Na Khelef Nassor
Community Forests Pemba - CFP kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Idara ya Misitu, Idara ya Mazingira,
Kamisheni ya Ardhi, viongozi wa shehia na wananchi wameanza rasmi mchakato wa
kuanzisha Mikataba ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii – CoFMA kisiwani
Pemba. Hatua hii inalenga kuweka mfumo wa ushirikishwaji wa jamii katika
usimamizi endelevu wa misitu ya mikoko.
Lengo kuu la CoFMA ni kuhakikisha misitu ya
mikoko inalindwa dhidi ya uharibifu na ukataji ovyo unaosababisha kuongezeka
kwa athari za mabadiliko ya tabianchi. Mikoko ni ngao muhimu kwa fukwe na jamii
kwani huzuia mmomonyoko wa ardhi na pia hufyonza hewa ya ukaa.
Mchakato huo umeanza kwa zoezi la kupima maeneo
ya uhifadhi, ambalo linahusisha kubaini mipaka ya shehia na kutambua maeneo
maalum ya uhifadhi na yale yatakayotengwa kwa matumizi endelevu ya jamii.
Wataalamu kutoka Kamisheni ya Ardhi wamepewa
jukumu la kuongoza zoezi hilo la upimaji, kwa kushirikiana na viongozi wa
shehia na wananchi wa maeneo husika ili kuhakikisha kila hatua inafanyika kwa
uwazi na ushirikiano wa pande zote.
Baada ya zoezi la upimaji kukamilika, hatua
inayofuata itakuwa ni utengenezaji wa ramani za maeneo hayo. Ramani hizo
zitakuwa dira ya wazi kwa jamii na wadau wote katika kutambua kwa usahihi
maeneo ya uhifadhi na maeneo ya matumizi endelevu.
Kupitia ramani hizo, jamii itakuwa na mwongozo wa
pamoja unaotambua mipaka, hivyo kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi na
kuongeza uwajibikaji wa pamoja katika kulinda misitu ya mikoko.
Mchakato wa kuanzisha CoFMA ni sehemu ya
utekelezaji wa mradi wa ZanzADAPT, unaotekelezwa na
CFP kwa kushirikiana na Community Forests International - CFI, na Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – TAMWA upande wa Zanzibar, chini ya
ufadhili wa Serikali ya Canada kupitia Global Affairs Canada.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa Uendeshaji
wa mradi wa ZanzADAPT kutoka CFP, Omar Mtarika Msellem, alisema
kuwa baada ya maeneo kutambuliwa rasmi, jamii zenyewe zitaunda sheria ndogo
ndogo za uhifadhi zitakazotumika kusimamia matumizi na kulinda mikoko.
"Hili
si jambo la CFP peke yake, bali ni mchakato unaomilikiwa na jamii wenyewe. Wao
ndiyo watakuwa wamiliki wa mikataba hii, na wao ndiyo watakaoamua sheria ndogo
ndogo za uhifadhi zitakazowaongoza," alisema Msellem.
Zoezi hili linafanyika katika shehia nne za mradi ambazo ni Kambini, Mchangamdogo, Chwale na Kiuyu, ambazo zina utajiri mkubwa wa mikoko lakini pia zinakabiliwa na changamoto za uharibifu kutokana na shughuli za kibinadamu.
Asha
Yussuf Nour, Afisa Mikoko kutoka CFP, alisema kuwa
mchakato huo umepokelewa vizuri sana na wananchi. Tangu kuanza kwake, serikali
za mitaa na viongozi wa shehia wamekuwa mstari wa mbele kutoa msaada wa kila
aina.
"Tumefarijika kuona jinsi wananchi
wanavyoshiriki. Wamekuwa wakihudhuria vikao, kutoa maoni, na hata kushirikiana
na wataalamu wa upimaji kuhakikisha kila eneo linatambulika vizuri,"
alisema Asha.
Kwa upande wake, Awesi Sharif Kombo,
Afisa Upimaji Ardhi kutoka Kamisheni ya Ardhi, alisema kuwa zoezi hili ni
msingi muhimu wa uhifadhi endelevu. "Huwezi kufanya shughuli ya uhifadhi
bila kutambua mipaka ya maeneo. Hii ndiyo hatua ya kwanza ya kuweka msingi wa
ulinzi wa rasilimali zetu," alifafanua.
Wanajamii wenyewe pia wameonyesha furaha yao kwa
kushirikishwa moja kwa moja katika mchakato huo. Walisema hatua hiyo imeongeza
uelewa juu ya thamani ya mikoko na nafasi yao katika kuhakikisha misitu hiyo
inalindwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Sharif
Juma Omar, Mwenyekiti wa kamati ya doria ya Kiuyu Minungwini, alisema
kuwa ushirikishwaji wa jamii ni hatua kubwa. "Hapo zamani tulikuwa
tunaona mikoko ni miti tu ya kukata mbao. Lakini sasa tunafahamu thamani yake
katika kulinda mazingira yetu na maisha yetu," alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa mikoko si tu kinga ya
mazingira bali pia fursa ya kiuchumi. Wanawake wanaoshiriki katika vikundi vya
ufugaji wa samaki na biashara ya uvunaji wa asali walieleza matumaini yao kuwa
uhifadhi wa mikoko utawasaidia kupata kipato endelevu.
Zoezi la CoFMA pia limechukuliwa kama jukwaa la
kujenga mshikamano wa kijamii. Watu kutoka makundi mbalimbali wanashirikiana
kwa karibu zaidi, jambo linaloongeza mshikamano na mshirikiano katika jamii.
Viongozi wa shehia walipongeza CFP na washirika
wake kwa kuhakikisha serikali, jamii na taasisi binafsi zote zinashirikishwa.
Walisisitiza kuwa kwa mara ya kwanza wananchi wanaona matokeo ya kushirikishwa
katika maamuzi yanayohusu rasilimali zao.
Mradi wa ZanzADAPT unaendelea kuonesha kuwa
suluhu za kimazingira zinaweza kufanikishwa kupitia mshirikiano kati ya
serikali, jamii na wadau wa maendeleo. Ushirikiano huu wa kuanzisha CoFMA
unatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa na maeneo mengine ya Zanzibar.
Kupitia mchakato huu, Pemba inatarajiwa kuweka
historia chanya ya usimamizi wa misitu ya mikoko. Hatua hii inatoa matumaini
kwamba vizazi vijavyo vitarithi rasilimali zilizo salama, mazingira yaliyo
imara, na jamii zilizo na mshikamano katika kulinda na kuendeleza utajiri wa
asili wa visiwa vya Zanzibar.



Comments
Post a Comment