UZINDUZI WA PROGRAMU YA ECD ZANZIBAR: UTPC yawanoa waandishi wa habari visiwani, 'Jamii yatakiwa kuzingatia malezi na makuzi bora kwa watoto wao'
IMEANDIKWA
NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
KILA
tuamkapo asubuhi, wazazi wengi wana tabia ya kukimbilia sehemu zao za kazi
kuliko kumkimbilia mtoto wake aliepo nyumbani.
Lakini hii ni kwa sababu watoto
huchelewa kuamka ndipo mama huona ni bora kumuacha amalize usingizi wake, huku
akijua hatoonana nae kwa masaa tisa baadae.
Inasikitisha sana kuona kwamba
wazazi wa zama hizi hawana muda wa kuwashughulikia watoto, hawachezi nao na
wala hawawajengei mazingira bora ya kumfanya achangamke kiakili na kukua
vizuri.
Ingawa hili linaenda kupatiwa
muarubaini baada ya UTPC kwa kushirikiana na Zanzibar Presidential Delivery
Bureau pamoja na Zanzibar Mult-Sectoral (ECCD) kuwapa mafunzo wanahabari kwa
ufadhili wa Shirika la UNICEF Zanzibar pamoja na Big Win UK.
Ni mafunzo ya kuwajengea uwezo wa
kuelimisha jamii na kuripoti habari mbali mbali zinazohusiana na malezi, makuzi
na maendeleo ya awali ya mtoto Zanzibar.
David Gisuka ambae ni Mtaalamu wa
Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania hakuwa nyuma
kuwanowa wanahabari ili kusudi jamii ipate uelewa wa kumlea mtoto katika
amazingira bora.
Anasema, wazazi wanasahau majukumu
yao ya kumlea mtoto na kuona kwamba, jukumu lao ni kumpa chakula tu huku
wakisahau majukumu mwengine muhimu kwa watoto wao.
Anachambua kuwa, watoto wanaanza
kujifunza tangu pale mimba inapotungwa, hivyo ni wajibu wa kila mzazi kuwatunza
watoto, kuwapatia lishe bora, kuhakikisha wanakuwa na afya njema, kumpa fursa
ya kujifunza mapema na kumshirikisha katika mambo mbali mbali, ambayo
yatamsaidia kukua vizuri na kuimarika kiafya.
"Elimu ya malezi na makuzi bora
ya watoto inahitajika katika jamii yetu, ili kuhakikisha wazazi wanalea watoto
wao katika malezi yaliyobora, kwa sababu wengine hawaelewi umuhimu wa malezi
bora kwa watoto na wanaoelewa basi wanapuuza", anaeleza.
Madhara ya kumlea mtoto katika
malezi yasiokubalika ni makubwa sana kwani humuathiri katika maisha yake yote
na hatimae jamii husema... mtoto huyo amepotea, kumbe alikosewa katika malezi
ya awali.
Anasema, kuna baadhi ya wazazi wana
tabia ya kushughulikia zaidi kazi zao na kuwaacha watoto wao wakiwa wapweke, hali
ambayo inawasababishia udumavu wa akili na kimwili.
"Watoto wanahitaji ukaribu wa
wazazi wao ili kujifunza mambo mbali mbali ambayo yatawajenga kiakili, kwa
sababu akili ya mtoto tangu akiwa tumboni mpakani siku 2000 baadae ni kama
sponji, unapoliweka litafyonza, hiyo anachokiona ama kukisikia ni lazima
atajifunza,"
Hivyo ni vyema wakawatengeneza
kujifunza mambo yaliyobora ambayo yatawajenga kiakili kwa manufaa bora ya
maisha yao ya baadae.
Wazazi wanatakiwa kuekeza mapema
kwani siku 2000 kwa mtoto hujifunza kwa asilimia 90 huku asilimia zilizobaki
hujifunza akiwa mkubwa, hivyo unapomkosea mtoto katika malezi ya awali, basi
unakosea kumjengea maisha mazuri ya baadae.
"Mtoto anapozaliwa anakuwa na
asilimia 25, anapotimiza miaka mitatu anakuwa na asilimia 80 na anapofikia
miaka mitano huwa ana asilimia 90 ambazo ni sawa na siku 2000, hivyo ni muhimu
kwa wazazi kujitahidi kwenye malezi kwa siku hizo, kwa sababu asilimia chache
iliyobaki ndio anayotumia akiwa mkubwa," anaeleza
Mkurugenzi wa taasisi ya Makuzi na
Malezi Bora ya watoto Zanzibar (MECP-Z) Sharifa Suleiman Majid anasema, watoto
wanahitaji kutunzwa, kupatiwa lishe bora, kuwa na afya njema, kucheza pamoja na
kutengenezewa mazingira mazuri ya kuishi.
"Kuna baadhi ya wazazi hujitia
pirika nyingi mpaka wakakosa muda wa kuwashughulikia watoto wao, jambo hili ni
hatari katika maisha yao ya baadae kwa sababu mtoto anajifunza zaidi kuanzia
pale mimba inapotungwa hadi miaka mitano kwa asilimia 90, hivyo iwapo atakosa
malezi bora hatokuwa vizuri," anafafanua.
Mkurugenzi Sharifa anawasisitiza
wazazi kuwapa watoto wao fursa ya kuzungumza na kuwasikiliza, ili wawe huru
kusema chochote kinachowakabili katika maisha yao.
Anasema, namna unavyomlea mtoto wako
siku 1000 (asilimia 80) ama siku 2000 (asilimia 90) baada ya kuzaliwa ndipo
anapoweza kukua vizuri kimwili na kiakili huku akirithi tabia za wazazi kwa
asilimia 50 na asilimia 50 zilizobaki hujifunza kwenye mazingira
yaliyomzunguka.
"Ujifunzaji wa mtoto huanza
kabla ya kuzaliwa, hivyo anahitaji lishe bora, kujifunza mapema, kumjengea
mahusiano mazuri kati yake, wazazi na jamii iliyomzunguka," anafafanua.
Dk. Ibrahim Byatike Kabole ambae ni
Meneja Huduma za Jamii (ZPDB), anawaambia waandishi wa habari kutumia kalamu
zao vizuri kwa ajili ya kuwaelimisha wanajamii juu ya umuhimu wa malezi na
makuzi bora ya watoto.
"Tushirikiane kuhakikisha kila
mzazi anapata uelewa wa kutosha kuhusu malezi bora ya watoto, hili litasaidia
watoto kukua vizuri na kuwa na ufahamu wa hali ya juu," anasema.
Anaeleza, mafunzo hayo yatasaidia
sana katika ukuwaji wa watoto ikiwa waandishi wa habari watakuwa mstari wa
mbele kutoa elimu kwenye vyombo vyao, kwani wao ni sauti ya wasio na sauti.
Dk. Kabole anaeleza kwamba malezi,
makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga taifa
bora, hivyo waandishi wachukue jitihada za makusudi kuhakikisha kila mwanajamii
anapata uelewa.
Kennethic Simbaya yeye ni Mkurugenzi
wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) anasema, wanahabari
wana jukumu la kuielimisha jamii juu ya malezi na matunzo ya watoto, kufanya
hivyo kutalisaidia taifa kupata wataalamu wabobevu hapo baadae.
Anasema, kuwaelimisha waandishi wa
habari ni kuweka msingi imara ambao utaleta mafanikio ya baadae, hivyo UTPC
umeona ni muhimu kuungana na Serikali kuhakikisha suala la ECD linapewa kipao
mbele.
Mtaalamu wa Programu ya Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka UNICEF Alinune Nsemwa anasema, ni
muhimu kuiwezeha jamii kuhakikisha wanatoa huduma bora katika makuzi ya awali
ya mtoto wa Tanzania ili wafikie utimilifu.
Anafafanua, asilimia 47 tu ya watoto
wa Tanzania ndio ambao wamekuwa kwa utimilifu na asilimia 53 wanahitaji wakuwe
na kufikia utimilifu, hivyo ni jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake kutoa elimu
kwa jamii ili lengo walilolikusudia lifikiwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said anasema, ili kupata taifa lenye maendeleo
na wataalamu wabobevu, kila mmoja anapaswa kuekeza mapema kwa watoto.
"Kuekeza mapema ni kupi? Ni
kuhakikisha tunampatia malezi bora mtoto wetu tangu siku ya kutunga mimba kwa
kumpatia lishe bora, awe na afya njema, tuhakikishe tunampa fursa ya kujifunza
mapema na mazuri kutoka kwetu na mazingira yaliyomzunguka, tumpe fursa ya
kucheza na tuwe nao karibu," anafahamisha Katibu huyo.
Anasema, nchi isipokuwa na wataalamu
itachelewa kupata maendeleo, hivyo ni muhimu kumkuza mtoto katika malezi bora
kuanzia akiwa tumboni, jambo ambalo litawajenga kuwa na kipaji kikubwa ambacho
kitawaleta mabadiliko chanya katika maisha yao.
Bakar Hamad Magarawa ambae ni Meneja
wa Kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar anasema, wataendelea kuwajengea uwezo
wanajamii na kuonyesha changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kupatiwa
ufumbuzi, ili kusudi waboreshe malezi ya watoto wao.
"Akinababa pia wawe makini
wakati wa ujauzito wa wake zao kwa sababu mtoto anasikia kila kitu na anaanza
kujifunza pale, hivyo ikiwa atakosa lishe bora au atakosa furaka pamoja na kuwa
na msongo wa mawazo kuna hatari ya kuzaa mtoto ambae atakuwa na changamoto ya
udumavu," anafahamisha.
Meneja Mradi wa Programu ya Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Zanzibar Maryam Issa anasema, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imeamua kuongeza nguvu katika malezi,
makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
"Licha ya Serikali kuboresha
huduma za afya imeona kuna haja kubwa ya kuongeza nguvu katika makuzi z malezi
na maendeleo ya awali ya mtoto kuanzia umri wa zero (0) hadi miaka nane (8) ili
kuwa na watoto wenye afya bora ya kimwili na kiakili," anafafanua Meneja
huyo.
Mafunzo hayo ya utangulizi kuhusu
utelekezaji wa Programu Jumuishi ya Zanzibar ya Malezi, Malezi, Makuzi na
Maendeleo ya Awali ya Mtoto Zanzibar, yaliyowashirikisha waandishi wa habari
kutoka vyombo mbali mbali vya Zanzibar ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa
hoteli ya Jamirex jijini Dar-Es-Salaam.
MWISHO.
Comments
Post a Comment