NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAJUMBE wa Kamati ya kupambana na udhalilishaji wilaya ya Chake
chake, wametakiwa kuongeza nguvu katika ulinzi na hifadhi ya mtoto, ili
waendelee kuwa salama katika maisha yao.
Hayo yameelezwa
na leo Januari 22, mwaka 2026 katika ukumbi wa zamani wa TASAF Chake chake,
na Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali wilayani humo, Burhan Khamis Juma, wakati
akiyafungua mafunzo ya siku tano ya ulinzi na hifadhi ya mtoto, yaliofadhiliwa
na UNICEF.
Alisema,
nguvu za pamoja ni hatua moja kubwa, katika kuhakikisha watoto wa wilaya ya
Chake chake, wanakuwa salama katika maisha yao ya leo na baadae.
Alieleza
kuwa, kuwepo kwa kamati hiyo, iwe ni chachu kwa ulinzi na hifadhi ya watoto, na
kuendelea kushirikiana kwa karibu miongoni mwao, ili kuhakikisha watoto
hawaingii kwenye majanga.
‘’Niwaombe
sana wajumbe wa kamati hii, kuhakikisha mnakuwa na ushirikiano na nguvu za
pamoja, katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama,’’alieleza.
Katika
hatua nyingine, Afisa huyo Elimu na Mafunzo ya Amali wilaya ya Chake chake
Burhan Khamis Juma, alisema jamii, itaendelea kuwa na wajibu wa kwanza, katika
hifadhi na ulinzi wa mtoto.
Alifahamisha
kuwa, familia na jamii kwa ujumla, ndio wenye jukumu la mwanzo na kubwa, katika
kuhakikisha watoto wanakuwa salama na kukingwa na majanga.
Katika
hatua nyingine, alivikumbusha vyombo vya ulinzi na usalama vinavyofuatilia haki
za watoto, kutenda haki wanapofanyakazi zao hizo.
‘’Nivikumbushe
vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinasimamia haki za mtoto, kuhakikisha
wanatenda haki kwa watoto wanaodhalilishwa, wapate haki zao mbele ya vyombo vya
ulinzi na usalama,’’alifafanua.
Akiwasilisha
mada ya hifadhi na ulinzi ya mtoto Katibu wa Kamati ya kupambana na
udhalilishaji wilaya ya Chake chake Rashid Said Nassor, alisema wazazi kukataa
kuwapa huduma watoto wao ni aina ya udhalilishaji.
Alisema,
ijapokuwa udhalilishaji, imeshazoekeleka katika jamii, kuwa ni ubakaji, ulawiti,
ndoa za mapema na mimba za umri mdogo, lakini hata suala la kumkosesha chakula ni
ukatili.
Alieleza kuwa, kati ya watoto wa kike 20, mmoja amesharipotiwa kufanyiwa udhalilishaji katika maisha yao, ambapo kwa wanaume 10, mmoja alishapitia udhalilishaji katika maisha yao.
Aliongeza
kuwa, asilimia 71 ya watoto wa kiume na asilimia 62 ya watoto wa kike waliripoti
kupambana na udhalilishaji wa kimwili kabla ya kufikia miaka 18.
Aidha alifafanua
kuwa, utafiti unaonesha kuwa, zaidi wanawake saba kati ya 10 na wanaume sita kati
ya 10 wenye umri kati ya miaka 12 hadi 24 wameshakumbwa na udhalilishaji.
Katika
hatua nyingine aliongeza kuwa, asilimia 12.3 wanawake na wanaume 20.3 waliripotiwa
kuitwa majina mabaya na jamii, umegundua utafiti huo wa mwaka 2009 uliofanywa Zanzibar.
Mjumbe wa kamati hiyo Kassim Ali Omar, alisema bado
nguvu za pamoja na zinahitajika, ili kuhakikisha majanga yanayowagusa watoto yanapungua.
Alisema, zipo sheria mpya na kali, kanuni na miongozo
kadhaa, ambayo yanalenga kupunguza majanga hayo, ambapo kama ushirikiano haukua
nambari moja, wataendelea kudhalilishwa.
Nae Suleiman Said Salim aliomba serikali kwa
kushirikiana na wadau wake, kufanya utafiti wa kina kujua chanzo hasa cha
kuendelea kuwepo kwa matendo hayo wanayowanyima raha watoto.
Nae mjumbe Robart Migua Ndalami, aliviomba vyombo vya
habari, kupunguza madhara wakati wanaporipoti habari zao za udhalilishaji.
Akiwasilisha mada ya hifadhi ya mtoto katika sheria,
za kimataifa, kikanda na kitaifa Afisa Hifadhi na mtoto kutoka Unguja, Fatma
Maulid, alisema bado juhudi zinahitajika.
Alieleza kuwa, ni vyema kila mmoja, kujenga maslahi
bora yam toto, bila ua ubaguzi wowote, kama ilivyolelekeza mikataba na sheria
mbali mbali.
Alifahamisha kuwa, sheria zimekuja kuwapa usawa
watoto wote, wakiwemo wenye ulemavu, ingawa bado kwenye jamii, hali iko kinyume
na mitazamo ya sheria.
Katika mafunzo hayo ya siku tano, mada kadhaa
zitawasilishwa ikiwemo hifadhi ya mtoto, mikataba ya kitaifa na kikanda ya haki
za mtoto
Mwisho
Comments
Post a Comment