NA ZUHURA
JUMA, PEMBA@@@@
Serikali imetakiwa kuweka mazingira mazuri ili
kuwalinda wasichana wadogo dhidi ya vitendo vya ubakaji kisiwani Pemba.
Kati ya hayo, ikiwemo kutoa elimu ya
kutosha, kuwafanya wasichana wajue haki zao, kuweka ulinzi dhidi ya wanaotaka
kutoa taarifa na msaada wa kisaikolojia kwa walioathirika, imeelezwa.
Mapendekezo haya yamekuja kufuatia
ripoti ya uchunguzi ya gazeti hili, iliyoonyesha kwamba kesi nyingi zinazohusu
kubakwa kwa mabinti wenye umri chini ya miaka 18 zinaishia njiani kwa wahusika
kutochukuliwa hatua yoyote.
Pamoja na hoja hizo zinazosemwa katika jamii, bado mtoto chini
ya miaka 18 ni mtoto kutokana na sheria ya Zanzibar nambari 6 ya mwaka 2011 ilivyoeleza
Jambo la kwanza ambalo wadau waliozungumza ni hili
wamesisitiza ni umuhimu wa Serikali kuendelea kusisitiza kwamba kwa mujibu wa Sheria
za nchi, mtoto wa kike maana yake ni mtu mwanamke mwenye umri wa chini ya miaka
18.
Mkaazi wa Shehia ya Kiungoni, Ali Haji Omar alimwambia
mwandishi kwamba la muhimu ni kila mtu kujua kwamba mtu mwenye umri wa chini ya
miaka 18 awe mwanamke au mwanamume, ni mtoto na elimu zaidi ya kujitambua na
kujithamini inatakiwa.
Namna ya kuwasaidia watoto
Omar aliliambia gazeti hili kwamba ili kuhakikisha watoto wanaoathiriwa
na vitendo hivyo wanatoa ushahidi mahakamani, wanahitaji wapewe elimu zaidi kwa
sababu kwa mujibu wa Sheria za Zanzibar, mwenye umri chini ya miaka 18 bado ni
mtoto.
‘’Wapewe elimu ya umuhimu wa kutoa ushahidi na athari zinazoweza
kujitokeza iwapo watakataa kutoa ushahidi katika Mahakama, kwa sababu Hakimu na
Mwendesha Mashitaka hawakuwepo kwenye eneo la tukio’’, anasema mwananchi huyo.
Kwa upande wake, Saade Hamad Khlfan, mkaazi wa Shehia ya Piki
yeye amependekeza kuwepo utaratibu wa kushughulika na kesi hizo mara tu baada
ya muathirika kuwa tayari kutoa ushahidi, kwani kuchelewa ndiko huwafanya watoto
na familia kubadili mawazo.
‘’Kwa mfano unasikia leo Hakimu hayupo, kesho Mwendesha Mashitaka
ana kikao, kwa hiyo katika haya tubadilike na kubwa zaidi ni kuondoa dharura
ikiwa mashahidi wapo na hasa shahidi nambari moja ambae ni mtoto mwenyewe’’,
anaeleza.
Mwananchi kutoka Shehia ya Piki, Fatma Kassim Issa, anaeleza kuwa
Mahakama zingetengeneza mazingira mazuri hasa ya ushahidi na si kuwapeleka
mashahidi nusunusu, kwani hapo ndiyo huwa mwanzo wa watoto hao kugeuka.
‘’Kwa sababu unamkuta leo mtoto amesema vizuri lakini siku
zikipita anaanza kujifikiria kusema kuwa hajanifanyia huyu, kanifanyia mtu
mwengine na wala siwezi kumsema, lakini ikiwa Mahakama zina mazingira mazuri
upelelezi unapokamilika tu hakuna haja ya kuzikosesha haki kwa mtoto’’,
anasema.
Anasema kuwa, walio wengi wamekuwa wakigeuka baada ya kukaa siku
nyingi bila ushahidi kusikilizwa na ndio wengine huchukua fedha kutokana na
kukaa siku nyingi, hivyo wanakosa haki zao.
Rashid Ali Khamis mkaazi wa Mzambarau Takao, anasema jambo
lingine linaloweza kufanyika ni kupunguza umri wa mtoto anayelindwa kisheria,
kwani inawezekana pia kwamba wale ambao umri wao umevuka miaka 15 huwa
wanajielewa na kujua wanachofanya.
Kwa upande wake, mkaazi wa Shehia ya Minungwini Maryam Faki
Ali anapendekeza kuwepo kwa nyumba maalumu ya kuwatunza mabinti wadogo
wanaotakiwa kutoa ushahidi mahakamani, ili wahifadhiwe na wasishawishiwe
kuharibu ushahidi.
‘’Wengi wao wanashawishiwa, kutishwa au kuahidiwa ndoa na ndio
maana wanakuwa wanabadilisha ushahidi au hawafiki mahakamani, lakini
wakihifadhiwa sehemu maalumu itakuwa ni vigumu kubadilika’’, anaeleza.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anaeleza kuwa,
waathirika wa vitendo vya ubakaji wanahitaji kupewa msaada wa kisaikolojia na
kuelezwa kuwa matendo hayo waliyofanyiwa yanawaathiri kisaikolijia na wabakaji
wakiachwa wataendelea kuwabaka watu wengine.
‘’Pia tuwaeleze athari zinazoweza kuwapata wao wenyewe iwapo
watakataa kutoa ushahidi na vipi watakaposhindwa kutoa ushahidi itachangia
watoto wengine kuendelea kudhalilishwa’’, anaeleza.
Anaeleza kuwa, watoto wenye umri huo bado hawajajielewa na
ndio maana wakifikishwa mahakamani wanawalinda watuhumiwa kwa kusema kuwa ni
wapenzi wao, hivyo wanahitaji elimu ya kujitambua ili wajijue wao ni nani.
‘’Na ndio maana wanashindwa kutoa ushahidi mahakamani kwa
sababu watuhumia wanawaambia kuwa asipotoa ushahidi ataenda kumuoa’’,
anafafanua Mratibu huyo.
Mwananchi wa shehia ya Mtambwe Kaskazini, Husna Salum Bakar,
anasema elimu itasaidia kuwajenga watoto hao waweze kuwa na misimamo thabiti ya
kuweza kutoa ushahidi.
Akizungumza na mwandishi, Hakimu wa Mahakama Maalumu ya Kushughulikia
Kesi za Udhalilishaji Mkoa iliyopo Wete, Ali Abdulrahman Ali, anasema watoto
hao wanatakiwa kuwa na elimu hasa ya kujua athari zitakazotokea endapo atajiingiza
katika mapenzi ya mapema.
‘’Zipo athari nyingi zinaweza kuwatokezea watoto hao iwapo watajiingiza
katika ngono za mapema, kwa hivyo wapewe elimu ya kutosha na waambiwe kuwa
unapofanya hivi kuna moja, mbili, tatu litakutokea hii itawasaidia kuachana na
masuala hayo’’, anaeleza.
Anataja kesi za kubaka ambazo zimefikishwa mahakamani kuanzia
mwaka 2020 hadi 2021 ni 49 huku za watoto kati ya umri wa miaka 15-17 zikiwa
19, ambapo nne washtakiwa wamefungwa, mbili wametozwa faini na kesi 13 zimeondolewa
(kufungwa).
Hakimu huyo anafafanua kuwa, mwaka 2021 kesi za kubaka
zilizofikishwa mahakamani ni 25, miongoni mwa hizo kesi za watoto wenye miaka
15-17 ni 16, ambapo kesi 11 zimeondolewa, kesi tatu washtakiwa wamefungwa na
kesi mbili washtakiwa wametozwa faini kutokana na kuwa wapo chini ya miaka 18.
“Kesi za ubakaji zilizofikishwa mahakamani mwaka 2020 ni tisa (9),
kati ya hizo watoto wenye miaka 15-17 ni kesi tatu, ingawa moja tu ndio
iliyopata hatia na mbili ziliondoshwa”, anafafanua.
Mratibu kutoka Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Wilaya ya Wete, Asya
Ibrahim, anaeleza kuwa wanawasaidia watoto hao kwa kuwapa ushauri nasaha na
kuwaeleza ili wazungumze ukweli, jambo hilo litasaidia kuondosha maasi ikiwa ni
pamoja na huo udhalilishaji.
‘’Kwa sababu yule ambaye atakwenda kumtolea ushahidi (mtuhumiwa)
atahukumiwa na jamii itajifunza kwamba kufanya hivyo ni kosa na utakapokwenda
mahakamani utachukuliwa hatua za kisheria’’, anasema.
Rashid Hassan Mshamata ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana
na Udhalilishaji anaeleza kuwa, msaada mkubwa kwa watoto hao ni kuongezwa
kupewa elimu ya kujua namna gani watafanya iwapo limetokea tukio hilo.
‘’Kwa sababu ikiwa hawakupewa elimu maisha yao ya baadaye, yote
yataharibika na watashindwa kutimiza malengo yao waliyojiwekea,’’ anafahamisha
Mshamata.
Khadija Mohamed mkaazi wa Mzambarau Takao anasema, watoto wapewe
mafunzo mbali mbali ili wajue nini wafanye na kitu gani hawapaswi kufanya
kutokana na umri wao, hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha vitendo hivyo
katika jamii.
Kwa mujibu wa takwimu za jeshi la Polisi Wilaya Wete za mwaka 2020
zinaonyesha kesi takribani 85 za udhalilishaji i ziliripotiwa, huku
kesi 30 zikiwa ni kesi za ubakaji zinazohusisha watoto kati ya mika 15-17.
Kati ya hizo kesi 30 zilizoripotiwa, ni kesi nne (4) tu ambazo
zilitolewa hukumu huku 17 zikfutwa katika kituo cha Polisi, kesi saba (7)
zilifutwa mahakamani na kesi mbili (2) zikiwa katika upelelezi.
Wakati mwaka 2021 kesi zilizoripotiwa zilikuwa 44, kesi 28
zikiwa za watoto wenye umri wa miaka 15-17 ambapo ni kesi nne (4) tu
zilizotolewa hukumu kama mwaka 2020, huku kesi 12 zikifutwa Polisi na saba (7)
mahakamani na kesi tano (5) upelelezi wake bado unaendelea.
MWISHO.
Comments
Post a Comment