IMEANDIKWA NA FATMA HAMAD, PEMBA@@@@
WANANCHI wametakiwa kuwatumia wasaidizi wa Sheria waliomo shehiani mwao,
ili kupatiwa msaada wa kisheria kwalengo la kupata haki zao za msingi.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Rais Katiba Sheria na
Utawala bora Zanzibar Salma Suleiman wakati akizungumza na wananchi na
wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Msuka, katika mkutano maalumu wa kuijengea
uwelewa jamii juu ya masuala ya kisheria, uliofanyika Skuli ya Sekondari Msuka
wilaya yaMicheweni Kaskazini Pemba.
Alisema Wananchi waliowengi wamekua wakipata matatizo mbali mbali ikiwemo
migogoro ya ndoa, Ardhi pamoja na utelekezwaji, lakini bado uwelewa wa
kuwatumia wasaidizi wa Sheria katika kuzitatua changamoto hiyo.
Alisema kazi kubwa ya Wasaidizi wa Sheria ni kuhakikisha wanatoa msaada wa
kisheria katika Jamii, hivyo ni mihimu kwa jamii kuwatumia wasaidizi hao, ili
kupata ufumbuzi wa changamoto.
Aidha alieleza kua, kwa vile kazi ya Idara ni kutoa msaada wa kisheria,
watahakikisha wanaweka Msaidizi wa Sheria kila shehia ili kuinusuru jamii na
migogoro.
Mapema Afisa Sheria kutoka Tume ya Haki za Binadamu Ofisi ya Pemba Muhamed
Massoud Said aliwasisitiza wananchi kuwatumia watoa msaada wa kisheria kujifunza
baadhi ya Sheria ambazo zinawaongoza katika nchi ili waweze kuzifahamu.
Alisema kujifunza sheria itasaidia kujiepusha na vitendo vitakavyopelekea uvunjifu
wa haki za binadamu.
Alisisitiza kwamba, kufanya kosa kwa kutojua sheria haimzuii mtu kutohukumiwa,
hivyo ipo haja ya kila mmoja kujifunza Sheria kufahamu wajibu nahaki yake, ili
kijikinga na vitendo viovu ikiwemo uvunjifu wa amani hasa katika kipindi hiki
cha kuelekea Uchaguzi mkuu.
Aidha aliwataka wananchi hao kuwamstari wa mbele ili kuhakikisha wanatoa
taarifa pindi watakapoona kunaviashiria vya uvunjifu wa haki za binadamu.
‘’Wananchi msikae kimya na nyinyi ni sehemu ya serikali, toeni taarifa
iwapo mnanyimwa ama kuvunjiwa haki zenu za msingi ambazo mnastahiki muzipate
kama binadamu,’’alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Msaada wa kisheria Pemba Bakar Omar Ali
alisema, lengo la mkutano huo ni kuwahamasisha wananchi kuwatumia fursa
wasaidizi wa Sheria waliopo katika kuripoti malalamiko yao yaweze kusikika na
kupatiwa ufumbuzi kiurahisi.
Nao wananchi wa Shehia hiyo wameufurahia ujio wa wanasheria hao kijiji
kwao, huku wakiiomba serikali ya wilaya kuendelea kuwashughulikia wanafunzi
ambao wanaacha masomo na kuingia katika ndoa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment