NA MARYAM SALUM, PEMBA@@@@
Wito huo ulitolewa August 28, 2025 na Mkurugenzi wa Baraza la Mji la
Manispaa ya Chake Chake, Shida Kombo Hamad, kwa niaba ya mkuu wa wilaya
ya Chake Chake, wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wanahabari hao, juu
ya kuripoti habari za uchaguzi, katika ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar
‘ZBC’ Pemba.
Alisema kuwa vyombo vya habari ni taasisi muhimu kwa jamii
nchini, vinavyotoa huduma ya kuhabarisha, ambayo ni haki ya msingi raia kama
inavyotamkwa kwenye katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 18.
Alieleza kuwa, dhima ya sekta ya habari ni kuelimisha na
kuburudisha jamii, ambapo kwa upande wa utangazaji, sekta ya habari inahudumiwa
na vyombo vya habari ambavyo ni redio, television na mitandao ya kijamii, na sio
kuwa sehemu ya uchafuzi wa amani.
"Hivyo ni wajibu wetu na ni jukumu la kila mmoja,
kuhakikisha tunazingatia maadili ya habari, wakati wa kutekeleza shughuli zetu
za utangazaji," alisema.
Akizungumzia sula la utolewaji wa leseni kwa vyombo vya
habari, alisema kuwa Tume ya Utangazaji Zanzibar ‘TUZ’ ndio yenye dhamana hiyo,
pamoja na kupanga na kusimamia masafa ya utangazaji, kudhibiti shughuli za
watangazaji na maadili yao,’’alifafanua.
"Ni kawaida kwa vyama vya siasa kutumia vyombo vya
habari katika kueleza sera, ilani na ahadi za zao, ili kufahamika na wananchi,
hata hivyo vyombo vya habari havipaswi kusahau majukumu yao ya msingi,’’alifafanua
Mkurugenzi huyo.
Hivyo aliwataka waandishi wa habari kuacha propaganda za
chuki, na badala yake kuripoti taarifa kwa usahihi, na kuepuka kuingiza nchi
kwenye vurugu.
Mapema Mrajisi Tume ya Utangazaji Zanzibar Ali Ayoub, wakati
akimkaribisha mgeni huyo rasmi, alisema kuwa waandishi wa habari ni wadau
wakubwa, katika kuripoti taarifa za uchaguzi, ndio maana Tume ya Utangazaji,
imeona ipo haja kutoa taaluma kwao.
Afisa Sheria kutoka Tume ya Utangazaji Zanzibar, Khadija
Mabrouk Hassan, akiwasilisha mada kuhusu kanuni za huduma za utangazaji wakati
wa uchaguzi, alifahamisha kuwa mtoaji wa huduma ya maudhui ya utangazaji,
ahakikishe kuwa taarifa zote zinaripotiwa kwa usahihi na bila upendeleo.
Aliwatakata waandishi wa habari, kutoripoti taarifa kwa
mtazamo binafsi, ili kupendelea upande wowote wa kisiasa katika vipindi vyake,
ili kuepusha uvunjivu wa amani.
Nae Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania ‘TCRA’ Andrew Kisaka, akiwasilisha mada muongozo wa utangazaji kuhusu
machafuko na majanga, alieleza kuwa zaidi ya watu1,000 walipoteza uhai na
wengine 600,000 kupoteza makazi nchini Kenya mwaka 2007.
Aidha mwaka 2011 nchini Nigeria, zaidi ya watu 800
walipoteza uhai katika machafuko yaliyotokea katika kipindi cha uchaguzi.
Hivyo ni muhimu kwa mwandishi wa habari kuepuka kusambaza taarifa
za uongo, kuchochea migogoro au kutoa mahukwaa kwa wale wanaochochea migogoro
au vurugu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment