NA
HANIFA SALIM, PEMBA@@@@
UTELEKEZWAJI
wa familia ni ukatili wa kijinsia, hali hii husababisha chuki, maradhi, udhalilisha
na watoto kukosa haki zao za msingi.
Jukumu la malezi ni la wazazi wote wawili, kupanga matumizi ya
rasilimali za familia na mahitaji ya watoto ni jambo la kupewa kipaumbele.
Katika jamii ya sasa, wanawake waliowengi tumeona wakiachwa na waume
zao pamoja na watoto, jambo ambalo huleta athari, watoto kukosa haki zao wakati
mwengine hata kufanyiwa matendo yasiofaa.
Kutokana na kukosa huko huduma, kutoka kwa familia zao ndipo
wanapodhalilishwa kwa kushawishiwa, kupatiwa jambo dogo ambalo alilikosa na
alistahiki kupatiwa na familia yake.
ATHARI
ZINAZOIKUMBA FAMILIA ILIYOTELEKEZWA
Zipo athari nyingi ambazo huikumba familia ambayo imetelekezwa ikiwemo
mama kubeba mzigo mkubwa wa majukumu wa kuwatafutia watoto huduma muhimu kama
vile chakula, matibabu, elimu na mengineyo.
Watoto kukosa watu wa kuwadhibiti ambapo huweza kutumbukia katika
majanga mbali mbali ikiwemo ubakaji, madawa ya kulevya, ulawiti, uchokoraa na
ajira za watoto.
Watoto wengi wanaoacha skuli asilimia kubwa wameonekana kutoka katika
familia ambazo zimetelekezwa, mama kukosa nguvu kazi ni sababu ambayo pia
inatokana na utelekezwaji wa familia.
Changamoto ni nyingi ambazo humfika mwanamke anapotelekezwa na watoto,
wakati mwengine watoto hupatwa maradhi, hukimbia kwenda skuli na madrasa jambo
ambalo ni haki yao ya msingi.
WAHANGA
WENYEWE
Akizungumza na mwandishi wa Makala, hii mmoja miongoni mwa wahanga wa
janga hilo la utelekezwaji mkaazi wa shehia ya Chonga anasema, ni miaka mitano
sasa tangu kuachwa na mume wake wa ndoa.
“Mume amenikimbia huu ni mwaka wa tano, nimezunguka katika taasisi
zote za sheria kutafuta haki, lakini sina ambacho nimefanikiwa, nimeachwa na
watoto wawili wakiume mmoja akiwa ni mlemavu,” anasema.
Anasema, alikwenda kituo cha huduma za sheria, wanawake na watoto,
bila ya kupata mafanikio yoyote, hadi alikata tamaa huku mtoto wake mmoja
kupoteza maisha.
“Yule mgonjwa ambae ni mlemavu wa akili alinitoka ghafla, mimi
mwenyewe nahangaika huku naumwa, ili tupate riski nile na watoto baba yao
kanitelekeza muda mrefu”, anaeleza.
Alipambana kwa juhudi kubwa kufika hadi dawati, wanawake na watoto
hakuna ambalo lilifanyika, wala kupata haki yake ambayo aliitegemea.
“Nende wapi nikatafute haki baada ya kumaliza sehemu hizo, ambazo
nilikwenda bila ya kupata mafanikio yoyote, na hawa ndio daraja la kufika pale
ambapo haki yangu ipo”, anasema.
Anasema vituo vya sheria bado havijawa tayari kuisaidia jamii katika
masuala ya utoaji wa huduma, kwani kupitia madhila ambayo aliyapata katika
maisha yake, alibaini jambo hilo.
Baada ya kufuatiliwa na kituo cha huduma za sheria, aliambiwa mwanamme
ambae ni baba wa watoto wake, yuko kisiwani Unguja.
“Kwani Unguja ni Dubei au kuna umbali gani wakusema sheria haziwezi
kumkamata, kama kafanya kosa kubwa la uhujumu uchumi asingetiwa hatiani?, lakini
kwa vile ni mimi walishindwa kumpata”, anauliza.
Anasema, aliendelea kudumaa na kukosa haki zake kwa mwanamme ambae aliishi
nae kwa muda wa miaka 40, tangu afunge nae ndoa.
Kazi zote za kiume alilazimika kuzifanya ili tu ahifadhi maisha ya
ndoa yake pamoja na watoto wake ambao walikua ni walemavu lakini juhudi za
kupambania familia yake zilikwisha.
“Samaki niliuza mimi, nazi, Mombasa nilikwenda mimi kufanya biashara,
gari ya Ng’ombe nimeendesha, kuni nimekata, nikiendesha gari la ng’ombe huwezi
kuamini, niletee Ng’ombe wowote hata awe mkali hatonishinda”, anaeleza.
Yote hayo ambayo yalimkuta alifunzwa na mwanamme huyo ambae
alimtelekeza, alijitahidi kwa uwezo wake wote kuhakikisha analinda ndoa yake,
lakini hakupata ndoa wala haki yake ambayo aliipigania kwa muda mrefu.
Alizishauri taasisi za sheria kuzisemea haki za wanawake kwa mdomo na
vitendo pamoja na kuziangalia kwa kina kwani wanawake waliowengi katika jamii wanaathirika
kwa kuachwa na watoto.
Mama mwengine ambae alitelekezwa mkaazi wa shehia ya Msuka Magharibi anasema,
aliachwa na mume wake akiwa na watoto wanne wakike.
“Mwanzo alikua anatupatia huduma baada ya kuniacha kindoa lakini sasa
hivi ni karibu mwezi wa tisa hatuulizi hata hali zetu, ni mimi mwenyewe ambae
napambana na watoto”, anasema.
Alibadilika ikawa watoto hawashuhulikii kwa lolote, apambana na watoto
wake kwa kuwatafutia riski kwa kupitia shughuli zake za kilimo ambacho
kinamsaidia katika maisha yake.
“Kama si kilimo na kwenda kutafuta nazi nikafanya mafuta nikauza
nikapata pesa ya chakula basi tunalala njaa, tunaathirika sana na haya maisha
wanawake majukumu ambayo tunaishi na watoto wetu ni magumu mno”, anasema.
WANASHERIA
WANASEMAJE
Wakili kutoka chama cha wanasheria Pemba Asha Suleiman Said anasema, mambo
yanayopelekea kuongezeka masuala ya utelekezwaji wa wanawake na watoto kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa na chama chao ni jamii kukosa elimu ya sheria.
Wanawake kuwa na muhali, kwa kuhofia kuwapoteza ndoa zao pale ambapo
wanaonesha dalili za manyanyaso na udhalilishaji ambao wanaufanya kwao, kutoyaripoti
masuala hayo katika vyombo vya sheria.
Anasema, suala hilo linapotokea wanaoathirika zaidi ni watoto kwani
watoto wengi hufanyiwa udhalilishaji kutokana na kukosa malezi na uwangalizi wa
wazazi wao.
“Mwanamme anapokuacha akawa hakuhudumikii huo ni utelekezaji
linapotokezea suala hili tunachotakiwa wanawake tusikae kimya tuyaripoti katika
vyombo vya sheria ikiwemo Idara ya ustawi wa jamii ili kupata haki zetu”,anasema.
OFISI YA
WILAYA
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya anasema, kesi za
utelekezwaji wa akina mama na watoto ni nyingi sana ambapo kesi hizo zimeonekana
kujitokeza zaidi katika maeneo ya ukanda wa pwani.
“Serikali ya Wilaya ndio ambayo inabeba mizigo maana wanatujia akina
mama kutwambia leo ya nne hajakula na watoto anakuja kutafuta chakula kwetu,
tunachokifanya ni kutafuta mawasiliano ili waweze kutoa huduma”, anasema.
Wanaume walio wengi wameonekana kuwakimbia wake zao pamoja na watoto
na kwenda nje ya kisiwa cha Pemba kama vile Tanga, Mombasa, Unguja na Kenya
kujenga familia mpya.
“Jamii ya makaazi ya ukanda wa pwani ni wavuvi wanapokwenda ago miezi
minne au mitano huziacha familia zao bila ya huruma, na wengine huwaacha
kabisa”, anasema.
Anasema jambo hilo linawapa hali ngumu akina mama, kwani hulazimika
kutafuta riski ili watoto wao waweze kuishi, hivyo wilaya imechukua hatua za
kutoa elimu kwa wanaume wa kila shehia ili kupunguza matendo hayo.
USTAWI
WA JAMII
Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii jinsia na watoto Pemba Mwanaisha
Ali Massoud anasema, mwezi Julai 2021 hadi Juni 2022 wamepokea malalamiko ya
kesi 126, kati ya malalamiko hayo 71 walalamikaji wamepata haki zao.
“Wanapokuja walalamikaji tunawasikiliza kwa kina halafu tukawapa
ushauri ili kuona wanashirikiana wazazi wa pande mbili katika malezi ya watoto wao”,
anasema.
Kupitia makala hii anaishauri jamii kuwa na subira katika uwendeshaji
mzima wa familia zao, kuzitumia familia zao kuweza kupata suluhu juu ya
matatizo walionayo.
Wazazi wanapofanya migogoro ndani ya familia zao watambue ndio kizingiti
kikubwa cha familia kukosa maendeleo ya haraka hivyo, lazima wanandoa wawe
makini huku wakitambua kwamba waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.
TAMWA
Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA)
Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, wamekua wakiwasaidia wanawake ambao
wametelekezwa kwa kuwapa ushauri wa kupeleka malalamiko yao Idara ya ustawi wa
jamii.
“Tunawaunganisha na Idara ya ustawi wa jamii, mahakama ya kadhi ili
waweze kupata haki zao, mwaka jana hatukua na kesi utelekezwaji kwani sisi
zaidi tunashuhulikia kesi za udhalilishaji wa kingono”, anasema.
Anasema, mwaka 2021 walipokea kesi 61 kwa Wilaya ya Wete, 48 Mkoani,
huku akiwataka akina baba kufahamu kwamba familia hulelewa katika pande mbili
hivyo aliwanasihi wawe na subra pamoja na kuwapatia huduma watoto wao licha ya
kuwa ndoa imeshavunjika.
WANANCHI
WANASEMAJE?
Fatma Hamad Khamis mkaazi wa Gombani anasema, wanaume wamekosa huruma
na mapenzi kwa wanawake na watoto wao kwani majukumu yote ya familia huwaachia
na kuona kwamba ni adabu ambayo humpa mwanamke baada ya kuachana.
‘’Wanaume wanapokutaka watakufuata kwa mahaba, lakini kinyume chake
hutokezea ambapo kutatokea mfarakano wa ndoa yao, wanatuacha na watoto bila ya
kuelewa kwamba watoto wanahitaji huduma kutoka kwa baba’’, anasema.
Abdalla Mohamed Ramadhan mkaazi wa machomane, anasema wapo wanaume
ambao wamekosa uwelewa wa kutambua majukumu yao pale ambapo wameachana.
‘’Mwanamke uapomuacha na watoto unamuachia mzigo mkubwa ambao yeye
hatoweza kuumudu, nawashauri wanaume wenzangu wajenge utamaduni wa kuwapatia
huduma watoto hata pale wanapotengana’’, anasema.
Salama Kassim Haji mkaazi wa Mwambe anasema, familia inapotelekezwa
kinachotokezea ni kuwaathiri watoto kufanyiwa udhalilishawaji na watu wabaya
kutokana na kukosa huduma stahiki ambazo walizikosa.
NINI
KIFANYIKE?
Ni vyema jamii kuzitumia familia
zao kuleta suluhu katika kutatua matatizo yao ili kuepusha uvunjifu wa ndoa na
kuongezekeza idadi kubwa ya malalamiko ya kesi za utekelezwaji wa wanawake na
watoto ndani ya jamii.
Kwani jamii ya sasa imeonekana
kutokuzitumia familia zao kutatua changamoto kama ilivokua zamani jambo ambalo
linachangia kwa kiasi kikubwa uvunjifu wa ndoa.
Vile vile kuwa na subra katika uendeshaji
wa familia, wazazi watambue wanapofanya migogoro ndani ya familia kutakuwa na
kizingiti cha kutokupata maendeleo ya haraka.
SERIKALI KUU
Akisoma hutuba ya mwaka wa fedha
2022/2023 ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma, alisema kwa mwaka huo walipokea malalamiko
373 ya ukiukwaji wa haki za watoto na
kuyafanyia kazi.
Kati ya hayo, yaliyopokelewa Unguja yalikuwa
151 na Pemba 222, ambapo yanayohusu matunzo ya huduma yalikuwa ni 211 Unguja 79
na Pemba 132, na 162 ya mvutano wa malezi wakati kwa Unguja yalikuwa 72 na
Pemba 90.
Malalamiko 167 yalipatiwa ufumbuzi na
malalamiko 25 yalitolewa rufaa kwenda mahakamani, wahusika 100 walikubaliana
kifamilia na 81 wanaendelea na hatua.
MWISHO.
Comments
Post a Comment