NA MWANDISHI WETU, PEMBA@@@@
JAMII imetakiwa kuendelea kuwasimamia na kuwapatia
huduma stahiki ndugu zao ambao wamejaaliwa kuwa ni walemavu wa akili, kwani
kuwatenga na kuwaficha kutazidi kuwafubaza kifkira na kimakuzi.
Wito huo umetolewa na
Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Ahmed Abuubakar alipokuwa
akizungumza na wazazi na walezi, wenye watoto wenye ulemavu wa akili na
wananchi, waliohudhiria katika ftari ya pamoja iliyofanyika Tibirinzi Kiwanja
cha Kufurahishia watoto wilaya ya Chake chake.
Alisema licha ya kujaliwa
kuwa na ulemavu wa akili lakini, watu wa kundi hilo wanakuwa na mitazamo mizuri
pale wanapokuwa hawatengwi na familia, au jamii kwa kuweza kushirikishwa katika
mambo tofauti.
Mdhamini huyo
alilisisitiza, umuhimu wa kuwatoa watoto na watu wenye ulemavu kujumuika na
kupatiwa haki zao mbali mbali ikiwemo elimu, afya pamoja na kuweka mazingira ya
kujichanganya na wenzao.
Hata hivyo amesifu mwamko
wa wazazi na walezi wa kuwasimamia vyema vijana wao, wenye ulemavu wa akili
kwani kwa juhudi hizo za kuwasimamia na kuwa nao karibu kwa kuwashirikisha kwa
sasa imekuwa nadra kuwakuta watu hao.
Katika hatua nyengine Afisa Mdhamini huyo, ameipongeza
jumuiya kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar, ZAPDD kwa hatua ya
kuwaweka pamoja watu wanye ulemavu wa akili katika futari hiyo.
Aidha Mdhamini huyo
amesema Ofisi ya Makumu wa Kwanza wa Rais ambayo ndiyo yenye dhima ya kusimamia
watu wenye ulemavu Zazniabar, itasimamia na kupigania upatikanaji wa maslahi ya
watu wenye ulemavu kwa wakati.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Jumuiya kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar ‘ZAPDD’ Mkubwa Ahmed Omar
amesema kuwa walikuwa na utaratibu wa kuandaa futari kwa wanachama wao kwa
ngazi ya mkoa, ingawa kwa mwaka huu wameamua kuwakutanisha kwa pamoja.
Amewaomba wadau kuwa
mstari wa mbele katika kutetea haki za watu wenye ulemavu, pamoja na
kuwashirikisha katika shughuli mbali mbali za kijamii na wasiwachukulie kama ni
watu wa kichekesho au kiburudisho.
Kwa upande wake Mratibu wa
Ofisi ya Mufti Pemba Sheikh Said Ahmad Mohamed, amesema jamii haipaswi kuwatesa
watu wenye ulemavu wa akili, kutokana na hali zao kwani ni matakwa ya Muumba
mwenyewe.
Aidha Shekh Said ameahidi
kushirikiana na watu wenye ulemavu wa ajili na makundi mengine ya watu hao, na
kusema milango ya Ofisi ya Mufti Pemba ipo wazi wakati wote kwa ajili ya
kushikiana nao.
Mapema Mratibu wa Jumuiya
ya Watu wenye ulemavu wa akili Pemba Khalfan Amour Mohamed amewashukuru wadau
mbali mbali waliofanikisha ftari hiyo sambamba na kuwaomba kutosita kuwaunga
mkono pale watakapokuwa na uhitaji.
Aidha amemwomba Ofisa
Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais kuendelea kuwapa ushirikiano zaidi katika kuzitatua na changamoto na kutetea haki za
watu wenye ulemavu.
Mwisho
Comments
Post a Comment