NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAUSHIRIKA wa ‘jambo nia’ wa kijiji cha Fuuweni shehia ya Mfikiwa
wilaya ya Chake chake, wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki, wamesema wanategemea,
kujiingizia wastani wa shilingi milioni 1.6, ikiwa mizinga yao 13, itazalisha chupa
65 za asali.
Walisema, fedha hizo wanategemeza kuzipata, miezi minne ijayo kutoka
sasa, kupitia mzinga yao 13 walioitega mwaka jana.
Walieleza kuwa, fedha hizo zitatokana na kuuza chupa 65, wastani wa shilingi
25,000 hadi 30,000 kwa chupa moja, yenye ujazo wa lita moja.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, walisema
waliamua kuanzisha kilimo cha nyuki, kwa malengo kadhaa, ikiwemo kujipatia kipato
na kuhifadhi mazingira.
Walieleza kuwa, kupitia mizinga hiyo 13, kama hakutavuna upepo mkali ukiambatana
na mvua, wanategemea kila mzingia, kuvuna chupa tano, na kujipatia chupa 65 kwa
mizinga yote.
Mwenyekiti wa ushirika huo Hassein Khamis Salum, alisema wazo hilo,
lilikuja kuanzia mwaka 2022, baada ya fedha zao za hisa kukua.
Alieleza
kuwa, kutokana idadi ya wanachama wao 23, walikuwa na uwezo wa kukusanya
shilingi 506,000 kwa mwezi na kujikuta wanatimiza zaidi ya shilingi milioni 6,
kwa mwaka na kuamua kuanzisha mradi wa huo.
‘’Ilipofika
mwisho wa mwaka tuliamua tusigawe, bali tukopeshane, ingawa wastan wa shilingi 700,000
tulielekeza kwenye ufugaji ya nyuki, na ndio hizo tunatarajia zikazae shilingi milioni
1.6,’’alieleza.
Kwa
upande wake Msaidizi Katibu wa ushirika huo Salim Msellem Salum, alisema huku
hisa inaendelea na ufugaji nyuki ukiendelea, kwa lengo la kujisaidia maisha.
‘’Tumeshaona
kuwa serikalini ajira hazitosehelezi, na ndio maana tukamua kuunda ushirika
huu, ili kujiwekea hisa na kisha kukopeshana, na kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki,’’alieleza.
Alieleza
kuwa, malengo yao ya baadae ni kuangalia uwezekano kwa wanachama wao 23, waweze
kujiajiri na kisha nao kuwaajiri wingine.
Mwanachama
wa ushirika huo Ali Thabiti Ali, alisema tokea aingie kwenye ushirika huo, manufaa
makubwa anayaona na kuwa na sehemu ya uhakika ya kukopa.
‘’Kabla
sijaingia kwenye ushirika wetu wa ‘jambo nia’ sikua na uhakika wapi naweza kukopa
kati ya shilingi 200,000 hadi shilingi 300,000 lakini sasa nnapo,’’alieleza.
Hata hivyo wanaushirika hao, wamewaomba wafadhili
kuangalia uwezekano wa kuwapa mafunzo na mbinu zaidi za ufugaji nyuki, na kuongezewa
idadi ya mizinga.
Sheha wa Mfikiwa Bimkubwa Rajab Tangwi, alisema amekuwa
bega kwa bega kwa ushirika huo, ili kuhakikisha anawasaidia, ikiwemo
upatikanaji mikopo.
‘’Miongoni
mwa ushirika ambao unafanyakazi kwa bidii na kwa malengo ni huu wa ‘jambo nia’,
hivyo nimeshausaidia mambo kadhaa ikiwemo mafunzo na kuwaunganisha na wataalamu,’’alifafanua.
Baadhi ya wananchi wa shehia hiyo, walisema vijana
hao wamekuwa mstari wa mbele, kufanyakazi kwa bidii na malengo.
Waziri
wa Nchi Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Sharif Ali Sharif, wakati akiwasilisha
hutuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025, alisema serikali, inaimarisha sekta ya ushirika,
ili kuleta ufanisi wa kutoa ajira, kunyanyua pato la mwananchi na uchumi wa nchi.
Sekta
hiyo inashajiisha uundaji wa vyama vya ushirika, kwa lengo la kuwaweka pamoja,
ili kupata huduma kadhaa, ikiwemo mafunzo ya ujuzi na mitaji.
Ndio
maana, alieleza kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wizara imesajili vyama vya ushirika1,
560 ikilinganishwa na vyama 1,822 kwa mwaka 2022/2023.
Waziri
Sharif anasema, wamepiga hatua katika utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali,
katika maeneo ya ufugaji wa nyuki, usarifu wa matunda na mboga, utengenezaji wa
vifaa vya sola, masoko, ujasiriamali na mafunzo ya uokaji.
Hili
linatajwa kuongezeka kutoka wajasiriamali 1,239 kwa mwaka 2022/2023 hadi
kufikia 3,979, ambapo Unguja ni 1963 na Pemba 2,016, kwa mwaka 2023/2024.
Mwisho
Comments
Post a Comment