IMEANDIKWA
NA ZUHURA JUMA, DAR-ES-SALAAM@@@@
KATIBU
Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdalla Said amesema,
ili kupata taifa lenye maendeleo na wataalamu wabobevu, kila mmoja anapaswa
kuekeza mapema kwa watoto.
Akifunga mafunzo ya siku nne kwa
waandishi wa habari wa Zanzibar, kuhusu makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya
mtoto, alisema kuwa waandishi wanapaswa kutumia kalamu zao vizuri kuibadlisha
jamii na kuwa yenye kutekeleza malezi bora kwa watoto.
Alisema kuwa, kila mmoja anapaswa
kuekeza mapema kwa mtoto, hivyo ni jukumu la wanahabari kuhakikisha wazazi
wanafuata utaratibu mzima wa malezi na makuzi bora ya watoto kwa kuwapatia
lishe bora, afya imara, kuwapa nafasi ya kujifunza mapema na kuwa nao karibu,
hali ambayo itawajenga kuwa na kipaji kikubwa ambacho kitawaleta mabadiliko
chanya.
"Tusipokuwa na wataalamu
tutachelewa kupata maendeleo, hivyo tuanze kumkuza mtoto katika malezi bora
kuanzia, kwa ajili ya kujenga taifa imara," alieleza Katibu huyo.
Aidha aliwataka waandishi wa habari
watetee kwa sauti kubwa ili watoto wapate haki zao za msingi kwa mustakbali wa
maisha bora ya baadae.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Programu
ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka UNICEF Alinune Nsemwa,
alieleza kuwa ni muhimu kuiwezeha jamii kuhakikisha wanatoa huduma bora katika
makuzi ya awali ili watoto wa Tanzania wafikie utimilifu wao.
"Asilimia 47 tu ya watoto
Tanzania wamekuwa kwa utimilifu lakini asilimia 53 wanahitaji wakue na kufikia
utimilifu, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunatoa elimu ipasavyo ili tufukie
malengo, " alieleza.
Nae Meneja wa Huduma za Jamii
Zanzibar (ZPDB) Dk. Ibrahim Byatike Kabole alifafanua kuwa, mafunzo hayo
yanasaidia sana katika ukuwaji wa watoto ikiwa waandishi wa habari watakiwa
mstari wa mbele kutoa elimu kwenye vyombo vyao, kwani wao ni sauti ya wasio na
sauti.
"Malezi, makuzi na maendeleo ya
awali ya mtoto ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga taifa bora, kwa hiyo
waandishi tunawaomba mutumie kalamu zenu vizuri ili jamii iwelewe umuhimu wa
kumlea mtoto katika malezi bora," alieleza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vilabu vya
Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenethic Simbaya alisema kuwa, kuwaelimisha
waandishi wa habari ni kuweka msingi imara ambao utaleta mafanikio ya baadae,
hivyo Umoja huo umeona ni muhimu kuungana na Serikali kuhakikisha suala la ECCD
linapewa kipao mbele.
Meneja wa Kitengo cha Elimu ya Afya
Zanzibar Bakar Hamad Magarawa alisema, wataendelea kuwajengea uwezo wanajamii
na kuonyesha changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi, ili
kusudi waboreshe malezi ya watoto wao.
Mafunzo hayo ya utangulizi kuhusu
utelekezaji wa Programu Jumuishi ya Zanzibar ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya
Mtoto Zanzibar, yameandaliwa na UTPC kwa kushirikiana na Zanzibar Presidential
Delivery Bureau pamoja na Zanzibar Mult-Sectoral (ECCD) kwa ufadhili wa Shirika
la UNICEF Zanzibar pamoja na Big Win UK.
MWISHO.
Comments
Post a Comment