IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAHASIBU wametakiwa kuhakikisha wanafuatilia na kutunza vielelezo vya matumizi ya fedha za serikali pamoja na fedha za miamala ya kodi, ili wafanye kazi kwa ufanisi na zipatikane kwa wakati.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa Utekelezaji wa Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Kamati za Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali (PAC), Juma Ali Khatib aliwataka wahasibu hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na muhali na badala yake wafuate sheria na kuilinda fani yao.
Alisema kuwa, ili wafanye kazi kwa ufanisi na kuepusha ubabaishaji kuna haja ya kufuatilia na kutunza vielelezo vyote, kwani ni muhimu katika kuweka taarifa sawa za mapato ya Serikali.
‘’Msikubali kuendeshwa, fanyeni kazi kwa kuzingatia fani yenu, ili kujijengea heshima na kuziweka kumbukumbu vizuri, ili zikihitajika katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali zipatikane kwa wakati’’, alisema Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Mihayo Juma Nhunga alisema kuwa, wanapofanya zuio la kodi wanatakiwa wachukue risiti, ili wanapofika wakaguzi (CAG) zipatikane kwa wakati.
‘’Tusisubiri mpaka CAG wanakuja ndio tunaenda kutafuta risiti, tudai risiti mapema na tuzihifadhi, ili zitakapohitajika ziwepo’’, alieleza.
Nae Msimamizi wa Ukaguzi kutoka CAG Mohamed Suleiman Amour alisema, taasisi za Serikali zinatakiwa ziwe mfano wa kuigwa katika ukusanyaji wa mapato, hivyo ushirikiano unahitajika kuhakikisha huduma zote zinaenda sawa.
Aidha Msimamizi huyo aliwataka viongozi wa taasisi kulinda maslahi ya wafanyakazi wa chini, ili kuepuka malalamiko kwani wanajitahidi kuchapa kazi vizuri.
‘’Wafanyakazi wapewe stahiki zao kwa wakati, kwa sababu kuna baadhi ya taasisi mfanyakazi amefiwa tangu mwaka 2020 lakini hajapewa stahiki zao, tujitahidi jamani’’, alifahamisha.
Akiwasilisha taarifa Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau alisema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara ilitengewa shilingi 413,244,500 na taasisi zake, ambapo hadi kufikia Juni 2021 ilipata shilingi 143,507,00 sawa na asilimia 35 ya bajeti ya mwaka.
Alisema kuwa, upatikanaji wa fedha hizo ni mdogo sana ukilinganisha mahitaji yao, ingawa waliweza kufanikisha majukumu ya Serikali kwa kiasi, ambapo kupitia ukaguzi uliofanywa na CAG uligundua baadhi ya kasoro ambazo Wizara imejitahidi kuzitolea ufafanuazi kulingana na uhalisia uliopo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment