NA KHAULAT SULEIMAN,
PEMBA
MKURUGENZI wa Idara ya
Mafunzo ya Walimu Zanzibar Othman Omar Othman amesema, Wizara
itaendelea kuandaa mikakati ya kuwajengea uwezo walimu ili kuleta mabadiliko
chanya katika sekta ya elimu Zanzibar.
Aliyasema hayo
katika mahafali ya walimu kutoka Taasisi ya Malezi na Makuzi bora ya
Watoto Wadogo (MECP-Z) yaliyofanyika katika Ukumbi kiwanja cha kufurahishia
watoto Tibirinzi Chake Chake Pemba.
Mkurugenzi huyo
alisema kuwa, kupitia ujuzi waliopewa walimu hao iwe ni chachu ya kuleta
maendeleo kwa wanafunzi wao, kwa kuwajengea uwezo wa kujua kusoma na kuandika,
ili lengo la Serikali la kutoa elimu bora liweze kufikiwa.
"Wizara ya Elimu
haitasita katika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu, ili kila mmoja
aweze kupata haki yake ya elimu, hivyo walimu sasa ni jukumu lenu kuanda
programu mbali mbali ambazo zitasaidia wanafunzi kufahamu vizuri na kufaulu
katika mitihani yao" alieleza Mkurugenz huyo.
Aidha aliishukuru
Taasisi hiyo ya Madrasa kwa kuanda mafunzo hayo pamoja na kuwawezesha vijana
kujiajiri na kupunguza wimbi kubwa la vijana ambao hawana la kufanya mitaani,
hivyo serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali ambazo zinasaidia
kuleta maendeleo ya elimu katika jamii.
Akizungumza kwa niaba
ya Mkurugenzi MECP-Z, Afisa Maendeleo ya Jamii Pemba Haji Ali Hamad alieleza
kuwa, zipo tafiti mbali mbali ambazo zinaonesha muongozo mzuri wa kupata taifa
bora ni katika uwekezaji kwa watoto chini ya umri wa miaka nane, kwani ufahamu
wao unakuwa ni wa kiwango cha juu zaidi.
Alisema kuwa, Madrasa
Early Childhood inatekeleza mradi huo chini ya ufadhili wa Shirika la Global
Affair kutoka nchini Canada kwa kushirikiana na Shirika la Aga Khan foundation
Tanzania ambao unawawezesha walimu kuweza kujifunza kwa vitendo kwajili ya
ustawi bora wa maisha endelevu ya watoto.
Mkufunzi wa walimu hao
kutoka tasisi ya MECP-Z Hassan Ali Bakar alisema, wataendelea kuwaandaa
vijana hao ili kusaidia nguvu kazi ya taifa katika kuleta mabadiliko ya
elimu.
Jumla ya wanafunzi 34
wamehitimu na kukabidhiwa vyeti vyao, wakiwemo wanawake 30 na wanaume wanne,
ambapo mradi huo tayari umeshafundisha walimu 149 kisiwani Pemba.
Mwisho.
Comments
Post a Comment