NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAANDISHI wa habari
na wana asasi za kiraia Pemba, wametakiwa kufanyakazi kama mwili mmoja, ili
wanapofuatilia kero za wananchi, iwe kazi rahisi kuzipatia ufumbuzi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi
wa Mwemvuli wa asasi za kiraia Pemba ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, wakati akiufungua
mkutano wa siku moja, kwa waandishi hao wa habari na wanaasasi za kiraia Pemba,
mkutano uliofanyika leo Juni 21, 2024 ukumbi wa Maktba Chake chake.
Alisema, waandishi
wa habari na wanaasasi za kiraia, imegundulika wote wanawatetea wananchi wanaokabiliwa
na changamoto, mfano ya ukosefu wa barabara, hivyo ni vyema wakashirikiana katika
hilo.
Katika hatua
nyingine Najim, alisema ushirikiano kati ya pande mbili hizo, unaweza hata
kubadilisha sera na sheria, ambazo zinaonekana kupitwa na wakati, katika uendeshaji
wa shughuli zao.
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, alisema anategemea baada ya kumalizika kwa
mradi huo, kuweko na mabadiliko makubwa ndani ya jamii.
‘’Kwa mfano kundi
la wanawake na watoto, limekuwa likikumbwa na majanga mbali mbali na kisha
hukosa haki zao, hivyo ushirikiano wa waandishi wa habari na wanaasasi unaweza
kusaidia,’’alieleza.
Akiwasilisha mada
ya umuhimu wa ushirikiano kati ya waandishi wahabari na wanaasasi za kiraia,
Afisa Mawasiliano wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Gaspery Charles, alisema lazima kila mmoja ajue
kuwa anategemewa na mwenzake.
Alieleza kuwa,
waandishi wa habari moja ya vyanzo vyao ni wanaasasi, kama ilivyo kwao, kwamba
hawawezi kufanikiwa pasi na kuvitumia vyombo vya habari.
Wakichangia mada
kwenye mkutano huo, washiriki hao walisema, wamepata uwelewa na njia za kushirikiana
na waandishi wa habari, katika kazi zao.
Khadija Sultan,
alisema kilichobakia sasa baada ya mkutano huo, ni kukaa pamoja na vyombo vya
habari, ili sasa kushirikiana katika kazi zao.
Mwandishi wa ZBC
Khadija Kombo, Is-haka Mohamed wa ZENJ FM na Khadija Ahmed wa Redio jamii
Mkoani, walisema, umoja na mshikamano unaweza kufanikisha kila kitu.
Walieleza kuwa, baada
ya mafunzo hayo, watazidisha ushirikiano kati yao na wanaasasi za kiraia, kwa
ajili ya kuyaripoti maono na changamoto zao.
Akiufunga mkutano
huo, Mwenyekiti wa PACSO Mohamed Ali Khamis, alisema atafurahi kama maazimio sita
yalioibuliwa hapo, yatafanyiwa kazi.
Alieleza kuwa, wazo
la kufuatilia ahadi za ujenzi wa barabara ya Chake chake- Mkoani, vitendo vya
udhalilishaji, mporomoko wa maadili, dawa za kulevya na uharibifu wa msitu wa
Ngezi ni maeneo ya kuwekewa mkazo.
Mkutano huo, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi
wa ‘uraia wetu’ unaotekelezwa na ‘PACSO’ kwa muda wa miaka minne, kwa ufadhili
wa The Foundation For Civil Society kupitia Umoja wa Nchi za Ulaya ‘EU.’
Mwisho
Comments
Post a Comment