HOTUBA YA MHE. RIZIKI PEMBE JUMA WAZIRI WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO KWA WAANDISHI WA HABARI KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU 16 ZA HARAKATI ZA KUPINGA UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA, KATIKA UKUMBI WA WIZARA, KINAZINI MKOA WA MJINI MAGHARIBI, TAREHE 21/11/2024.
· MHE. ANNA ATHANUS PAUL, NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO,
· NDUGU MWADINI KHATIB MWADINI, KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO,
· NDUGU WAKURUGENZI WOTE,
· WAANDISHI WA HABARI ,
ASSALAAMU ALAYKUM.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kutujaalia uzima na afya njema na kutuwezesha kukutana hapa tukiwa wazima wa afya, kwa lengo la kuzungumza nanyi kuhusu siku 16 za mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na Udhalilishaji tuseme Alhamdulillah.
Kwa kipekee napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kutusimamia vyema wananchi wake Wa Zanzibari, kuendelea kutupa miongozo na maelekezo ambayo yamekuwa yakituongoza katika kusimamia majukumu ya Wizara yetu. Aidha, nichukue nafasi hii pia kumpongeza kwa kutimiza miaka minne ya Uongozi wake ambao tumeshuhudia Mapinduzi makubwa ya maendeleo ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa yakiendelea ndani na nje ya nchi yetu. Tumuombe Mwenyezi Mungu ampe Afya njema na aendelee na majukumu yake ya kuiongoza nchi kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
Tukiwa tunaelekea kuadhimisha siku 16 za harakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia napenda kutoa masikitiko yangu makubwa kwa kitendo cha ukatili alichofanyiwa mtoto Khadija, mwenye umri wa miaka sita kudhalilishwa kingono na baadae kupotezewa uhai wake, Wizara imesikitikitishwa na kitendo hicho na kwa kushirikiana na mamlaka nyengine haitosita kumchukulia hatua yeyote atakaebainika kufanya ukatili na udhalilishaji huo.
Chimbuko la siku 16 za wanaharakati za kupinga vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa Kijinsia ni kampeni ya ulimwenguni kote ambapo chimbuko lake linatokana na mkutano wa wanaharakati dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia uliofanyika mjini Bogota Colombia America ya kati tarehe 18 - 21 November 1991 kwa kubadilishana mawazo juu ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia duniani. Mkutano huo uliazimia na kuchagua siku 16 kuanzia tarehe 25/ Novemba hadi tarehe 10 Disemba ambayo ni siku za kimataifa dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji na hadi tarehe 10 Disemba ambayo ni siku ya Kimataifa ya haki za binaadamu kwa lengo la kuhusisha masuala ya ukatili na masuala ya haki za binaadamu.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI .
Mwaka 1999 Umoja wa Mataifa uliridhia na kutangaza kuwa siku 16 za wanaharakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, kwa hapa kwetu Zanzibar harakati hizi zilianzia mwaka 2011 na kuendelea hadi leo kwa kufanya shughuli mbali mbali.
Lengo la maadhimisho haya ni kutathmini juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na wadau katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, kuhamasisha wadau na jamii kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi na kupanga mikakati mipya ya kupambana na kadhia hii.
Kwa kawaida maadhimisho haya kwa kila mwaka huwa na ujumbe maalum unaoakisi mikakati ya kuondoa tatizo hilo. Kwa mwaka huu tumelenga kuwaleta pamoja watu wote kwa kupaza sauti na kuonesha hisia zetu na kila mmoja kuonesha hatua za kuchukua katika kukabiliana na tatizo la vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
Ujumbe wa mwaka huu wa 2024 ni "kuelekea 2030 tuungane kutafakari na kuchukua hatua kumaliza udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto Zanzibar." Kwa hakika kauli mbiu hii inatupa ari ya kukaa kwa pamoja na kushirikiana ana kwa ana kutokomeza kabisa vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia ambao umekuwa tishio hapa Zanzibar na kuumiza akili za walio wengi.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
kwa mwaka huu maadhimisho ya siku 16 yanatarajiwa kuzinduliwa Zanzibar na kufungwa kisiwani Pemba ambapo katika siku hizi 16 za harakati za kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa shughuli mbalimbali zikiwemo kuanda shindano la uandishi wa Insha kwa wanafunzi wa Sekondari na Vyuo vikuu kuhusiana na vitendo vya udhalilishaji kwa Wanafunzi.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
Shuguli nyengine ambazo zinatarajiwa kufanywa na Wizara ni Kongamano la Wajasiriliamali wanawake na Wanaharakati wengine Unguja na Pemba kuhusiana na mapambano dhidi ya ukatili pamoja na kupewa elimu ya ujasiriamali ikiwemo uandaaji wa miradi. Kufanya mikutano na wadau wa GBV na waratibu wa wanawake na watoto wa shehia pamoja na kutoa mafunzo kwa Wanafunzi kupitia Serikali zao za Wanafunzi katika Skuli.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
Wizara pia imepanga kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya kupinga udhalilishaji na ukatili dhidi ya wazee, wanawake na watoto wakiwemo Tamwa, Zafela, Mahakama, Fawe, Dawati la jinsia pamoja na wadau wengine kwa kuwasilisha shughuli zinazotekelezwa na taasisi zao na kutoa elimu kwa wananchi watakaofika katika ufunguzi huo.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
Jumla ya matukio 165 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi wa julai 2024,ambapo waathirika walikuwa 165, ikiwa Waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 86.1, wanawake asilimia 10.9 na wanaume asilimia 3.0.Miongoni mwa watoto ambao wameathirika ni142, wasichana walikuwa 115 sawa na asilimia 1.0 na wavulana walikuwa 27 sawa na asilimia 19.0.
Matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yaliyoriptiwa kwa mwezi Agosti 2024 yalikuwa ni 157 ambapo waathirika wengi walikuwa ni watoto sawa na asilimia 87.2 wanawake asilimia 11.5 na wanaume asilimia 1.3. Miongoni mwa waathirika watoto ni 137, wasichana walikuwa 112 sawa na asilimia 81.8 na wavulana walikuwa 25 sawa na asilimia18.2
Katika mwezi wa Septemba`2024, jumla ya matukio 148 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa ambapo waathirika walikuwa 148. Waathirika wengi walikuwa watoto kuanzia kuzaliwa hadi miaka 17 sawa na asilimia 87.9, Wanawake miaka 18 na zaidi sawa na asilimia 7.4 na Wanaume kuanzia miaka 18 na kuendelea sawa na asilimia 4.7, miongoni mwa watoto waathirika 130 Wasichana walikuwa 107 sawa na asilimia 82.3 na wavulana walikuwa 23 sawa na asilimia 17.7.
Takwimu hizi zinaonesha kupungua kidogo kwa matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ukilinganisha na mwezi wa July na hii ni kwa mujibu wa toleo la Takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar, hii haimaanishi tupunguze kasi ya kupambana na vitendo hivyo bali nguvu zinahitajika zaidi ili tuweze kuyatokomeza kabisa matendo hayo thakili.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
Pamoja na juhudi nyingi zinazochukuliwa na Serikali na zisizo za Kiserikali, bado vitendo vya udhalilishaji vinaendelea. Jamii bado haijashajiika na kufahamu athari ya vitendo hivi na badala yake inaendeleza rushwa muhali.
Hivyo, ni jukumu letu sote kuendeleza kutoa taaluma ya athari za vitendo hivi ili jamii ipate uelewa wa kina kuhusiana na ubaya wa vitendo hivyo.
NDUGU WAANDISHI WA HABARI
Naomba nimalizie hotuba yangu kwa kuyashukuru Mashirika ambayo tumekuwa tukishirikiana pamoja katika harakati hizo ambayo ni shirika la UNWOMEN, UNFPA Tanzania, UNICEF, IOM, UNESCO, Save the Children, Zanzibar Maisha Bora Foundation, PATHFINDER, C-SEMA, ACTIONAID, Asma Mwinyi Foundation, TAMWA, ZAFELA, ZCRF, na mengineo kwa kutuunga mkono kwenye mapambano ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Kabla kumalizia maelezo yangu naomba nikushukuruni Waandishi wa habari kwa kushirikiana nasi katika mapambano haya na nakuombeni muendelee kutuunga mkono ili lengo letu la kuvishinda vitendo hivi liweze kutimia.
Mwisho kabisa, nitoe shukrani na pongezi za dhati kwa Jeshi la polisi mkoa wa kusini Unguja kwa kufanikiwa kumkamata mtuhumumiwa wa ubakaji na mauaji ya mtoto Khadija kilichotokea Mwera pongwe, niwaombe waendelee kuchukua juhudi za haraka kuhakikisha kuwa kesi hii inaenda katika vyombo vya kisheria ili sheria iweze kuchukua mkono wake.
Kwa pamoja tunaweza kuutokomeza ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ndani ya taifa letu.
Zanzibar bila ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia inawezekana sana
Tanzania bila ya ukatili na udhalilishaji inawezekana sana.
Chukua hatua.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.
Comments
Post a Comment