NENO ujauzito si geni katika maisha ya kila siku ya binadamu.
Kwa kawaida hali hiyo ya ujauzito, mama hupitia matatizo mengi hadi pale anapofikisha wiki 38 yaani miezi tisa ambapo ndio wakati wa kujifungua kwa kawaida ya umri wa mimba ya binadamu kiafya.
Kuumwa
mara kwa mara kichwa, tumbo, kutapika, kutojiskia hamu ya kula humkumba
mjamzito wakati mimba inapoendelea kukua ndani ya tumbo la uzazi.
Hii
inatokana na mabadiliko ya makuzi ya mtoto na mabadiliko ya afya ya
mama ambayo hubadilika kutokana na makuzi ya mimba ,uzito na mengine.
Wataalamu
wa afya wanasema makuzi ya mtoto tumboni huambatana na mabadiliko ya
afya ya mama, ama mauzi na hata baadhi ya magonjwa .
Maudhi kama kujisikia uchovu wa mwili, kutapika , hamu ya kula sana ama kutopenda kula, kuchagua ama kupenda chakula cha aina fulani , hasira , kutokuwa mchangamfu na baadhi ya kinamama kusikia aibu.
Uangalizi
wa masuala ya lishe bora , kufuatilia afya ya mama na mtoto, matunzo ya
familia wakati wa ujauzito ni jambo la muhimu.
Katika kipindi chote cha ujauzito ushiriki wa mwenza ni muhimu, kwa kulinda afya ya mama na mtoto, ingawa ndani ya miezi tisa kuna miezi mitatu ya kwanza ndiyo yenye hatari zaidi ya kuharibika ama kupata matatizo ya kiafya.
Ndio
maana, watalamu wa afya wakasisitiza kula mlo kamili, kwa usalama wa mjamzito
na mtoto wake, ambapo ni jambo la msingi kutafuta ushauri wa daktari, kulinda
usalama wa mama na mtoto.
Katika
ukuwaji na maendeleo mazuri ya ujauzito huo mchango wa baba (mume), unahitajika
kwa asilimia 100 ikiwemo kuhudhuria klinik kwa lengo la kupata taarifa kamili
juu ya maendeleo ya ukuwaji wa mimba hiyo.
Sio tu
kufahamu maendeleo, lakini pia na kujuwa changamoto zinazoweza kujitokeza na
namna ya kuweza kukabiliana nazo na kuhakikisha ukuwaji bora wa mimba
hiyo.
Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa baba ana wajibu wa kuhakikisha kuwa lishe bora, inapatikana ipasavyo kwa mke au mwenza wake anapokuwa mjamzito.
Pamoja na kuwa wapo akina baba waliowengi sasa wanajuwa umuhimu wa kuwasindikiza wenza wao kituo cha afya wakati wa ujauzito, bado wapo wingine wenye dhana tofauti na lengo lililokusudiwa.
MAMA
WAPEWA HUDUMA
Akisimulia
baada ya kumshauri mume wake kuongozana nae kituo cha afya baada ya
kujibaini na ujauzito Asha Faki Juma wa Mkoani, anasema mume wake, alikataa
huku akidai sababu kubwa ni kuhofia kupimwa Virusi Vinavyosababisha
UKIMWI (VVU) .
“Aliniambia
nikishapimwa mimi inatosha na ni sawa na alopimwa na yeye jambo ambalo
lilinitia unyonge”anasema.
Fatma
Kombo Makame wa Mwambe anasema baada ya mume wake kuongozana nae mara moja, alimwambia
hawezi kurejea tena kwani yeye ameshajiona yuko salama.
Zuhura Juma wa Chake chake anasema hufanya kazi kubwa hadi pale mumewake anapokubali kwenda nae klinik anachodai humpotezea muda katika shughuli zake za kazi.
WANAUME
Ali
Omar Makame wa Mkoani, anasema suala la kumsindikiza mke wake kituo cha afya,
halipi kipaumbele maana sie aliyebeba ujauzito,
Hassan
Mbarouk anasema kwa sasa baada ya kupewa elimu na mke wake, anamsindikiza
ingawa si mara zote.
Ali Hilali wa Mkanyageni anasema kwa vile yuko salama kiafya huenda klinik kwa kumridhisha mke wake tu na sio kwa hiari yake.
AKINA
BABA WALIOPATIWA ELIMU YA AFYA YA UZAZI
Khamis Mohamed wa Mkoani anasema kwenda pamoja klinik na mke wake hana pingamizi, kwani humsaidia kujuwa afya ya mama ili kuweza kumlinda yeye na mtoto mtarajiwa.
"Mimi
namsindikiza mke wangu, kwani kunanizidishia mapenzi kati yetu na mke
wangu na pia kunamfanya kuwa na furaha,"anasema.
Khatib
Juma wa Mbuyuni, anasema kumsindikiza mwenza wake klinik sio jambo baya, kwani
unapimwa vipimo vinavyosaidia kumlinda mtoto mtarajiwa iwapo atakuwa na
magonjwa kama virusi vya ukimwi.
Kwa
vile klinik ya uzazi hutolewa elimu na ushauri bora kwa mama, humsaidia kujuwa
jinsi ya kumtafutia huduma za lishe bora.
Akitowa mfano baada ya mke wake kupata mimba ya mwanzo Said Sharif Omar wa Kengeja, ndipo alipojuwa mabadiliko ya kimaumbile na tabia kupitia elimu aliyoipata klinik.
UTOWAJI
WA ELIMU UKOJE
Muhudumu
wa afya ngazi ya jamii wilaya ya Mkoani Raya Deyyum anasema, elimu kwa akina
baba majumbani kuhusu kuongozana na wenza wao kwenda klinik inatolewa.
Anasema
hali ya kukubali kwa wanaume kuwasindikiza wake zao klinik kwa sasa inatia moyo
ingawa bado wapo akina mama kwa mara ya kwanza hufika klinik bila ya waume zao
ingawa huwataka wanaporudisha vipimo waende na waume zao.
Mkuu wa vituo vinavyotoa huduma na tiba kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kanda ya Pemba Dokta Rahila Salim Omar anasema kwa vile wanaume ndio viongozi wa familia ni wajibu wao kujuwa elimu ya afya ya uzazi.
Anasema ni vyema baba kwenda klinik na kuelezwa na daktari ama muhudumu wa afya ana kwa ana, kwani ni rahisi kuliko kuelekezwa na mke wake huchangia kukosa amani pia.
Akigusia
matatizo yanayoweza kujitokeza iwapo baba hatokuwa na elimu ya afya ya
uzazi ni ndoa kuvunjika, kupata ufanisi mdogo wa utumishi wa uzazi wa
mpango na kupata mimba zisizotarajiwa.
Dk.
Rahila anafafanua kwamba , kwa upande wa uchunguzi wa VVU
ni vyema mke na mume kuchunguuza pamoja kwa sababu inawezekana mmoja
akawa ameambukizwa na mwengine yuko salama na VVU.
‘’Tunao wana ndoa ambao ni ‘’discordant couples’’ yaani mmoja ameambukizwa na mwengine hana VVU ‘’ na kupima pamoja ni vyema kwani kunazuia maambukizo kwa mtoto au wenza wao,’’anasema.
NI
IPI FAIDA YA BABA KUMSINDIKIZIKA MKE KLINIK
Mwenyekiti wa jumuiya ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi VVU ZAPHA+ wilaya ya Chakechake Maryam Said Abdalla, anasema moja ya faida ya baba kumsindikiza mke wake klinik ni kujua afya zao, ili kumlinda mtoto mtarajiwa.
Dokta Rahila anasema, husaidia baba kuongeza uelewa wa majukumu yake, ikiwemo lishe bora kwa mama ili mtoto tumboni akue vizuri, pamoja na kumfanya mama kuwa na furaha kwa ujauzito alionao.
Msimamizi
wa vituo vya huduma rafiki kwa vijana Pemba Fatma Hassan Khamis, anasema akina
baba wasione tabu kwenda klinik, kwani kuna vipimo ambavyo hupimwa akina mama
pekee,navyengine hupimwa pamoja ikiwemo cha virusi vya ukimwi .
DINI INASEMAJE
Sheikh Said Abdalla Nassor kutoka ofisi ya Mufti Pemba anasema, kwa dini ya kiislamu haijakataza mume kumsindikiza mke wake klinik ama katika kituo cha afya.
Anasema
Mtume Muhammad (S.A.W) amesisitiza kwa wanaume kuwaanagalia kwa huruma wanawake
na kuwasimamia, hivyo katika hali ya ujauzito amabayo anakuwa na mabadiliko ya
kimwili, mume anahitajika kuwa nae karibu.
“Mwenyezi Mungu anasema kaeni na wanawake kwa wema hivyo kuwasindikiza klinik ni miongoni mwa wema huo, kwani wanapata kupima afya zao kwa pamoja wao na mtoto pia.
Mchungaji
wa kanisa la TAG Makangale na mwangalizi upande wa Pemba, Samwel Elias
Maganga, anasema dini haijakataza mume kumsindikiza mke wake katika kituo cha
afya .
Anasema
katika bibilia kitabu cha mwanzo mlango wa pili mstari wa 18 mpaka 24,
inasema Mwenyezi Mungu alimuumba mwanamme na mwanamke, ili waishi pamoja kwa
mashirikiano ya mambo yote ikiwemo ya afya.
MIKAKATI YA SERIKALI IKOJE
Mkuu
wa vituo vinavyotoa huduma na tiba kwa watu wanaoishi na virusi vya
UKIMWI kanda ya Pemba Dokta Rahila Salim Omar, anasema miongoni mwa
mikakati ya serikali ni kutoa elimu, kuhusu wanaume kwenda pamoja na wake zao
klinik.
Anasema elimu hiyo ambayo inatolewa kupitia vituo vya afya , hospitalini na hata wahudumu wa afya ngazi ya jamii, amabao hupita majumbani.
Serikali imeanzisha mkakati wa makusudi wa ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya afya yaani ‘male involvement’ ili kusaidia akinamama na watoto, kwenye masuala ya afya na uangalizi wa familia ya afya ya mama.
Akiainisha vipaombele 10 wakati akisoma bajeti ya mwaka 2024/2025 waziri wa Wizara ya Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, ni pamoja na kupunguza vifo vya mama wajawazito kutoka 145 kwa kila vizazi hai 100,000.
Kupunguza
vifo vya watoto wachanga kutoka 28 kwa kila vizazi hai 1000.
Kwa mujibu wa malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa lengo ni kufikia vifo 12 kwa kila vizazi hai 1000 ifikapo mwaka 2030.
Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022, imebainisha kuwa, wanawake wenye umri wa kuzaa kati ya miaka 15-49 kwa Tanzania ni 14,992,288, ambapo kwa Tanzania bara ni 14,501431, wakati kwa Zanzibar ni 490,859.
Mwisho
Comments
Post a Comment