NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
WAANDISHI wa habari nchi wametakiwa kujikita katika kuandika habari jumuishi na haki za watu wenyeulemavu, ili kuongeza upatikanaji wa haki na michango yao katika maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Afisa Programu na Mawasiliano wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania (TAMWA - Zanzibar) Khairat Ali Haji wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya uwandishi jumuishi.
Akizungumza katika mafunzo hayo alisema waandishi wananafasi kubwa katika kubadilisha mitazamo hasi kuhusu watu wenye ulemavu, hivyo ni vyema kutumia nafasi walizonazo ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika hatua za kimaendeleo.
" Waandishi wa habari wanakua na mchango mkubwa katika kubadili mitazamo iliomo katika jamii, hivyo ni muhimu kutumia nafasi hii kubadili mitazamo hayo, kwa kuwaibua na kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika kila hatua za kimaendeleo"alisema.
Aliongeza kua, mafunzohayo ni miongoni mwa juhudi za kuhakikisha vyombo vya habari vinashiriki katika utetezi wa haki za watu wenye ulemavu, kwa kuibua sauti zao pamoja na uonyesha uwezo walionao katika kushiriki kwenye hatua mbali mbali za kukuza maendeleo ya nchi.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Mwenyekiti wa baraza la watu wenye Ulemavu Zanzibar Salma Haji Saadati alisema, ulemavu ni hali ya upungufu wa kimwili, kiakili au kihisia unaomzuia mtu kushiriki katika shughuli za kijamii kama wanavyoshiriki wengine.
Alieleza kua, kumekua na ongezeko la watu wenye ulemavu duniani kote, hii nitokana na sababu mbali mbali, ikiwemo maradhi, ajali, vita, utapiamlo utokanao na lishe duni pamoja na umasikini.
Alifafanua kua kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), 2025 watu wenye ulemavu wamefikia asilimia 16 ya watu wote duniani, ikiwa ni ongezeko la asilimia moja kutoka asilimia 15 ya mwaka 2011.
Aidha alieleza kua matokeo ya Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022, yameweka wazi kua asilimia 11.2 ya watu wote Tanzania bara ni wenye ulemavu, huku Zanzibar ikifikia asilimia 11.4 kati ya watu Milioni 1.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5 kutoka mwaka 2012.
" Takwimu zinaonesha kua kunaongezeko la watu wenye ulemavu kila uchao, na nikutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo maradhi, ajali, vita na mengineyo, na asilimia 50 ya ulemavu unatokana na umasikini na asilimia 20 ni kutokana na utapiamlo, ambapo mawili haya yanaweza kuzuilika" alieleza.
Alieleza kwamba, changamoto wanazokutana nazo watu wenye ulemavu mara nyingi husababishwa na jamii husika, hii ni kutokana na mitazamo hasi ilionayo jamii jambo linalopelekea unyanyapaa, kutengwa na kudharauliwa.
Aliongeza kua, mara nyingi jamii humuangalia mtu mwenye ulemavu kama ni mtu tengemezi katika kila kitu, jambo linalopelekea kumnyima fursa mbali mbali anazostahili, ikiwemo elimu, uchumi, na ushiriki katika nyanja za siasa.
Alisisitiza kua, pamoja na kuwepo kwa sera, sheria na mikataba mbali mbali yanayoeleza haki za watu wenye ulemavu, lakini bado jamii haijazingatia ipasavyo kuhusu umuhimu wa sera, kanuni, shria na mikataba hiyo.
Hivyo ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo, kuhakikisha wanaielimisha jamii kuhusu haki na umuhimu wa ushiriki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo, ili kubadilisha mitazamo hasi iliomo katika jamii juu ya watu wenye ulemavu.
Nao washiriki wa Mafunzo hayo walisema, watatumia mafunzo waliopatiwa katika kuhakikisha wanawajumuisha, kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu, ili kuongeza uwelewa kwa jamii juu ya uwezo na mchango mkubwa walionao watu wenye ulemavu katika maendeleo ya nchi.
Mafunzo hayo ni miongoni mwa utekelezaji wa mpango 'Collective Actions for Disability Right ' unaolenga kunyanyua sauti, haki, ushiriki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika jamii kupitia vyombo vya habari, sera na mipango ya maendeleo.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya TAMWA-Zanzibar, ZANAB na Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar.
MWISHO
This comment has been removed by the author.
ReplyDelete