JUMA MUSSA, PEMBA.
WAUMINI wa dini ya Kiislam wametakiwa kuishi kwa kuendana na malengo ya Qur- an ili kupata amani , maendeleo na salama hapa ulimwenguni na Akhera siku ya malipo.
Afisa Mdhamini Tume ya Mipango Pemba Khamis Issa Mohamed aliyasema hayo Machi 3, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Matar Zahor Massoud Ole Kianga katika ufunguzi wa Ijitimai ya 24 ya Kitaifa inayofanyika Kisiwani Pemba.
Alisema bila kuwepo umoja, maadili mema na mshikamano hakuna maendeleo yatakayopatikana kutokana na umma kuwa na fadhaa jamboambalo linatokana na kusahau maamrisho ya dini yao.
“ Tusifichane ndugu zangu waislamu bila ya nchi kuwa na amani hakuwezi kupatikana maendeleo kwani kila mmoja atakuwa anapigania uhai wake na hatimae hata kufanya Ibada jambo ambalo tumeletewa hapa ulimwenguni tutakuwa muda hatuna hivyo tutakuwa na makosa mbele ya Allah (S.W.T)”, alisema.
Alifahamisha kuwa ili amani na utulivu wa nchi uweze kudumu ni wajibu wa kila mmoja ni kutekeleza maamrisho ya mola wetu na kaucha mambo ya kidunia ambayo yameigubika baadhi ya mataifa na kupelekea amani yao kutetereka.
Awali Mwenyekiti wa Fiiy sabili llahi Markaz Zanzibar Amir Ali Khamis alisema Jumuiya hiyo imekuwa ikishirikiana na Serikali katika kutatua migogoro mbalimbali ya kijamii ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia..
“ Pamoja na kwamba tumekuwa tukikusanyika kila mara katika Ijitimai kama hizi , lakini tumekuwa tukishirikiana na Serikali katika mambo mbali mbali ikiwemo utatuzi wa migogoro”, alieleza.
Aidha Mratibu wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Said Ahmad Mohamed aliitaka jamii kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali kuendeleza uwelewa na umuhimu wa amani na usalama kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
“ Waumini wenzangu tushirikiane na viongozi wetu mbali mbali wa kidini , kiserikali na taasisi mbalimbali za kimataifa katika kuilinda amani ya nchi yetu kwani amani ni neno dogo kulitamka lakini ni kubwa kwa matendo yake na likiondoka ni tabu kurejea kama ilivyokuwa , tuangalieni mataifa ya wenzetu yalivyo sasa hivi”, alisema Sheikh
Said.
Hata hivyo nao baadhi ya washiriki wa Ijitimai hiyo walisema Ijitimai hiyo imekuja wakati muafaka kwani imekuja kuwakomboa na kuwaonesha njia ya kwenda kwenye kheri hasa katika kueleke mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
MWISHO .
Comments
Post a Comment