NA HAJI NASSOR, PEMBA::
WANAFUNZI wa skuli Pondeani na Michakaini wilaya ya Chake chake, wameanza kufanyiwa vipimo vya aina tofauti, ikiwa ni pamoja na
usikivu, zoezi linaloendeshwa na Milele Zanzibar Foundation kwa kushirikiana na
Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, kupitia Ofisi ya watu wenye ulemavu wilayani humo.
Akizungumza kwenye
zoezi hilo skuli ya Michakaini msingi wilaya ya Chake chake, Afisa miradi Idara
ya afya kutoka taasisi hiyo Mohamed Abdalla Rashid, alisema Milele imekuwa
ikijali mno afya za jamii.
Alisema, lengo
la zeozi hilo ni kuangalia afya za watoto walioko skulini, ili kuwagundua
mapema, hasa katika eneo la uoni, usikivu na kisha kupatiwa matibabu.
Alieleza kuwa,
katika zoezi hilo limewashirikisha wataalamu wa koo, maskio na macho, kwa lengo
la kuwafanyia uchunguuzi kwa kina na kisha kufikishwa hospitali kwa huduma
zaidi.
Afisa huyo
alieleza kuwa, zoezi hilo linaumuhimu mkubwa kwa mustkbali wa ukuaji wa watoto,
kwani wakati mwengine wanaweza kugundua tatizo mapema, na kulitibu.
‘’Milele kwa
kushirikiana na Idara ya watu wenye ulemavu, tuliona tuwafanyie wanafunzi hili,
ili kuwapa uhakika wa kushirikishwa kikamilifu wakati wa masomo yao darasani,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, alisema afya ni jambo la msingi na muhimu kwa mtoto anayesoma, na
kama akiachiwa bila ya kufanyiwa uchunguuzi, unaweza kukaathiri maendeleo yake.
Hata hivyo
amewakumbusha wazazi na walezi, kutopuuza mazoezi kama hayo, kwani huwasaidia
watoto wao katika malezi na makuzi.
Mratibu wa
Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar ofisi ya Pemba Mashavu Juma
Mabrouk, ameishukuru tasisi ya Milele Zanzibar Foundation, kwa kubali
kufanikisha zoezi hilo.
Alisema Milele
inatekeleza kwa vitendo, juu ya haki za makundi mbali mbali wakiwemo watu wenye
ulemavu, kwani nao wana haki sawa na wengine.
Alieleza kuwa,
zoezi hilo linaweza kwagundua mapema watoto wenye mahitaji maalum, na kama
watapata ushauri na matibabu husika, wanaweza kuondokana na ulemavu
unaozuilika.
‘’Kwa hakika
zoezi hili linaumuhimu mkubwa, maana kwanza unaweza kumjua mapema mtoto
anakabiliwa na changamoto gani, katika malezi na makuzi yake,’’alieleza.
Hata hivyo
aliiomba Milele Zanzibar Foundation kulifanya endelevu zoezi hilo, na hasa
kuelekeza nguvu katika maeneo ya nje ya miji.
Wazazi Hassan
Khamis Ali na Mwamke Mtumwa Omar wa Machomane Chake chake, walisema zoezi hilo
limesaidia kuwagunuda watoto wao, aina ya changtamoto walionayo kiafya.
Mzazi Tamima
Mohamed Rajab, alisema amegundua kuwa mtoto wake anakabiliwa na changamoto ya
uoni hafifu, baada ya zoezi hilo kukamilika.
‘’Kama
ningekaa naye nyumbani nisingejua kuwa, mtoto wangu anakabiliwa na tatizo la macho
ya uasho, lakini baada ya zoezi madaktari wameniambia na kupata dawa bila ya
malipo,’’alieleza.
Mtaalamu
kutoka kitengo cha macho hospitali ya Chake chake Dk. Shadya Mohamed Salum,
amesema baada ya zoezi hilo, wamegundua kuwa wapo wanafunzi wanakabiliwa na
changamoto ya uoni, bila yao wenyewe kujijua.
‘’Kwenye
tatizo hilo, wapo wasioona mbali, wengine karibu na wengine wanahitajia
matibabu ya haraka, kabla ya kupata athari zaidi,’’alieleza.
Mapema mwalimu
wa upimaji wa usikivu kisiwani Pemba Omar Massoud Saleh, alisema wanafunzi
wengi wamegundulika kuwa na nta ‘wax’
na wengine kutokwa na taka masikioni mwao.
Alieleza kuwa,
kuwa upande wa taka, husababishwa na mafua ambayo hayatoki kwenye pua, na kisha
hukaa na kwenda kwenye mishipa ya sikio.
‘’Kwa
kawaida mafua hutokea kwa njia ya mirija ya pua, lakini haya baada ya kukosa
njia, hukaa kwenye miraja ya sikio na kisha kugeuka taka, baada ya kupevuka,’’alifafanua.
Alieleza kuwa,
masikio yote ya binadamu kwa kwaida huzalisha nta ‘wax’ na kisha kujisafisha wenyewe kwa kutoa maji maji mithili ya
jasho na kisha kuganda.
‘Nta ‘wax’ ndio kinga na sikio na kama ataingia mdudu mdogo, anaweza kuganda na akijaribu kula, hupata uchungu ambao ndio sumu husika,’’alieleza.
Wanafunzi 560 wa skuli za msingi za Michakaini A, B na Pondenia wilaya ya Chake chake, wanaosoma darasa la kwanza, wamefikiwa na wataalamu wa macho, miwani, usikivu na saikolojia, ili kuwafanyia uchunguuzi wa awali ikiwa wanakabiliwa na changamoto za kiafya.
Milele
Zanzibar Foundation inashughulika zaidi na uungaji mkono wa maono ya serikali kuu, katika
maeneo ya afya, elimu na maisha ya jamii kwa ujumla hasa huduma za kibinadamu.
Mwisho
Comments
Post a Comment