MIAKA 62 YA MAPINDUZI YALIYOIJENGA PEMBA KIELIMU, YAMEONDOA GIZA LA ELIMU HADI KUFIKIA MNARA WA MAARIFA
HABIBA
ZARALI, PEMBA@@@@
HAKUNA
tukio lililobadilisha mwelekeo wa maisha ya Mzanzibari kama Mapinduzi ya 12
Januari 1964.
Mapinduzi
haya yaliibadili kabisa falsafa ya maendeleo ya jamii kwa kutambua elimu kama
haki ya kila mwananchi.
Miaka
62 ya Mapinduzi matukufu Zanzibar nzima Unguja na Pemba inasimama
kifua mbele kama ushahidi hai wa Mapinduzi yaliyoamua kuwekeza kwenye akili za
watu wake.
Kwa mujibu wa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), elimu imekuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa tangu siku za mwanzo za Mapinduzi.
ELIMU KABLA YA MAPINDUZI, HISTORIA ISIYOFUTIKA
Kabla ya Mapinduzi ya 1964, sekta ya elimu Zanzibar ilikuwa dhaifu na yenye
ubaguzi mkubwa.
Watoto
wa wanyonge hawakuwa miongoni mwa wenye kuipata elimu na badala yake waliopata
fursa ya kusoma ni wachache tena wenye uwezo na mamlaka pekee.
Mapinduzi
matukufu ya mwaka 1964 yalileta mwanga mpya katika sekta ya elimu kwa
kuwaondolea wazawa minyororo ya ujinga na ubaguzi uliokuwepo awali.
Kupitia
Mapinduzi, elimu ilitangazwa kuwa haki ya kila mwananchi bila kujali asili,
jinsia au hali ya kiuchumi.
Hatua
hii iliwawezesha wazawa wengi kupata fursa ya kusoma na kujiendeleza kielimu,
jambo lililoweka msingi imara wa maendeleo ya jamii.
Aidha, Mapinduzi yalihamasisha ujenzi wa skuli nyingi za msingi,
sekondari na taasisi za elimu ya juu katika maeneo mbalimbali.
Skuli
hizo ziliwafikia wazawa waliokuwa wakiishi maeneo ya pembezoni ambao hapo awali
walinyimwa huduma za elimu.
Upanuzi
huu wa miundombinu ya elimu uliwezesha watoto wengi kuanza masomo na kutimiza
ndoto zao.
Vilevile, Mapinduzi yalileta mageuzi katika mitaala ya elimu kwa kuhakikisha
kuwa elimu inayotolewa inazingatia mazingira, utamaduni na mahitaji ya wazawa.
Elimu
ikawa chombo cha kuimarisha uzalendo, kujitambua na kujenga fikra huru miongoni
mwa wanafunzi.
Hii
iliwawezesha wazawa kujiona kuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa taifa lao bila ya
ubaguzi.
Mapinduzi pia yaliimarisha mafunzo ya walimu na kuongeza ajira katika sekta ya
elimu.
Walimu
wazawa walipatiwa nafasi ya kusomea ualimu na kuchangia katika kuwalea kizazi
kipya chenye maarifa na maadili.
Kupitia
juhudi hizi, elimu ilizidi kuwa bora na yenye tija kwa maendeleo ya jamii.
Kwa ujumla, Mapinduzi yalikuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya
elimu kwa kuwakomboa wazawa dhidi ya ujinga, umasikini na utegemezi.
Elimu
ikawa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo,
Mapinduzi yameacha alama isiyofutika katika historia ya elimu na ustawi wa
wazawa.
Katika
makala hii naangazia mafanikio ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika sekta ya elimu kisiwani Pemba.
Kabla
ya Mapinduzi , elimu ya msingi na Sekondari Pemba ilikuwa chache
sana na haikutosheleza mahitaji ya wengi, na hii iliibua haja
ya mageuzi makubwa kufikiwa kupitia mapinduzi ya 1964.
Takwimu
zinaonesha kuwa kabla ya Mapinduzi kwa upande wa kisiwa cha Pemba kulikuwa na
skuli za msingi chache, ambapo skuli za sekondari ilikuwa ni 1 pekee
ambayo iliitwa Sayyid Abdallah na baadae Fidel Castro.
Kutokana
na kuwa watoto wa wazawa hawakupata fursa ya kupata elimu hapo kabla ya
Mapinduzi ilipelekea kuwa na idadi ndogo mno ya wanafunzi waliosoma kwani
hakukuwepo na vyuo vikuu wala wataalamu.
Ali Saleh ni mmoja wa walimu wastaafu wa Pemba anakumbuka na kusema “Tulikuwa
tunafundisha wanafunzi wengi sana katika mazingira magumu mapinduzi yalipokuja,
yalitupa heshima na dira mpya ya ualimu.”
MAPINDUZI NA MAGEUZI YA MIUNDOMBINU YA ELIMU
Tangu mwaka 1964 hadi 2026 ambapo inatimia miaka 62 ya mapinduzi, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeandika historia mpya ya elimu kwa vitendo na kwa
takwimu.
Skuli za msingi na maandalizi Pemba zimefikia 113, wakati skuli za
msingi pekee ni 35, na skuli za maandalili pekee ni 47, zikiwa jumla ya skuli
hizo kufikia 196.
Kwa
upande wa skuli za sekondari kutoka skuli moja hadi kufikia skuli 96 jambo
ambalo ni faraja kubwa wa wananchi.
Kwa
mujibu wa takwimu kutoka wizara ya elimu Pemba na bajeti ya 2024/2025
jumla ya wanafunzi wote Pemba ni 201,729 wakati hapo kabla waliopata fursa ya
elimu ni wachache mno wakiwemo watoto wa mabepari na matajiri peke yao.
Kwa
upande wa wanafunzi wa sekondari ni 43,013, wanawake 23,616, wanaume 19,397
huku wanafunzi wa msingi wakiwa ni 130482, wanawake 63342 na wanaume 67140.
Wanafunzi
wa maandalizi ni 20971, wanawake 10344 na wanaume 10627, ambapo kwa wanafunzi
wa skuli za jamii (Tutu) ni 7263, wanawake 3644 na wanaume 3619.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa amewahi
kueleza“Mapinduzi yaliamua kwa makusudi kuifanya elimu kuwa msingi wa maendeleo
ya Zanzibar, hii ndiyo sababu uwekezaji wake umeongezeka kila mwaka.”
SKULI ZA GHOROFA ALAMA YA ELIMU YA KISASA YA MAPINDUZI
Moja ya mafanikio makubwa zaidi ya SMZ ni ujenzi wa skuli za ghorofa, ambao
umeleta sura mpya ya elimu Zanzibar nzima.
Mwaka
1964 hakukuwa na hata skuli moja ya ghorofa leo hadi 2026 Zanzibar nzima
imebarikiwa kuwa na skuli za ghorofa ambapo kwa Pemba zimefikia 23 huku kukiwa
na nyengine 18 ziko katika hatuwa ya ujenzi.
Skuli
hizi zimejengwa katika wilaya zote, kuanzia Mkoani, Chake chake, Wete na Micheweni
ambapo 7 zipo wilaya ya Mkoani ,5 Chake ,5 wete na 6 Micheweni.
Makamu
wa Pili wa rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla katika hotuba moja ya kielimu
alisema “Skuli za ghorofa ni mkakati wa kimapinduzi unaotuwezesha kutumia ardhi
kidogo kutoa elimu kwa watoto wengi zaidi.”
Kwa upande wao, walimu wanasema skuli za ghorofa zimeleta mabadiliko makubwa
kwani kila mmoja anapata nafasi ya kusoma sawa na mwengine.
Mwalimu
wa skuli ya Sekondari ya Makombeni Wilaya ya Mkoani Khamis Mohamed Ussi anasema
“Tuna madarasa ya kisasa, maabara na mazingira bora ya kufundishia, hili
halikuwepo miaka ya nyuma.”
WALIMU NA WATAALAMU WA ELIMU
Kabla ya mapinduzi mwaka 1964, idadi ya walimu na wataalamu wa elimu ilikuwa
ndogo sana.
Leo
Zanzibar katika kisiwa cha Pemba kina maelfu ya walimu wa maandalizi, msingi na
sekondari.
kwa mujibu wa Takwimu Wizara ya elimu Pemba walimu wa maandalizi na
msingi ni 3676, wanawake 2856 huku wanaume wakiwa 820 wakiwa ni wazalendo.
Kwa
upande wa sekondari walimu ni 1881, wanawake 847 na wanaume 1034, huku
wataalamu wa mitaala wakifikia 5 mwanamke mmoja na wanaume 4.
Kabla
ya mapinduzi hakukuwa na vyuo vikuu ,kati na uwalimu wala wahadhir ambapo kwa
sasa vyuo hivyo vipo 13, vikiwa 6 vya Serikali na 7 binafsi.
Wahadhir
wapo 162, wanaotowa fani mbalimbali, kwa upande wa wakaguzi wa elimu wapo 43,
wanawake 18 na wanaume 25.
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu Pemba Mohamed Nassor Salim anasema“Kupitia sera
za Mapinduzi, walimu wamepata mafunzo endelevu na hadhi yao imeimarika.”
ELIMU
BURE AHADI YA MAPINDUZI KWA WANANCHI
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutekeleza sera ya elimu bure kuanzia
maandalizi hadi sekondari.
Hatua
hii imeongeza uandikishaji wa wanafunzi na kupunguza idadi ya watoto waliokuwa
nje ya mfumo wa elimu.
Mzazi Amina Bakar Mohamed wa Machomane Chake Chake anasema “Leo mtoto wa
maskini anasoma sawa na mtoto wa tajiri, hili ni tunda la Mapinduzi.”
SERA, SHERIA NA MIKAKATI YA KUKUZA ELIMU
Sera ya Elimu Zanzibar inasisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto
na lazima itolewe kwa usawa bila ubaguzi wa jinsia, dini au hali ya kiuchumi.
Sera
hii inalenga kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa wote, kuanzia elimu ya
awali hadi elimu ya juu.
Kukuza
elimu ya amali na ufundi stadi ili kuandaa rasilimali watu wenye maarifa, ujuzi
na maadili mema kwa maendeleo ya taifa.
Sheria
za elimu Zanzibar zinalazimisha wazazi na walezi kuhakikisha watoto
wanapata elimu ya lazima, sambamba na kudhibiti uendeshaji wa skuli za umma na
binafsi.
Pia
sheria zinaweka viwango vya ubora wa elimu, nidhamu maskulini, haki na wajibu
wa walimu pamoja na ulinzi wa watoto katika mazingira ya skuli.
Mikakati ya kukuza Elimu Zanzibar inalenga kuboresha miundombinu ya skuli,
kuongeza idadi na ubora wa walimu, kuimarisha mitaala na matumizi ya TEHAMA
katika elimu.
Mikakati
hiyo pia inahusisha kutoa mafunzo endelevu kwa walimu, kuboresha mazingira ya
kufundishia na kujifunzia, pamoja na kushirikisha jamii na wadau mbalimbali.
Ili
kuhakikisha elimu inakuwa chombo cha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi
ndio maana bajeti ya elimu ikafikia zaidi ya Shilingi bilioni 864 kwa mwaka
2025/2026.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar Khamis Abdalla Said anasema
“Sheria na sera hizi zimeweka msingi wa elimu yenye ubora, ushindani na
inayojibu mahitaji ya maendeleo ya Zanzibar.”
WANANCHI WANAVYOSHUHUDIA MAFANIKIO YA ELIMU
Asha Omar wa Chake chake na Fatma Abdalla wa Vitongoji wanasema mabadiliko ya
elimu yanaonekana kwa macho skuli zimekaribia jamii mazingira ya kujifunzia
yameimarika fursa za elimu zimeongezeka.
Asha
Muhidini wa Micheweni anasema“Skuli za ghorofa zimekuwa fahari ya maeneo
yetu, hii ni Zanzibar mpya.”
Ali
Bakar Kombo wa Mwambe anasifia kwa furaha kuwa kwa sasa wanafunzi wanasoma bila
ya kubanana madarasani, ni faida kubwa kwa wananchi.
Mapinduzi
yamejithibitisha kupitia elimu
miaka 62 baada ya Mapinduzi, sekta ya elimu Zanzibar katika kisiwa cha Pemba
imegeuka kutoka mfumo dhaifu hadi nguzo ya maendeleo ya taifa.
MWISHO
Comments
Post a Comment