NA HAJI NASSOR, ZANZAIBAR@@@@
WAZIRI wa Nchi, Afisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utawala Bora Zanzibar Haroun Ali Suleiman, amesema inafurahisha kuona serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinashirikiana katika kufanikisha utoaji wa msaada wa kisheria.
Alisema, ushirikiano huo umesababisha kuimarika kwa utoaji huo wa msaada wa kisheria, ikiwemo kupitia kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Waziri Haroun aliyasema hayo leo Novemba 20, 2024 ukumbi wa mikutano wa Michezani Mall, wakati akilifungua jukwaa la nne la msaada wa kisheria, lililoandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, kwa ushirikiano na UNDP.
Alisema, kwa upande wa Zanzibar Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuwa mstari wa mbele, kuungano mkono utoaji wa msaada wa kisheria, ikiwemo kutoa bajaji saba, kwa watoa msaada wa kisheria Zanzibar.
Alieleza kuwa, hili ni jambo la kupongezwa, kwa viongozi hawa, kwani wamekuwa wakiunga mkono kwa vitendo, kazi zinazofanywa na wasaidizi wa sheria mbali mbali.
‘’Mimi niwapongeze viongozi hawa, maana wamekuwa karibu na sisi, kwa kutusaidia na kutuungano mkono, lakini hata suala hili limesisitizwa kwa upana ndani ya Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 na dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050,’’alifafanua.
Aidha Waziri Haroun alisema, juhudi nyingine za serikali za kuunga mkono, ni kufuta ada kwa watoaji wa msaada wa kisheria Zanzibar, kuanzia mwaka 2023.
Akizungumzia kaulimbiu ya jukwaa hilo ambayo ni ‘ushawishi wa upatikanaji wa rasilimali za kuendeleza huduma za msaada wa kisheria Zanzibar ’ alisema ni muhimu kwa vile inahimiza ubunifu na mbinu imara, katika kutafuta rasilamali za kuimarisha upatikanaji haki.
Katika hatua ningine, Waziri Haroun alisema ni muhimu kila mmoja, ahakikishe hakuna mtu ambae anahitaji msaada wa kisheria na kuukosa.
Mapema akiwasilisha maazimio ya jukwaa la tatu msaada wa kisheria, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hajjat, Hanifa Ramadhan Said, alisema mingi yao yameshaanza kutekelezwa.
Alisema, moja wapo ni kwa skuli ya sheria Zanzibar kufanya marekebisho ya mitaala yao, jambo ambalo limeshanza kutekelezwa.
‘‘Lakini pia kulikuwa na wazo la kufutwa kwa ada kwa wasaidizi wa sheria, hili nalo limeshatekelezwa na tayari kwa mwaka huu wasadizi wa sheria hawakulipa,’’alifafanua.
Akitoa salamu kutoka Shirika la maendeleo la kimataifa ‘UNDP’ kwa niaba ya mkurugenzi mkaazi, mwakilishi huyo Ali Shaib, alisema wanafurahishwa kuona, UNDP inakuwa sehemu ya upatikanaji haki hapa Zanzibar.
Hata hivyo, alisema UNDP itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali, ili kuhakikisha upatikanaji haki kwa wananchi hasa wanyonge wanapata haki zao.
Afisa Miradi Mwandamizi kutoka taasisi ya ‘LSF’ Bakar Hamad, alisema karibu shilingi bilioni 5.1 zimekuwa zikitumika kwa Tanzania nzima, kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji haki, na asilimi 30 ua fedha hizo, zimeekezwa Zanzibar.
Hata hivyo aliwapongeza wasaidizi wa sheria Zanzibar, kwa kazi kubwa wanazozifanya, licha ya changamoto wanazokumbana nazo wanapokuwa kazini.
Mapema Katibu Mkuu wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mansura Mosi Kassim, alisema Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, imekuwa ikifanyakazi kubwa, na kuibeba wizara kwa saifa nzuri.
Alieleza kuwa, kinachohitajika ni kuendeleza juhudi hizo, ili jamii ipate mwamko wa kudai haki zao za kisheria, ikiwa ni hatua ya kuimarisha utawala bora na utawala wa kisheria.
Katika jukwaa hilo mada kadhaa zitawasilishwa ikiwa ni uendelevu wa rasilimali fedha katika taasisi za msaada wa kisheria, jukumu la washirika wa maendeleo katika sekta ya msaada wa kisheria juu la rasilimali fedha Zanzibar.
Katika jukwaa hili la nne la msaada wa kisheria kwa mwaka huu 2024, kauli mbiu ni ‘ushawishi wa upatikanaji wa rasilimali za kuendeleza huduma za msaada wa kisheria Zanzibar’.
Mwisho
Comments
Post a Comment