NA FATMA HAMAD, PEMBA@@@@
‘MIMBA
yangu ya nne manusura niiage dunia’.
Asha Said mama wa watoto wanne ambae sio jina lake halisi
anasema, mimba yake ya pili alijifungulia nyumbani, na alipata tatizo la
kutokwa na damu nyingi, na kupelekea hadi kupoteza fahamu.
‘’Baada tu ya kujifungua sikujifahamu tena, mpaka
nilikuja kuzinduka nimewekewa chupa ya maji hospitali ya Micheweni,’’anaeleza.
Mume wa mama huyo ambae hakupenda jina lake
lichapishwe, anasema baada ya kuona hali ya mke wake imeshakuwa mbaya, ndipo
usiku huo, alipokodi gari na kumpeleka Hospitali.
Hivyo alipatwa na huzuni, hali ambayo ilipelekea
kupoteza gharama kubwa ya matibabu, kwa ajili ya kuokoa maisha ya mke wake,
pamoja na mtoto.
‘’Nilipata
funzo na sasa nikimuona tu uchungu umeanza namuwahisha hospitali haraka, kwani
huko akipata matatizo anaweza akawahiwa mapema na watalamu wa afya,’’anaeleza.
Maryam Said
mkaazi wa Chake chake ambae anaishi na virusi vya ukimwi kwa muda wa miaka 18,
alimuambukiza mtoto wake wa mwanzo mambukizi ya virusi vya ukimwi.
Kwani mimba yake ya kwanza, alijifungulia nyumbani,
kwa hofu ya kwenda hospital kwa kuogopa kunyanyapaliwa na wahudumu wa afya kwa
wakati huo.
‘’Hadi leo najilaumu, na najutia nafsiyangu, kwa
kitendo cha kutokimbilia hospitali kwa ajili ya kwenda kujifungua, nikidhani
kwamba nyumbani ni salama,’’anasimulia.
Kwa sasa ameshajifungua
watoto wingine watatu, ambao wako salama na vvu, baada ya kusikiliza na kutekeleza
kwa vitendo, ushauri wa watalamu wa afya.
Kumbe
hata Halima Juma wa Mjini Kiuyu wilaya ya Wete nae amepitia machungu kwa kule
mimba zake tatu kujifungulia nyumbani.
Linalomkimbiza
hosptali anasema ni lugha za madaktari, nenda rudi isiyozaa matunda na hata
suala la uhaba wa watalamu halimshawishi kujifungulia hospitali.
Khadija
Khamis mama wa watoto watano, mkaazi wa Sizini hadi leo hii bado hajafikiwa na
elimu ya kuhudhuria kliniki, na ndio maana hufika kwa watalamu baina ya miezi sita
hadi saba ya ujauzito.
‘’Mimi sipendi kwenda kituo cha afya ikiwa
bado mimba ni changa, si pendi ile kila siku nenda na keshokutwa uje tena naona
tabu,’’anfafanua.
Amina
Omar Msellem mkaazi wa Chake chake anasema amejifungua mimba saba na zote ni
kituo cha afya, wala hajapata changamoto yoyote yeye wala watoto wake.
‘’Tuache
kuzaa changamoto zetu wenyewe, kama hatutaki kuhudhuria kliniki tukae kimnya,
lakini unapokwenda unapewa huduma kama ilivyotakiwa, maana daktari hajiskii vizuri
kumpokea mjamzito kisha kufariki,’’anasema.
MTAALAMU WA AFYA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO
Akieleza
athari anazozipata mama mjamzito anapojifungulia nyumbani Maryam Ali Said Mratibu
wa huduma za mama na mtoto Pemba, anasema moja ni kukosekana kwa huduma za mapema za kimataibabu.
‘’Inawezekana mama hawezi kujifungua kwa njia
ya kawaida, analazimika afanyiwe upereshini, lakini mkunga wa jadi hana taluma
ya kujua hilo,’’anaeleza.
Anasisitiza kuwa, kuhudhuria kituo cha afya kuanzia
wiki ya mwanzo ya ujauzito hadi kufikia kujifungua ni lazima kwa mjamzito, ili
kujikinga na majanga.
‘’Kujifungulia
nyumbani ni sawa na kununua mauti, ya mama na mtoto wake, maana hakuna mtalamu,
vifa vya kinga ya maradhi na wengine wanaishi mbali na vituo vikuu vya
afya,’’anasema.
Fatma
Suleiman Daudi msimamizi wa huduma ya mama na mtoto hospital ya Chake chake,
anaeleza kuwa, mjamzito akijifungulia nyumbani, huwa rahisi mno kumuambukiza maradhi
mtoto wake na mkunga.
‘’Kama
mama atakua ana mambukizi kama vile homa ya Ini au Virusi vya ukimwi, bila ya
kutumia kifaa kinga cha aina yoyote, anaweza kusababisha mtoto, mkunga kupata
mambukizi,’’anaeleza.
Mjamzito anaejifungulia nyumbani, anaweza kupata
athari kiwemo kukaa kwa muda mrefu na uchungu, jambo ambalo linaweza likasababisha
kuchanika haraka kwa fuko lake la uzazi.
‘’Mara
nyingi wanapokuja Hospitali inakua mama ameshachoka, hali taabani, mpaka iwe
wameshashindwa, hata ukija ukitoa tena hizo tiba muda umeshapita,’’afafanua.
Kumbe
unapochanika kwa fuko la uzazi maranyingi mama, hutokwa na damu nyingi ambayo
inaweza kusababisha hata kifo chake.
‘’Unapochanika
kwa fuko la uzazi, hatuwezi kusema kama ndio mwisho wa maisha, lakini kama
hukuwahiwa mapema kupatiwa matibau unaweza ukapoteza maisha,’’anafafanua.
‘’Kuna siku tulimpokea mama na alikuwa ni
ujauzito wa tatu, alivyo kuja akapelekwa kwenye chumba cha kujifungulia, kabla
ya kumlaza kwa ajili ya kujifungua, tulimuhisi kalala kumbe
ameshafariki,’’anasimulia.
WANAUME
WANASEMAJE?
Abdalla
Nassor Abdala mwananchi wa Chake chake anasema, mama anapojifungulia nyumbani,
mazingira ya usafi pamoja na usalama wa
mama kujifungua salama yanakua, hayatoshelezi.
Mkewake
amejifungua mimba nane, na zote alikua anampeleka hospitali wakati anapoumwa tu
na uchungu, na hawajahi kulalamikia huduma,’’anafahamisha.
Khamis
Haji Omar, anasema ameshamsindikiza mke wake hospitali kujifungua mara nne,
bila ya changamoto yoyote.
SERIKALI
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja anasema
ni vyema kwa wizara ya Afya, kuongeza mkakati wa elimu ili wanawake
washawishike kujifulia hospitalini.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed
Mazrui anasema wizara imeimarisha miundombinu ya kutolea huduma hospitalini,
ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Afisa Mdhamin wizara ya Afya Khamis
Bilal Ali, amewataka wahudumu wa afya kuwa na lugha nzuri kwa wajawazito, ili
iwe ni sehemu ya ushawishi ya kuhudhuria kliniki.
‘’Wizara kwa upande wake inaendelea kuimarisha
miundombinu bora ikiwemo vifaa tiba dawa, lakini ni nafasi kwa watalamu wetu wa
afya, nao kutumia lugha laini ili kufanikisha hilo’’,anasema.
Wizara ya Afya Zanzibar imechukua hatua kadhaa kuhakikisha
wajawazito wanapata huduma bora wakati wa kujifungua. Hapa ni baadhi ya
mikakati na hatua wanayochukua:
Mikakati mwingini ni upatikanaji wa Huduma za
Afya, ambapo Wizara inahakikisha kuwa vituo vya afya
vinapatikana kwa urahisi, ili wajawazito waweze kujifungulia salama.
Mkakati wa elimu kwa wajawazito, hapa Wizara inaendelea kutoa
elimu kwa wajawazito kuhusu umuhimu wa kujifungulia hospitalini na athari za
kujifungulia nyumbani.
Eneo jingine ni kuimarisha vifaa tiba, ambapo
hapa wizara inahakikisha kuwa hospitali zina
vifaa tiba vya kutosha kwa ajili ya kujifungulia, ikujumisha vitanda, vifaa vya
upasuaji, na dawa.
Hata hivyo wizara hiyo imesema katika kuwavuta wajawazito
kujifungulia hospitali, wanaimarisha ufuatiliaji kwa kufuatilia takwimu za
kujifungua, ili kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi.
TAKWIMU
Kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya mama na mtoto
Pemba, inaonyesha kuwa, mwaka 2022 wajawazito 2019, walijifungulia nyumbani,
kati ya hao wanne [4] walifariki.
Waliojifungulia hospital ni 1,6269 kati ya hao,
Micheweni ni 985, Mkoani 754, Wete 9445 na Chake chake 5365, ambapo waliofariki
kutoakana na uzazi ni 15.
Kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka 2023,
wajawazito waliojifungulia nyumbani ni 1,450, kwa upande wa wilaya ya Mkoani
walikua ni 270, Chake chake 99,
Micheweni 230 na Wete ni 292.
Ingawa wanaojifungulia Hospital kwa Pemba ni 8481,
ambapo kwa wilaya ya Mkoani ni 1562,
Chake chake 2601, Wete 2140 na Micheweni 2178, huku vifo vikiwa tisa [9],
ambapo Wete na Micheweni kulikuwa na vifo vitatu vitatu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment