NA HAJI NASSOR, UNGUJA@@@@
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan, amesema njia nzuri ya kufanyakazi kwa jumuiya za wasaidizi wa sheria, ili kupata mafanikio, ni kuondokana na umimi wakati wa utekelezaji, wa shughuli zao.
Alisema, wafadhili wanapotoa fedha zao, wanataka kuona matunda ya kilichofanywa na taasisi husika, sasa njia nzuri ni kushirikiana, wakati wanapotelekeza miradi hiyo.
Katibu Mtendaji huyo aliyasema hayo jana, ukumbi wa mikutano wa Michenzani Mall mjini Unguja, wakati akichangia mada ya namna bora, ya kupata mafanikio, kwa watoa msaada wa kisheria, kwenye jukwaa la nne la msaada wa kisheria Zanzibar.
Alisema, kama jumuia zitaendeleza na umimi na kujifungia ndani, wakati wanapotekeleza miradi, inaweza kuwa vigumu kupata mafanikio, yaliokusudiwa.
Alieleza kuwa, jumuia za watoa msaada wa kisheria, zimekuwa zikifanyakazi moja kubwa, ingawa shida iliyopo ni kutoshirikiana wakati wanapofanyakazi hizo.
‘’Kwa mfano, jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake inapiga vita udhalilishaji, basi ishirikiane na ile ya Mkoani, yenye kazai kama hiyo, ili kuwa na nguvu za pamoja na mfano wa hayo,’’alipendekeza.
Katika hatua nyingine, Katibu Mtendaji huyo wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan, alisema wafadhili mbali mbali, waendelee kutoa rukuzu kubwa, ili baadae jumuiya hizo, ziweze kujitegemea.
Alisema, jumuiya hizo zinafanyakazi kubwa na kwenye mazingira magumu, hivyo kama zikipatiwa ruzuku kubwa zinaweza kujitegemea, hapo baadae.
‘’Niwaombe sana wenzetu wa UNDP, UN-Women na LSF kuangalia uwezekano, sasa kutoa rukuzu zilizotononoka, ili jumuia zetu za watoa msaada wa kisheria, zijiendeshe zenyewe,’’alifafanua.
Mapema Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa Kisheria na Haki za Binaadamu Zanzibar ‘ZALHO’ Harusi Miraji Mpatani, alisema inawezekana, ufadhili mdogo ndio chanzo cha jumuia nyingi za msaada wa kisheria, kutofikia ndoto zao.
Akichangia mada kwenye jukwaa hilo, Msaidizi wa sheria kutoka wilaya ya Mkoani ‘MDIPAO’ Shaaban Juma Kassim, alisema yapo mafanikio wanayopata, kupitia ufadhili wanaopewa na washirika wa maendeleo.
Alifahamisha kuwa, ijapokwa jigografia ya maeneo wanayofanyakazi yanawatesa kwa kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha, lakini wanafanyakazi kwa bidii.
Mapema Mwakilishi kutoka ‘UNDP’ Ali Shaib, alisema kadiri fedha inavyopatikana, wanaendelea kuigawa kwa taasisi kadhaa, ili kuunga mkono judu za upatikanaji haki Zanzibar.
Akiahirisha kongamano hilo kwa siku ya kwanza, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, Hajjat Hanifa Ramadhan Said, aliwapongeza wasaidizi wa sheria, kwa kazi wanazozifanya.
Mwisho
Comments
Post a Comment