NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
WANAFUNZI wa skuli za msingi za Madungu
na Michakaini wilaya ya Chake chake, wametakiwa kuacha mara moja
aina yote ya michezo, inayoashiria kukamatana sehemu za siri, ukiwemo unaoitwa ‘cheni
dole’.
Hayo yameleezwa
na Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar
ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, wakati akizungumza na wanafunzi, kwenye kampeni
maalum ya kuongeza uwelewa, kwa wanafunzi wa skuli, madrassa, vyuo vikuu na
klabu za sanaa.
Alisema, ipo
michezo katika skuli na madrassa inayofanywa na wanafunzi wa kike na kiume,
ambayo mingi inaelekeza namna ya kukamatana, maeneo yao ya siri ikiwemo
makalio.
Mratibu huyo
alieleza kuwa, michezo hiyo na mengine husababisha wanafunzi, kufukuzana hadi
kichakani, na kisha kuanza kufanyiana vitendo viovu.
‘’Kuanzia
leo michezo kama cheni dole, cheni saluti, nichum kwanza na nishike, iwe
marufuku kwa watoto wote, kwani inaashiria udhalilishaji,’’alifafanua.
Katika hatua
nyingine Mratibu huyo wa TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said,
aliwataka wanafunzi hao kuendelea kutoa taarifa, pindi wakifanyiwa vitendo vya
udhalilishaji.
Kwa upande
wake Afisa Ustawi na Hifadhi ya mtoto wilaya ya Chake chake Rashid Said Nassor,
alisema moja ya madhara makubwa ya udhalilishaji, ni kwa mwanafunzi wa
kukatisha masomo.
‘’Lakini
hata suala la kupata madhara ya kiakili, kimwili, kutengwa, kupata magonjwa yanaweza
kujitokeza kwa aliyefanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji,’’alifafanua.
Katika hatua
nyingine Afisa huyo, amewakumbusha watoto hao kutokubali kupokea zawadi, mfano
wa fedha au chakula kwa mtu wasiyemjua.
‘’Hata kwa
unamjua, uwe makini sana, na ukihisi anazisogelea sehemu zako za siri, toa
taarifa za haraka, iwe kwa mwalimu, baba, kaka, mama, jirani au mwanafunzi
mwenzako,’’alifafanua.
Hata hivyo,
aliwasisitiza wanafunzi kutokubali kuoneshana au kuoneshwa picha za ngono,
kwani huo ndio mwanzo, wa wao kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Akizungumza kwenye
mikutano hiyo, wakili wa watoto kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’
tawi la Pemba Siti Habibu Mohamed, alisema adhabu ya mtu aliyebaka ni kuanzia
miaka 30 hadi maisha, chuo mafunzo.
Aidha aliwataka
wanafunzi hao, kwa sasa washughulikie masomo yao, wasijihusishe na vitendo vya
yoyote, ambavyo kwa njia moja ama nyingine, vinazuia mtiririko wa masomo yao.
‘’Nyinyi kwa
sasa jukumu lenu ni kuhudhuria madarasaa na skuli na kusoma kwa bidii, ili
mujijengee msingi madhubuti wa maisha yenu, hapo baadae,’’alieleza.
Awali Msaidizi
mwalimu Mkuu wa skuli ya Madungu Baya Is-mail Khamis, aliwataka wawezeshaji
hao, kujenga utamaduni wa kila baada ya muda, kufika skulini hapo.
Alisema,
elimu hiyo haikuwasaidia wanafunzi pekee, bali hata waalimu, imewakumbusha
mambo kadhaa likiwemo umuhimu wa kutoa ushahidi.
Nae Mwalimu Mkuu wa skuli ya Michakaini Said Ali Ahmed, amesema vitendo vya udhalilishaji vipo ndani ya jamii, hivyo elimu isipotolewa, hali inaweza kuzidi.
Ofisa kutoka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wilaya ya Chake chake Khamis Mohamed Yahya, ameipongeza TAMWA-Zanzibar kwa hatua yao ya kuwafuata wanafunzi hao kuwapa elimu.
TAMWA-Zanzibar
kwa sasa inaendelea na kampeni ya kusaidia wadau katika mapamabano ya udhalilishaji
wa wanawake na watoto kupitia skulini, madrassa, vyuo vikuu na vikundi vya sanaa
na kisha kuchukua hatua, kupitia mradi tumia jukwaa la habari kumaliza udhalilishaji.
Mwisho
Comments
Post a Comment