ikilenga
usawa wa asilimia 50 kwa 50 kwa muda mrefu, hatua hii ni muhimu kwani inafungua
milango kwa wanawake wengi zaidi, wakiwemo wenye ulemavu.
Aidha, miradi
kama Strengthen Women-In-Leadership (SWIL) unoendeshwa na TAMWA Zanzibar, imekuwa
chachu ya mabadiliko kwa kuwapatia wanawake wenye ulemavu, mafunzo ya uongozi,
kujiamini, na ushauri wa kitaaluma.
Mifano kutoka
Tanzania Bara pia inaweza kutumika kama rejea kwa Zanzibar, maana Shirika la UN-
Women kama Women’s Leadership, Empowerment and Rights (WLER) imeonesha kuwa
pale wanawake wenye ulemavu wanapopewa mafunzo, fursa za kushiriki katika
utungaji wa sera, na msaada wa kifedha.
Kwani
imefahamika kuwa, wanaweza kugombea na kushika nyadhifa za uongozi kwa
mafanikio.
Maana Programu
hizi zinaweza kunakiliwa na kurekebishwa kulingana na mazingira ya Zanzibar,
ili kuongeza ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika uongozi.
Ili kufanikisha
ushiriki wa maana wa wanawake wenye ulemavu katika siasa, hatua za makusudi
zinahitajika, serikali ya Zanzibar inapaswa kuhakikisha michakato yote ya
uchaguzi inakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu kwa kurekebisha vituo vya
kupigia kura na vifaa vyingine muhimu.
Hata kutoa vifaa vya kura vinavyofikika kwa
wote, na kuweka wakalimani wa lugha ya alama.
Kwa upande wa vyama
vya siasa Haji Mohamed Issa kutoka ZANAB Pemba, anasema vinapaswa kutekeleza
sera za ubaguzi chanya (affirmative action), kwa kutenga asilimia maalum ya
nafasi za uongozi au uteuzi kwa wanawake wenye ulemavu.
Anasema hilo pia
ni sambamba na kuwapatia mafunzo na ulezi wa kisiasa wanawake hao.
Mashirika ya
kiraia kama JUWAUZA (Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar) na ZANAB yana
nafasi muhimu ya kuimarisha utetezi kwa kushirikiana na vyama vya siasa.
Vilevile,
kampeni za uhamasishaji wa umma ni muhimu ili kubadili mitazamo hasi, kuonesha
mifano ya wanawake wenye ulemavu waliofanikiwa, na kusisitiza kuwa ulemavu si
kikwazo cha uwezo.
Mipango
shirikishi na bajeti zinazozingatia jinsia zitahakikisha rasilimali
zinagawanywa kwa usawa na kuunga mkono wanawake wenye ulemavu katika nafasi za
uongozi.
Kwa ujumla,
wanawake wenye ulemavu ni sehemu muhimu na yenye uwezo mkubwa katika jamii ya
Zanzibar, ushiriki wao kamili katika siasa si suala la hisani bali ni haki ya
kikatiba.
Kwani zaidi ya
hapo, ni mkakati wa kuimarisha demokrasia na kuhakikisha sera na maamuzi
yanawakilisha mahitaji ya wananchi wote.
Kupitia
miundombinu rafiki, programu za uongozi, sera za ubaguzi chanya, utetezi
madhubuti, na uhamasishaji wa jamii, Zanzibar inaweza kujenga mazingira ya
kisiasa yanayompa kila raia.
Kuwezesha
wanawake wenye ulemavu ni hatua muhimu kuelekea Zanzibar jumuishi, yenye usawa
na uwakilishi wa kweli.
Mwisho




Comments
Post a Comment