NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
UTOAJI mimba ni jambo lisilokubalika.
Lakini na hata jamii,
serikali na sheria za nchi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, linakatazwa.
Ingawa sheria kwa upande mmoja hata hizo za dini,
zinakubali, kutoa mimba, ikiwa mtaalamu wa afyua alishathibitisha, mimba hiyo
kubakia ni madhara makubwa zaidi.
Jamii zetu kumekuwa na baadhi ya wanawake na wakati
mwingine wakishirikiana na wanaume, katika utoaji wa mimba usio salama, kwa
sababu wanazozijua wao wawili tu.
Jambo hili limetajwa na wataalamu wa afya kuwa, huhatarisha
maisha yake, fuko lake la uzazi na wakati mwingine kifo.
‘’Hali hii inatokana na kuwa dini yetu ya kiislamu
pamoja na sheria za nchi haziruhusu kutoa mimba, labda kuwe kuna tatizo la
kumuhatarishia maisha,’’ anafafanua Mratibu wa Afya ya Uzazi Pemba Dk. Rehema
Abdalla Abeid.
Hivyo kwa vile wanatoa kwa matakwa yao bila kuwepo
sababu za msingi, hawaendi hospitali na hutumia njia za kienyeji, jambo ambalo
ni hatari kwa maisha yao.
Utoaji wa mimba unaweza kusababisha utasa hasa kwa
wale wanaotoa mimba nyingi au mara kwa mara, kwani hupelekea kuharibika fuko la
uzazi na hatimae hutolewa kabisa.
Kwa nini wanawake wanatoa mimba?
Dk. Rehema anasema ni kwamba, mbebaji wa mimba ile
huwa hajajipanga, hivyo hakuitarajia na ndio maana anaamua kuitoa bila kujali
athari inayoweza kumpata.
‘’Lakini mimi husema, hiyo mimba huwa ameitarajia
kwa sababu anaenda kukutana na mwanaume huku akijua hatumii uzazi wa mpango,
sasa atarajie nini kama sio mimba?,’’ alihoji.
Anasema, wengine hutoa mimba kwa kupoteza ushahidi
hasa kwa wasichana ambao hawajaolewa na wajane, kwani sio utamaduni wa jamii
yao kubeba ujauzito kabla ya kuolewa.
‘’Wanakosa elimu ya uzazi salama, hivyo wanashindwa
kujua sehemu sahihi ya kwenda na wengine wanajua ingawa wanaona aibu kwenda
hospitali,’’ anasema.
Dk. Rehema anasema, wanapokwenda hospitali huwa
tayari mimba imeshatoka na amepata madhara ambayo yanahatarisha maisha yake na
hivyo husema kuwa, ameharibu.
Wazazi na watoto wenyewe hawapo wawazi kusema
ukweli, ingawa kwa uzoefu walionao wanabaini kwamba, mwanamke huyo ametoa mimba
na kumletea madhara.
‘’Wanapokuja na wazazi wao wanasema mtoto wao
ameharibu na sisi tunatekeleza jukumu letu la kumtibu, kwani hatuwezi kujua
kama ni mwanandoa ama la,’’ anafahamisha.
Amina Hamad Ali mkaazi wa Pujini anasema, wanaotoa
mimba huwa na sababu tofauti ingawa wasio na waume wamekuwa wakitoa mimba
kiholela, jambo ambalo ni hatari.
‘’Mimba inapokuwa na matatizo unaambiwa hospitali
na madaktari ndio wanayoitoa, lakini hawa wanaobeba mimba wasizozitarajia huwa
hawajulikani, ndio maana wanatumia njia za kienyeji kutoa,’’ anaeleza.
Athari za utoaji mimba
Dk. Rehema anasema, mwanamke anaetoa mimba ana
uwezo mkubwa wa kuchanika fuko lake la uzazi, kwani hutumia madawa ya kienyeji
na vifaa visivyostaki.
Anasema, kutokana na ukali wa madawa hayo na yasiyo
na kiwango, hulisababishia fuko la uzazi madhara ikiwemo kuchunika na hatimae
kutoboka kabisa.
‘’Zana wanazotumia sio sahihi, hivyo fuko la uzazi
linaweza kutoboka na kupata tatizo jengine ikiwemo kutolewa kwa kizazi na
wakati mwengine kumsababishia kifo,’’ anafafanua.
Pia anaweza kupata saratani ya shingo ya kizazi na
ikiwa haikutibiwa mapema inaenea kwenye fuko la uzazi na hatimae kutolewa
kizazi na kumsababishia kifo pale saratani inapoenea mwilini.
Athari nyengine ni kuwa na safura, kupata matatizo
kwenye via vya uzazi kutokana na viungo vya uzazi kutokuhimili pamoja na
kutengwa na jamii.
Anasema, ingawa wanapofika hospitali hawasemi
kwamba wametoa mimba, lakini wanabaini kutokana na kuona viashiria vya bakteria
ambao ni tofauti na vya yule alieharibu.
Anasimulia kuwa, waliotoa mimba wanakuwa na dalili
ya harufu mbaya, kutokwa na maji machafu, homa kali, nemonia, hivyo wanatibiwa
kama wagonjwa walioharibu, ingawa wao wanakuwa katika hali ya hatari.
‘’Huko mitaani kuna madaktari ambao hawajasoma ndio
wanaowatoa mimba wanawake na wengine wanatumia njia za asili kwa kushauriwa na
watu tofauti, hii ni hatari kwao,’’ anaeleza.
‘’Kama hawa wasichana wanaoenda kukutana na wapenzi
wao bila kutumia kinga yeyote watarajie nini? matokeo yake anatoa mimba kwa
njia zisizo sahihi,’’ anafafanua.
Dk. Robert Shokolo akitoa mafunzo kwa waandishi wa
habari jijini Dodoma anasema, utoaji wa mimba husababisha madhara mbali mbali kama
vile, ugonjwa wa fistula, kumwagika damu, kutoboka kwa fuko la uzazi, kubakia
tishu ambazo husababisha viungo kukatwa.
Lailat Mohamed Shaali mkaazi wa Michenzani wilaya
ya Mkoani anasema, utoaji wa mimba unaweza kupoteza maisha ya wanawake wengi,
hivyo elimu inahitajika zaidi.
‘’Kwenye hichi kijiji chetu kuna msichana alibeba
ujauzito na kuutoa kwa kutumia dawa za miti shamba, alihatarisha maisha yake
kwa sababu mimba ilikuwa na miezi mitano, hivyo alifikia kunuka na kila mtu alimjua,’’
anahadithia.
Maryam Said Hamad (sio jina lake halisi) mwenye
miaka 46 mkaazi wa Fuoni Unguja anahadithia alivyohatarisha maisha yake baada
ya kutumia njia za kienyeji kutoa mimba.
Dada huyo mwenye mume na watoto wanne anaelezea,
alitoa ujauzito kwa sababu hakuwa tayari kuzaa kwa muda huo, hivyo akaamua
kuwafuata watu wake wa karibu kumsaidia dawa.
‘’Kila mmoja alinishauri dawa yake, nilianza
kutumia moja moja na ikiwa hainifai nabadilisha, hivyo nilijikuta nimetumia
dawa nyingi kutoa mimba hiyo, lakini nilikuwa hali mbaya na karibu ya nipoteze
maisha,’’ anasema.
Hakuamini kuwa, kuna siku angerudi katika hali yake
ya kawaida, kwani kwa hatua aliyofikia kipindi hicho alijutia kwa nini aliamua
kutoa mimba na kusema, ni kheri angebaki nayo kwa vile hakuwa na tatizo la
kiafya.
Kutokana na funzo alilolipata, dada huyo
anawanasihi wenzake wasitumie dawa za kienyeji na wala wasitumie njia ambazo
sio sahihi, kwani watapoteza maisha yao.
Mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe,
alimshuhudia madhara yaliyomkuta jirani ambae alitoa mimba kwa sababu tu mtoto
alienae hajafikia miaka miwili, alikuwa ni mwenye kutia huzuni.
‘’Alikonda sana, hawezi kula, muda wote anaumwa,
kwa kweli ilimfanyia shida, hivyo tutambue kuwa hili jambo ni hatari
tusilifanye na ikiwa mtu ana matatizo basi afike hospitali,’’ anaeleza.
Msaidizi Katibu Mufti Pemba Sheikh Said Ahmad
anafafanua, asili ya utoaji wa mimba ni haramu hasa baada ya kufikia miezi
minne kwani tayari mtoto huyo ameshapulizwa roho, hivyo inapotolewa maana yake
umeua nafsi.
Na unapoua kiumbe (nafsi) ni dhambi kubwa kuliko
fadhaa yeyote ambayo inaweza kuikumba dunia, hivyo kila mmoja anapaswa kujua
uzito wa dhambi hiyo kabla hajaifanya.
Suratul-Maida aya ya 32 imeeleza kuwa… ‘Mtu
ambae ataua nafsi kwa makusudi iliyokuwa haijaua, dhambi yake ni sawa na mtu
alieua watu wote duniani’.
‘’Aya hiyo inaonesha wazi kwamba, kuuwa kiumbe
kisicho na hatia ni dhambi kubwa, isipokuwa ikiwa kuna sababu ambazo
zikimtokezea mwanamke zinaweza kuhatarisha usalama wake, tena athibitishe
daktari kuwa ana tatizo,’’ anasema.
Padri wa Kanisa la Anglicana Wete Essau Mhecha
anasema, bibilia inaeleza kwenye kitabu cha mwanzo 9.6 kuwa, ‘Atakae
mwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano
wake Mungu alimfanya mwanadamu’
Padri anafafanua, maandiko hayo yanajenga msingi
kwamba uhai wa mwanadamu ni zawadi kutoka kwa Mungu, na wenye thamani, hivyo
mtu anapotoa mimba kwa makusudi ni uuaji na ni dhambi.
Nini kifanyike
Dk. Rehema aliwataka wanawake wajipange wanapotaka
kubeba mimba kwa kutumia njia za uzazi wa mpango na sio kuhatarisha maisha yao
kwa kuzitoa.
‘’Kwa vile dini yetu inakataza kufanya mapenzi
kabla ya ndoa, tujitahidi kufuata maelekezo hayo ili tusipate mimba ambazo
mwisho wake ni kuzitoa,’’ anasema.
Lailat anashauri kuacha uzinifu au watakapopata mimba
wasizitoe, kwani ni makosa na pia hawezi kujua kiumbe alichonacho kitakuwa na
faida gani katika maisha ya Duniani na Akhera.
Sheikh Said Ahmad anawataka wazazi kujikita katika
malezi ya kiislamu ambayo yatamsaidia mtoto kukua katika hali ya kujitambua na
kujizuia kujiingiza katika dhambi.
‘’Kuna wanaofanya tendo la ndoa nje ya sheria ambao
huficha aibu na wingine wana upungufu wa imani tu, kwa sababu ameshatenda
dhambi ya kwanza na baadae anajiingiza kwenye dhambi mbaya zaidi ya kuuwa
nafsi,’’ anafahamisha.
Mkufunzi wa kitaifa wa Afya ya Uzazi Mgeni Kisesa
wakati akizungunza kwenye mafunzo na waandishi wa habari jijini Dodoma mwaka
jana anaeleza, kila mwaka wanawake wa kitanzania milioni 1 hupata mimba
zisizotarajiwa, ambapo asilimia 39 huishia kwenye utoaji, huku mimba
zinazotolewa kwa njia isiyo salama zikiwa ni 405,000.
Kwa mujibu wa gazeti la habari leo la online la
Julai 13, 2023 lilieleza, kila baada ya dakika 8 mwanamke mmoja hufariki kwa
kutoa mimba, ambapo wanawake wa bara la Afrika ndio wanaoongoza.
Mtandao huo unaeleza, kila dakika moja kuna
wanawake wanne ambao wanatoa mimba kwa njia isiyo salama, ambapo wanawake
milioni 56 hutoa mimba, huku watatu kati ya wanne wapo bara la Afrika.
Katika juhudi za kutoa elimu, Afisa Programu kutoka
Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA) Zaina Abdalla Mzee anafahamisha,
walifanya utafiti na kuona kuna haja ya kutoa elimu kwa wanajamii, pamoja na
waandishi wa habari.
‘’Tuligundua
elimu hii bado haijawafikia vizuri wanawake, na ndio maana tukawataka
wanahabari watoe elimu ya satratani ya mlango wa kizazi, uzazi wa mpango,
mabadiliko ya tabia kwa vijana, ushiriki wa wanaume kwenda kliniki na wake zao,’’
anafafanua.
Inashauriwa kwamba linapomfika mwanamke tatizo kwennye
ujauzito, afike hospitali ilia pate ushauri nasaha.
MWISHO.
Comments
Post a Comment