NA ZUHURA JUMA, Dar-Es-Salaam@@@@
ELIMU ya malezi na makuzi bora ya watoto inahitajika katika jamii ili kuhakikisha wazazi wanalea watoto wao katika malezi yaliyobora.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa wa hoteli ya Jamirex jijini Dar-Es-Salaam, Mtaalamu wa Sayansi ya Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto nchini Tanzania David Gisuka alisema, kuna baadhi ya wazazi wana tabia ya kushughulikia zaidi kazi zao na kuwaacha watoto wao wapweke, hali ambayo inawasababishia udumavu wa akili na kimwili.
Alisema kuwa, watoto wanahitaji ukaribu wa wazazi wao ili kujifunza mambo mbali mbali ambayo yatawajenga kiakili, hivyo ni vyema wakatenga muda maalumu kwa ajili ya watoto wao.
"Mtoto anaanza kujifunza akiwa tumboni mwa mama yake, hivyo tunatakiwa kuwa karibu nao zaidi na tuwape malezi bora ili wakue vizuri, hii itamfanya awe imara na mwenye uwelewa wa hali ya juu," alisema Mtaalamu huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Makuzi na Malezi Bora ya watoto Zanzibar (MECP-Z) Sharifa Majid alieleza kuwa, watoto wanahitaji kutunzwa, kupatiwa lishe bora, kuwa na afya njema pamoja na kutengenezewa mazingira mazuri ya kuishi.
"Kuna baadhi ya wazazi hujitia pirika nyingi mpaka wakakosa muda wa kuwashughulikia watoto wao, jambo ambalo ni hatari katika maisha yao ya baadae kwa sababu mtoto anajifunza zaidi kuanzia pale mimba inapotungwa hadi miaka mitano kwa asilimia 80, hivyo iwapo atakosa malezi bora hatokuwa vizuri," alifafanua Mkurugenzi huyo.
Aidha aliwanasihi wazazi kuwapa watoto wao fursa ya kuzungumza na kuwasikiliza ili wawe huru kusema chochote kinachowakabili katika maisha yao.
Meneja Huduma za Jamii (ZPDB) Dk. Ibrahim Byatike Kabole aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa ajili ya kuwaelimisha wanajamii juu ya umuhimu wa malezi na makuzi bora ya watoto.
"Tushirikiane kuhakikisha kila mzazi anapata uelewa wa kutosha kuhusu malezi bora ya watoto, hili litasaidia watoto kukua vizuri na kuwa na ufahamu wa hali ya juu," alisema.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenethic Simbaya alisema, wanahabari wana jukumu la kuielimisha jamii juu ya malezi na matunzo ya watoto, hivyo wachukue jitihada mbali mbali kuhakikisha kila mmoja anabadilika na kuwalea watoto wake vizuri.
Mafunzo hayo ya utangulizi kuhusu -utelekezaji wa Programu Jumuishi ya Zanzibar ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto Zanzibar, yameandaliwa na UTPC kwa kushirikiana na Zanzibar Presidential Delivery Bureau pamoja na Zanzibar Mult-Sectoral (ECCD) kwa ufadhili wa Shirika la UNICEF Zanzibar pamoja na Big Win UK.
MWISHO.
Comments
Post a Comment