NA
HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAWAKE
wenye dhamira ya kugombea uongozi wa nafasi mbali mbali katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025, wameshauriwa kuanza sasa kutengeneza mazingira, ikiwa ni pamoja na
kufanyakazi kwa karibu na jamii husika.
Kauli hiyo imetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha taifa
cha Zanzibar ‘SUZA’ Salim Ali ofisi ya Chama cha waandishi wa habari wanawake
Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba, kwenye mafunzo ya siku tatu ya
kuwajengea uwezo, wanawake wenye dhamira ya kugombea.
Alisema, maandalizi ya kuelekea kugombea, hutakiwa kuanza
mapema, ili kujua mipango, mikakati, njia za kupita, namna ya kuwafikia wapiga
kura na wasaidizi wake.
Alieleza kuwa, haiwezekani mwanamke anaetaka kugombea kwa
nafasi yoyote, ile kujiacha na kutojishirikisha vyema ndani ya chama chake, na
kugonjea miezi miwili, kabla ya uchaguzi mkuu ndio ajitokeze.
‘’Maandalizi ya kuingia kwenye uchaguzi wa kiushindani,
hutakiwa kuanza mikakati ya kimnya kimnya mapema, ikiwa ni pamoja na kutambua
udhaifu wa wagombea wengine,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mhadhiri huyo kutoka SUZA, alisema
suala la kujua ilani ya chama husika, sheria na kanuni za nchi japo kwa kiwango
kidogo ni wajibu, ili iwe rahisi kuelezea mikakati husika.
Hata hivyo alisema rushwa na ngono au pesa ndio jambo moja
wapo la kulikwepa kwa mgombea mwanamke, kwani humshushia heshima yake, kuanzia
kwenye chama na jamii kwa ujumla.
Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa TAMWA-Pemba Fat-hya
Mussa Said, alisema wakati umefika sasa kwa wanawake, kufanya uamuzi wa kuingua
majimbo kuafuta uongozi.
Aidha Mratibu huyo wa TAMWA- alisema, hakuna jimbo ambalo
linahati miliki kwa wanaume, bali kila jimbo la uchaguzi ni halali kwa makundi
yote.
‘’Yapo maneno yanasemwa kuwa, jimbo fulani ni jimbo dume,
kwamba kwa tafsiri ya juu juu, mwanamke ni marufuku, sasa dhana hii ndio
mnatayarishwa ili mkaiondowe,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Mratibu huyo, alisema majungu,
fitna, kutiliana maneno na kufanya mambo kinyume na sheria, sio njia mwafaka ya
kutafupta uongozi.
Mkurugenzi wa PEGAO, Hafid Abdi Said, aliwataka waweka
dhamira hao, wasisite kutoa mifano kwa wanawake wenzao waliofanikiwa, kwenye
nafasi mbali mbali za uongozi.
Alieleza kuwa, kufanya hivyo kutawavuta wengine kuona
wanawake wanaweza wanapopata nafasi mbali mbali za uongozi.
‘’Wapo wanawake waliofanikiwa vyema kwenye nafasi za
uongozi, sasa hawa tuwachukuweni kama kigezo chetu, ili tunapokutana na wapiga
kura, wasione wanawake hawawezi,’’alifafanua.
Mapema Mratibu wa mradi huo wa SWIL kutoka TAMWA-Zanzibar Maryam Ame, amesema wanawake kama watajipanga vizuri, wanaweza kuibuka na ushindi katika kila chaguzi.
Alisema, wanawake ndio wengi kuanzia chamani, kwenye kampeni na hata siku ya kupiga kura, hivyo atasimama mwanamke mwenye sifa na kujitangaaza vizuri, anaweza kushika uongozi.
Baadhi ya washiriki hao, walisema wamekuwa wakishiriki
kwenye chaguzi mbali mbali, ingawa changamoto kubwa ni ndani ya vyama vyao
hawajaaminiwa.
Maryam Mussa Sharifu, Zainabu Mussa Bakari, Nadhira
Suleiman Said pamoja na Asha Mbarouk Matano, walisema mafunzo hayo,
yamewasaidia kuona mbali zaidi.
Mradi wa Kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi, siasa
na demokrasia 'SWIL' ambao ulizinduliwa mwaka 2020, ukitarajiwa kumalizika
mwaka 2023, unatekelezwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar, Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira
Pemba ‘PEGAO’ na Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA.
mwisho
Comments
Post a Comment