NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
“TULIKUWA tunazurura
ovyo mitaani, kukaa vijiweni, hali ambayo ingeweza kuhatarisha maisha yetu,
kwani tungejiingiza katika makundi hatarishi na hatimae jela, lakini kwa sasa
tupo busy kutafuta pesa”, …hayo ni maneno ya baadhi ya vijana waliokabidhiwa
mkopo wa bodaboda Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Vijana hao
waliopatiwa mkopo wa bodaboda na Serikali kupitia benki ya CRDB kwa lengo la
kuwainua kiuchumi, ambapo kwa sasa wameimarisha maisha yao kupitia ajira hiyo.
Ali Issa Ali mwedesha
bodaboda anasema, uendeshaji wa huo wa bodaboda umempa mafanikio kwa sababu
kabla ya kupata mkopo huo alikuwa na maisha duni kiasi ambacho alikuwa hajui
atapata wapi kazi ya kuendesha maisha yake.
“Ilikuwa sina kazi
hata moja, kazi yangu kubwa ni kuzurura tu mitaani, lakini kwa sasa nashkuru
nimejiajiri na napata pesa ya kujikimu kimaisha, Dk. Mwinyi amefanya kitu cha
muhimu kwetu vijana, tunampongeza”, anaeleza.
Anasema, kipato
anachopata kutokana na uendeshaji wa bodaboda unakidhi mahitaji yake ni tofauti
kabisa na kukaa nyumbani bila ya kazi yeyote.
Kijana ambaye
hakutaka jina lake litajwe anaeleza kuwa, wamenufaika sana na mkopo huo kwani
vijana wengi wamejiepusha na madawa ya kulevya pamoja na uzururaji usio na
maana.
“Muda wote vijana
wapo kazini, hawana muda wa kukaa vijiweni kufanya mambo yasiyofaa,
tunamshukuru Rais wetu kwa kutuwezesha kupata hizi bodaboda, kwa sababu zamani
tajiiri alikuwa anataka kila siku 10,000 lakini kwa sasa anataka 8000”,
anasema.
Ali Mohamed Juma
anasema, amenufaika sana kwa biashara hiyo ya bodaboda kwani ameweza
kuwasomesha watoto wake ambao anaamini wakipata elimu itakuwa tegemeo la maisha
yao ya baadae kwa kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha.
Anasema kuwa, kwa
siku anaweza kupata zaidi ya elfu 50, hivyo anapata kiasi cha kukidhi mahitaji
yake kwa siku, ingawa sio kingi lakini amepiga hatua kubwa kimaisha tofauti na
mwanzo.
“Inategemea na abiria
wenyewe lakini tunashukuru kupata mkopo huu, kwani umetutoa katika hali duni
tuliyokuwa nayo kipindi cha nyuma, kwa kweli hakuna kupata kudogo”, anaeleza.
Mohamed Nassor
Mohamed anasema, wamenufaika na mkopo wa bodaboda waliopewa na Rais kwani
wameondokana na dimbwi la umasikini, kukaa ovyo bila ya kazi yeyote na kupungua
kuitwa wizi.
“Kwa sasa nahudumia
familia yangu kwa kile ninachokipata, tunapata kiasi si kama kukaa tu na
kusubiri wazee watulishe, hii ni faraja kubwa kwetu”, anaeleza.
Hamad Maulid Suleiman
anaeleza kuwa mkopo huo umewanufaisha sana kutokana na vijana wengi walikuwa
hawana kazi, lakini kwa sasa wamejiajiri kupitia bodaboda na maisha yanakwenda
vizuri.
“Sasa tupemapata
ajira, tulikuwa vijana wa maskani tu hatujui tufanye kitu gani ili kupambana na
maisha lakini tunaishukuru Serikali hii ya awamu ya nane kwa kutuona sisi
vijana na kututafutia ajira”, anaeleza.
Anafafanua kuwa,
wakati wa kampeni yake Dk. Mwinyi aliahidi ajira laki tatu kwa wananchi
wakiwemo vijana na wameliona hilo kwa sababu vijana wamepata mikopo ya bodaboda
na wengine wamepata mikopo ya kuwawezesha katika vikundi vyao vya ujasiriamali.
“Kwa kweli Rais wetu
amaejitahidi sana kwa hili, kinyume chake vijana wengi tungepotea njia kwa
kujiingiza katika makundi maovu na hatimae kuishia jela”, anasema.
Mwenyekiti wa
bodaboda ambazo zina leseni Seif Hamad Said anaeleza, mafanikio wanayopata kuwa
ni mazuri kwani vijana ambao wengi hawana kazi wapepata biashara ya kuendesha
bodaboda, ambapo kwa sana wana uhakika wa kupata milo mitatu kwa siku.
“Kuna vijana walikuwa
wameanza kujiingiza katika vitendo vya wizi, uvutaji bangi na mambo mengine
mabaya lakini kupitia mkopo huo umefanya yote hayo wayaache na watafute fedha
za halali za kujikimu kimaisha”, aneleza.
Kwa mujibu wa taarifa
za Mkoa wa Kusini Pemba za mwaka 2022
kuna jumla ya bodaboda 145 walizopewa vijana kwa mkopo, kati ya hizo bodaboda
100 zinatoka Wilaya ya Chake Chake na 45 kutoka Wilaya ya Mkoani.
Mathalani Wilaya ya
Chake Chake, yenye bodaboda 100 ikiwa kila dereva moja atakuwa na familia isiyopungua
ya watu watatu basi wastani wa watu 300 watakuwa ni wanufaika na uchumi
unaotokana na bodaboda hizo kila siku.
CHAGAMOTO
ZINAZOWAKABILI VIJANA HAO
Mwendesha bodaboda
Hussein Saleh Khamis anaeleza kwamba, pamoja na kunufaika sana na mkopo huo,
lakini wanakabiliwa na changamoto ya urejeshaji wa mkopo kwani watu wa benki
hawajui kuumwa wala kukosa pesa, wanachojua wao ni kulipwa pesa zao tu kila
siku.
“Tunajitahidi kadiri
ya uwezo wetu kulipa, lakini wakati mwengine mtu hajaweza kutoka kwa kuumwa ila
kila siku anatakiwa arejeshe shilingi 8000, jambo ambalo ikiwa unaumwa ni ngumu
kuipata, kwa sababu hata kuendesha mtu mwengine hawaruhusu”, anaeleza.
Anasema kuwa, Dk.
Mwinyi aliwapa muda wa mwaka mmoja na nusu kurejesha mkopo hiyo, ingawa ikifika
mwezi hujalipa wanazichukua bodaboda, jambo ambalo linawanyima amani.
Anafafanua kuwa,
angalau wangesubiri kijana aliefika miezi mitatu mpaka sita ikiwa hajalipa au
hajafikia hata nusu ya kiwango kilichowekwa, ndipo waichukue bodaboda hiyo.
“Ikiwa amekwama wiki
mbili mpaka mwezi kwanza afuatiliwe na kuangaliwa hali yake anaendeleaje? Na
sio kuchukua maamuzi ya kuichukua pikipiki tu, pengine mtu ni mgonjwa, ataitoa
wapi pesa?”, anasema.
Mohamed Nassor
Mohameda anaeleza kuwa, changamoto ni kutokuwa na amani wanapokuwa barabarani
kwa sababu, walipopewa mkopo waliambiwa kuwa hawatakuwa na shida yeyote kwani
itakuwa na bima kamili na vitu vyote vimekamilika kweli, ingawa askari wamekuwa
wakiwasumbua muda wote.
“Kwenye urejeshaji wa
mikopo sijapata usumbufu wowote, lakini wenzangu nawasikia wanasema,
wanapochelewesha kupeleka pesa wastani wa siku moja, mbili basi wanapokonywa
pikipiki na wanaziweka mpaka utakapokwenda kulipa, hii inazorotesha maendeleo
yao kwa kweli”, anasema.
“Vikoti tulipewa
siku tuliopokabidhiwa pikipiki, lakini kinachotushangaza sasa hivi tunaambiwa
tununue vikoti vyengine ambavyo vinauzwa shilingi 25,000, hii inazorotesha
maisha yetu, kila siku watu waibue mbinu mpya ya kututoza pesa tu kiholela”,
anasema dereva Hamad Maulid Suleiman.
NINI KIFANYIKE ILI
KUBORESHA ZAIDI
Huessein Ali Khatib
anasema, Serikali iangalie katika utendaji wao wa kazi katika urejeshai wa
mikopo kwa sababu biashara ni ngumu kutokana na hali ya mzunguko wa watu
kisiwani hapa kuwa ni mdogo huku wana familia zinawategemea.
“Siku nyengine chombo
kinahitaji matengenezo kwa hiyo lazima uweke pesa ya hakiba kwani ni sawa na
mtoto inahitaji kulishwa, kwa hiyo watufanyie ahueni kidogo”, anasema.
Mohamed Nassor
Mohamed anasema, kuna mambo ambayo hayafuati utaratibu, kwa sababu kuna ajenda
ya kikoti lakini wanatakiwa kupewa wale waliokamilisha usajili, ingawa kwa sasa
anapewa yeyote, jambo ambalo linawaumiza wao ambao wameshafuata taratibu
zote.
WANANCHI/ABIRIA
Hafsa Ali Said
anasema, jambo alilolifanya Dk. Mwinyi ni la maana sana kwa sababu amewatoa
vijana katika dimbwi la matatizo na kuwapeleka katika mwanga, hivyo vijana
waendelee kuzitumia fursa hizo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
“Vijana wengi siku
hizi wanaendesha bodaboda na bajaji, wamepunguza uzururaji, hivyo Serikali
iendelee kuwawezesha vijana kwa kuwapa mitaji itakayowasaidia katika maisha yao
ya kila siku”, anasema.
Fatma Ali Yussuf
anasema, usafiri wa bodaboda umewarahisishia safari zao, kwani hata unapokweda
sehemu zisizofika gari wao wanafika, wanajivunia kwa kweli.
“Zamani mtu anakuwa
na mzigo, anapokwenda daladala hazifiki, tulikuwa tunapata usumbufu kwa sababu
hupati hata mtu wa kukupelekea mzigo, lakini kwa sasa maisha yamekuwa rahisi
mno kwa usafiri wa bodaboda.
Suleiman Khamis Ali
anawataka waendesha bodaboda kupunguza mwendo wakati wanapokuwa barabarani, ili
kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
SERIKALI YA
WILAYA
Khatibu Juma Mjaja
ambae anakaimu Wilaya ya Chake Chake anasema kuwa, Serikali imekuja na mikakati
tofauti kuhakikisha inaondoa tatizo la ajira kwa wananchi wake, ikiwa ni pamoja
na kutoa mikopo kwa wajasiriamali.
‘’Boda boda
zilikuwepo ingawa hazikuwa nyingi, lakini Serikali imewekeza kwa kuwapatia
vijana bodaboda za mkopo kwa lengo la kupata ajira, wajitegemee na waweze
kujikwamua kimaisha’’, anaefahamisha.
Anaelezea mafanikio
yaliyopatikana kuwa ni vijana kujiajiri, kuoa na kuweza kuhudumia familia zao,
kupunguza kukaa vijiweni hali iliyosaidia kutokujiingiza katika makundi
hatarishi.
‘’Kuna vijana
walishindwa kuoa kutokana na kukosa ajira, lakini baada ya kupewa bodaboda hizo
za mkopo, wameoa na sasa wanahudumia familia zao, kwa kweli ni faraja kwetu’’,
anasema.
Mkuu huyo wa Wilaya
anawataka vijana hao kufanya kazi kwa bidii na warejeshe mikopo kwa wakati, ili
na vijana wengine wapatiwe mkopo huo kwa lengo la kujikomboa na umasikini.
Anasema kuwa, hiyo ni
fursa kubwa kwa vijana katika kukuza uchumi wao, hivyo wanatakiwa wazalishe
bodaboda nyingine kwa ajili ya kutoa fursa ya ajira kwa wengine au kuzalisha
mradi mwengine wowote ambao utamsaidia katika maisha yake.
‘’Nawambia vijana
kuwa hiyo ni fursa kwao, waitumie vizuri kwa ajili ya kuzalisha na sio
kusababisha ajali ambazo zinaleta maafa kwa taifa letu na tusizitumie kwa
kufanya uhalifu kwani lengo la Serikali ni kuwakwamua kiuchumi’’, anaeleza Mkuu
huyo.
Kwa mujibu wa utafiti
uliofanyika mwaka 2020/2021 Zanzibar, katika Bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya
Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji imeeleza kuwa, vijana wenye uwezo wa
kufanyakazi ni kati ya miaka 15 hadi 35, huku ukosefu wa ajira ukiongezeka.
Ukosefu wa ajira
umeongezeka kutoka asilimia 24.6 ya mwaka 2014/2015 hadi kufikia asilimia 27.6
ya mwaka 2020/2021, ambapo wathirika wa kubwa ni vijana ambao ndio nguvu kazi
ya Zanzibar.
Kipato cha nchi
hakiwezi kutosheleza kuwaajiri vijana wote, hata hivyo kwa mujibu wa mpango wa
maendeleo wa mwaka 2021-2026, wanatarajia ukosefu wa ajira kupungua na
kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2026, kutokana na miradi mipya na
inayoendelea.
Kila boda boda moja
ina thamani ya shilingi milioni 3,700,000 ambapo vijana waliopata mkopo wa
bodaboda hizo wanatakiwa kulipa kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.
MWISHO
Comments
Post a Comment