NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
VIJANA 150, waliojiajiri uchimbaji mawe, shehia za Mchakwe, Bwegeza, Kengeja, Shamiani na Mwambe wilaya ya Mkoani, wamesema wamerejesha matumaini ya uhakika wa kipato, baada ya serikali kutengua uwamuzi wake, wa kupiga marufuku uchimbaji wa rasimali hiyo.
Walisema, kuanzia juzi Novemba 14 mwaka huu, wameanza kurudi kwenye eneo lao walilojiajiri, kufuatia katazo la awali la serikali, kutengeuliwa mapema wiki iliyopita.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walisema kwa sasa wanauhakika wa maisha, maana eneo hilo, ndio walilolichagua kiajiri.
Walisema, kutenguliwa kwa agizo hilo, kwao ni faraja maana wengi wao, wanazofamilia zinazowategemea, katika maisha yao ya kila siku.
Mmoja kati ya vijana hao, Hamad Mcha Vuai wa Mchakwe Mwambe, alisema kwa sasa anajisikia faraja, kutokana na uamuzi huo, wa serikali.
‘’Sasa watoto wangu wataniita baba na mke wangu ataniita muume wangu, maana nimerudi kwenye ajira, nilioichagua, kwa ajili ya kuendeleza familia yangu,’’alieleza.
Nae Himid Mcha Mosi wa Mwambe, alisema anawake wawili na watoto wanane, ambao wote walikuwa wanamtegemea, kupitia kazi ya uchimbaji mawe.
‘’Leo tumefunguliwa baada ya kufungiwa kwa wastani wa mwezi mmoja na nusu, sasa najiona muume wa wake wawili na watoto wanane,’’alifafanua.
Kwa upande wake Muhdin Awadhi Hija ambae hununua na kuliuza kwa wenye gari za mzigo, alisema amekula hasara ya shilingi 1,000,000 kutokana katazo hilo la awali.
‘’Nilishachukua fedha za watu, kwamba mwezi wa Oktoba wengekuja kuchukua jiwe lao, lakini lilipokuja katazo, nilishazitumia fedha, ikanibidi nizilipe,’’alieleza.
Omar Haji Hassan na mwenzake Mkubwa Nassor Mwadini walisema wao, walikuwa wananunua jiwe kwa ajili ya kusarifia kokoto, ingawa katazo lilipo kuja hawakuathirika sana.
‘’Wakati katazo linakuja, tulishalipa madeni (kokoto), ambazo tulichukua fedha, tokea mwezi Mei mwaka huu, athari tuliyoipata ni hivi karibu, lilipomalizia jiwe la kubanjia kototo,’’walieleza.
Mfanyabiashara wa dula la chakula Mwambe Himid Mosi Makame, alisema alikaa zaidi ya mwezi mmoja na nusu, bila ya kulipwa deni, la shilingi 500,000 ambazo walichukua chakula wateja wake.
‘’Wakati zoezi la uchimbaji wa mawe halijazuiwa, ilikuwa wateja wangu wanakopa mchele, sukari, sabuni, mafuta na mwisho wa mwezi wanarejesha, ila katazo lilipokuja walichelewana wengine hadi leo hawajalipa,’’alifafanua.
Mmiliki wa gari ya mzigo Sharif Mohamed Ali, alisema athari aliyoipata ni kukosa kazi, maana wateja wake wengi, walikuwa ni wajezi wanaotumia mawe.
Mwananchi Kassim Omar Kassim wa Kiwani, alisema baada ya kufunguliwa tu, juzi alishaagiza gari tano, kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wake, uliosita.
Mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Hassan Shaibu Kaduara, alisema serikali inakataza matumizi ya jiwe, hadi hapo litakapotoka agizo jingine.
Alieleza kuwa, katazo hilo limeangalia maslahi mapana ya taifa, hivyo kila mwananchi alitakiwa kufahamu kuwa athari za kimazingira ni kubwa, kuliko faida inayopatikana.
"Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, juu ya athari za kimazingira juu ya rasilimali ya mawe, inavyo athiri mazingira,” alisema.
Kwa wakati huo wa katazo, alisisitiza kuwa, ni vyema wananchi kutumia matofali, kwa ajili ya ujenzi wa msingi na inaonesha ni rahisi, kuliko kutumia mawe.
Mwisho
Comments
Post a Comment