NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
KAMISHNA wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Hamad Khamis Hamad, amesikitishwa na tabia ya watanzania, kuendelea
kujichukulia sheria mikononi, jambo ambalo wakati mwengine husababisha vifo kwa
watuhumiwa.
Alisema,
tabia hiyo sio mwenendo mzuri kwa watanzania, kwani serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanania na ile ya Zanzibar, zimeanzisha vyombo maalum, vya kushughulikia
jinai na madai.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa njia simu, alisema zipo mahakama mbali mbali,
jeshi la Polisi, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka na ofisi za wapelelezi,
ambazo zimewekwa kazi hiyo.
Alieleza
kuwa, sheria zinaelekeza wazi wazi mara baada ya jamii kumshutumu mtu kutenda
kosa, liwe la jinai ama madai, ni kumlalamikia katika vyombo vya sheria, lakini
sio kujichukulia sheria mikononi.
Kamishna
huyo alisema, anakerwa mno na jamii kuendelea kuwaondoshea uhai watuhumiwa wa
makosa mbali mbali, kwani kazi ya kutoa hukumu, imepewa mahakama.
‘’Utamaduni
wa kila mtuhumiwa kuuawa sio wa watanzania, kwani zipo taratibu za kisheria,
tena maarufu ambazo, mtuhumiwa hutakiwa kuripotiwa na sio
kushambuliwa,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Kamishna huyo wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad, alisema
hata mtuhumiwa awe na kosa kubwa kiasi gani, ana haki zake kutokana na
ubinaadamu wake.
‘’Kwa mfano
kuna haki ya kuhojiwa, kusikilizwa, kupewa dhamana, kukata rufaa, kutumikia
chuo cha mafunzo na hata kupata msamaha kwa baadhi ya mazingira,’’alieleza.
Aidha
Kamishna huyo, ameikumbusha jamii kuendelea kuvitumia vituo vya Polisi, kuripoti
matukio mbali mbali, licha ya changamoto ambazo hujitokeza.
Kwa upande
wake, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, amesema hakuna kinga kwa
wanaowashambulia watuhumiwa, kwani kazi ya kutoa hukumu kisheria, ipo kwa
mahakama.
Alieleza
kuwa, jamii inapaswa kuzingatia sheria na kanuni za kijinai, ambazo zimeweka
utaratibu wa kushughulikia kesi zote, hadi kufikia kutolewa uamuzi.
‘’Mifumo ya
sheria imeweka utaratibu nzima wa kushughulikia haki jinai, na ukiangalia
mwanzo hadi mwisho, hakuna eneo ambalo mwananchi ameruhusiwa kujichukulia
sheria mikononi,’’alieleza.
Nae
Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba
‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema elimu wanayoitoa kwa jamii, hatarajii kuona
mwananchi, anajichukulia sheria mikononi.
‘’CHAPO
inaowasaidizi wa sheria katika shehia zote za wilaya ya Chake chake, wamekuwa
wakitoa elimu juu ya utaratibu nzima wa kushughulikia haki jinai, lakini sio
kujichukulia sheria mikononi,’’alifafanua.
Akizungumzia
kuhusu madhara ya kujichukulia sheria mikononi, Mratibu wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora Tazania ofisi ya Pemba, Suleiman Salim, alisema moja ni
kuendeleza visasi.
‘’Jingine ni
kupora mamlaka ya kisheria ya mahakama, ambayo ndio inayopaswa kutoa hukumu kwa
mshitakiwa, lakini sio jamii husika,’’alifafanua.
Alisema
jingine ni kupunguza nguvu kazi kwa wananchi, pamoja na kuiongezea gharama
serikali kwa matibabu, iwapo mtuhumiwa atapata majeraha.
Mwanamke
mmoja ambae muume wake aliuawa na wananchi wenye hasira mwaka 2019 eneo la Wawi
wilaya ya Chake chake, alisema kama serikali haifanyi juhudi za kuwakamata
waliosababisha vifo, utamaduni huo, utakuwa endelevu.
Hassan Juma
Hassan wa Msingini Chake chake, alisema wananchi wamekuwa wakijichukulia sheria
mikononi, kutokana na mifumo ya haki jinai, kuchelewesha utoaji wa hukumu.
‘’Inawezekana
wananchi wamemkamata mtuhumiwa na kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria na
ushahidi kamili, lakini baada ya muda unaskia hana kesi ya kujibu, hapo hasira
huibuka,’’analeza.
Daktari wa
saikolojia ya mwanadamu Ali Yussuf wa Chake chake, alisema moja ya sababu
inayowaskuma wananchi kujichukulia sheria mikononi, ni kukosa imani na vyombo
vya ulinzi na usalama.
‘’Kama
wamempeleka mtuhumiwa mmoja kaachia, na kisha anarejea tena kufanya makosa bila
ya hatia, akili huwashawishi kujichukulia sheria mikononi,’’alifafanua.
Aliyekuwa
Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Safia Saleh
Sultan, alisema elimu ya sheria bado iko chini, kwa jamii ndio maana
wanajichukulia sheria mikononi.
Ripoti ya uhalifu ya Jeshi la
Polisi Tanzania ya mwaka 2020, inaonesha kuwa, wapo wananchi 124 wameshauawa,
kutokana na watu kujichukulia sheria mikononi Zanzibar.
Uchunguzu
umebainika, hao ni wa kipindi cha miaka 10, kati ya mwaka 2011 hadi mwaka 2020,
kwa mikao mitano pekee ya Zanzibar.
Kwa
idadi ya wananchi hao waliouawa, kwa tuhma za kufanya uhalifu, ni sawa na kila
mwaka, wastani wa watu 13 kuuawa visiwani humo katika kipindi hicho.
Watu wao
waliouawa kwa Zanzibar, Mkoa wa mjini Mgharibi Unguja, uliongozwa kwa miaka
yote hiyo, na takwimu hizo haijwahi kushuka.
Imebainika
kuwa, mwaka 2011, Zanzibar kuliripotiwa matukio manne (4), mkoa wa Mjini
mgharibi pekee, uliripoti matukio matatu (3).
Mwaka 2015
ilikusanya matukio manane (8), mkoa wa Mjini mgharibi ukaripoti matukio matatu,
ingawa mwaka 2016 kati ya matukio 21, mkoa huo uliripoti matukio 16.
Hali
hiyo, ipanda juu zaidi mwaka 2017, kwa wananchi 26 kuuawa, ambapo kati yao, 18
walikuwa wa mkoa wa Mjini magharibi.
Kwa
mwaka huo mikoa mingine ya iliyoripoti matukio mengi zaidi, ni mkoa wa kusini
Unguja, matano (5), kusini Pemba matatu (3), na mikoa mengine kukiwa hakuna
vifo vilivyoripotiwa.
Mwaka
2019, ulibeba matukio 17, ambapo matukio 12 yalikuwa mkoa wa Mjini magharibi
pekee, kusini Pemba matukio mawili (2) na mikoa mengine kukiwa na idadi sawa na
tukio moja moja.
Hata
mwaka 2020, mkoa wa Mjini magharibi, ulikusanya matukio 10, ya mauwaji kwa
wananchi kujichukulia sheria mikononi, kati ya matukio yote 15 yaliyoripotiwa.
Mwisho
Comments
Post a Comment