NANA HAJI NASSOR, PEMBA
WANANCHI wa shehia ya Wawi wilaya ya Chake
chake, wametakiwa kuitumia fursa ya kuhudhuria mkutano maalum wa elimu ya
kisheria, ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, unaotarajiwa
kufanyika asubuhi hii shehiani humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Divisheni
ya Idara hiyo Pemba Bakari Omar Ali, alisema mkutano huo, ni maalum kwa ajili
ya wananchi hao, ili kuwapa elimu na msaada wa kisheria bila ya malipo.
Alisema, mkutano huo ambao utafanyika eneo la Kwa gerei
Wawi, ni sehemu ya utendaji wa kazi wa kawaida wa Idara hiyo, katika
kuhakikisha jamii inapata muelekeo wa kutambua haki na wajibu wao kisheria.
Alieleza kuwa, zipo njia kadhaa za wananchi kujua haki zao
za kisheria, moja wapo ni kuwapelekea wataalam wa sheria ndani ya shehia, na
kuelezea changamoto zao.
‘’Mkutano huu ambao unatarajiwa kufanyika asubuhi hii shehia ya Wawi ni maalum, ili kuona wanapata uwelewa, lakini pia kuuliza na kutoa changamoto zao za kisheria,’’alifafanua.
Mkuu huyo wa Divisheni ya Idara ya Katiba na Msaada wa
kisheria, alisema watalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, watendaji wa Tume
ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora pamoja na wasaidizi wa sheria wa Chake
chake watakuwepo.
‘’Wataalamu hawa watahakikisha kila mwananchi atakaefika
kwenye mkutano wa leo, na akiwa anajambo lolote la kisheria atauliza na kupata
jawabu papo hapo,’’alisema.
Katika hatua nyingine, aliwahimiza wananchi hao, kuitumia
fursa hiyo, kwani kinyume chake wakiwafuata baadhi ya wanasheria watahitaji
fedha nyingi, ili kusikiliza na kuchambua changamoto zao.
Mapema sheha wa Wawi Khamis Mohamed Khamis, alisema
matayarisho yote kwa ajili ya mkutano huo mkubwa wa wazi, yamekamilika.
Alisema, baada ya kupokea taarifa hiyo kutoka Idara ya
Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, alishakutana na kamati yake, na
wameshatoa taarifa kwa wananchi.
‘’Niliwatumia wajumbe wangu kutoa taarifa kwa wananchi wa
makundi kadhaa kama ya watu wenye ulemavu, watumishi wa umma, wakulima, waalimu
wa vyuo vya qur-an na wanamichezo,’’alifafanua.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake
chake ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, alisema hiyo ni heshima kubwa kwa Idara
ya Katiba na Msaada wa Kisheria kuwapa fursa ya kuandaa mkutano huo.
Msaidizi wa sheria shehia ya Wawi, Fatma Hilali Salim,
aliwakumbusha wananchi wa shehia hiyo, kufika kwa wingi kwenye mkutano huo, ili
kupata ufafanuzi wa changamoto zao za kisheria.
Mjumbe wa sheha Nassor Rashid Said na Katiba wa sheha Sham
Haroub Said, waliipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, kwa uamuzi
wake wa kuandaa mkutano huo.
Mikutano kama hiyo, inatarajiwa kufanyika katika shehia za
wilaya ya Mkoani, Wete na Micheweni.
Mwisho

Comments
Post a Comment