NA
HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MAMLAKA
ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar kisiwani Pemba, imewataka
wanawake wanaogombea nafasi mbali mbali za uongozi, wasisite kuwaripoti
wanaowanyemelea kwa rushwa ya ngono.
Afisa kutoka ZAECA Kassim Yussuf
Ali, aliyasema hayo Machi leo 29, 2023 kwenye mafunzo ya siku tatu, ya
kuwajengea uwezo, wanawake wenye dhamira ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema, kama wanaona suala
la rushwa ya ngono kwao limekuwa changamoto kuelekea katika kila chaguzi,
wahakikishe wanaandaa mazingira ya kuwaripoti wanaotaka kuwachafua.
Alieleza kuwa, ZAECA
imeanzishwa kisheria kwa kushughulikia changamoto kadhaa ikiwemo viongozi
wanaotumia madaraka na uwezo wao vibaya.
Alifafanua kuwa, ZAECA
imekuwa ikishughulikia migogoro ya ina hiyo, inayowakumbuka watu wa makundi mbali
mbali, hivyo na wao wasisite kuwafikisha wale wanaowakwaza, katika kutafuta
haki ya uongozi.
‘’Wanawake mmekuwa woga
kuwaripotia wale wanaowakwaza katika kutafuta uongozi, na mkiendelea kukaa
kimnya, haki yenu ya kuwa viongozi itakaliwa,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Afisa
huyo, alisema kwa uchaguzi mkuu uliomalizika, wapo wanawake wagombea kadhaa
waliofikishwa ZAECA, wakitumia rushwa katika kampeni zao.
Akiwasilisha sheria ya Tume
ya Uchaguzi pamoja na sera ya jinsia, Afisa Uchaguzi Msaidizi wilaya ya Chake
chake Shikha Kitwana Sururu, alisema jambo la kuzingatia kwa wagombea wanawake,
ni ujazaji wa fomu.
Aidha alieleza kuwa, kasoro
nyingine ni vyama kuwateua wanaume wengi zaidi kuliko wanawake, jambo ambalo Tume
haiwezi kuliingilia.
‘’Ni kweli wanawake
hawaonekani kwa wingi majimboni, lakini hili lina pande mbili moja, inaonekana
hawagombei kwa wingi, lakini pili ni vyama kutowapa kipaumbele,’’alieleza.
Hata hivyo alisema, jambo
jingine linalowaangusha wanawake, ni kutokuwa makini katika ujazaji wa fomu,
kutumia majina zaidi ya mawili na kutozikagua fomu kabla ya kuziwasilisha Tume.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
PEGAO, Hafid Abdi Said, aliwataka waweka dhamira hao, wasisite kutoa mifano kwa
wanawake wenzao waliofanikiwa, kwenye nafasi mbali mbali za uongozi.
Alieleza kuwa, kufanya hivyo
kutawavuta wengine kuona wanawake wanaweza wanapopata nafasi kadhaa iwe za
kisiasa au maeneo mengine.
‘’Wapo wanawake waliofanikiwa
vyema kwenye nafasi za uongozi, sasa hawa tuwachukuweni kama kigezo chetu, ili
tunapokutana na wapiga kura, wasione wanawake hawawezi,’’alifafanua.
Wakichangia kwenye mafunzo hayo,
akiwemo Maryam Saleh Juma kutoka Chama cha ukombozi wa Umma, alisema bado
anaona kunachangamoto ndani ya Tume za uchaguzi.
Nae Amina Omar Msellem kutoka
CCM, alieleza kuwa, wakati umefika kwa Tume za uchaguzi, kutoa elimu ya mpiga
kura, hata kabla ya uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake Iptisam Hamad
Abdalla kutoka CHADEMA, Maryam Mussa Shaif kutoka ACT-Wazalendo na Asha Mbarouk
Matano kutoka CUF, walisema mafunzo hayo yamewasaidia kujua kasoro.
Mapema Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ Salim Ali, alisema moja ya jambo linalowaangusha
wagombe wanawake, ni kukosa kuchagua timu nzuri ya kampeni.
‘’Inawezekana huangalii sifa
za meneje wako kampeni, pengine ni mtu tamaa, anaependa fedha, wasiotosheka na
hawajui ajenda yako, hawa wanaweza kukuangusha,’’ alieleza.
Akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, Dk.
Mzuri Issa Ali, aliwataka watia nia hao kuzisoma sera, sheria na ilani za vyama
vyao.
Alieleza kuwa, haiwezekani
mgombea hajui ilani ya chama chake, hajui mipaka ya jimbo lake, na hajui
wananchi wanataka nini kama akipata nafasi hiyo.
‘’Lakini tusikubali kupewa
taarifa za kusikia sikia, bali sisi wagombeA ndio tuwe watafutaji, wahariri na
wasambaazaji wa taarifa za vyama vyetu na majimboni,’’alieleza.
Wakati huo huo, Mratibu wa mradi wa SWIL kutoka TAMWA-Zanzibar
Maryam Ame, amesema wanawake wana haki ya kuongoza na kushika nafasi mbali
mbali, katika maeneo kadhaa.
‘’Ndio maana, TAMWA kwa kushirikiana na PEGAO na ZAFELA ikaandaa
mradi huu, lengo ni kuwawezesha ili muweze kudai haki zenu za kisiasa,
demokrasia na uongozi,’’alieleza.
Mradi wa Kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi, siasa
na demokrasia 'SWIL' ambao ulizinduliwa mwaka 2020, ukitarajiwa kumalizika
mwaka 2023, unatekelezwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar, Jumuiya ya
Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba ‘PEGAO’ na Chama cha wanasheria wanawake
Zanzibar ZAFELA.
mwisho
Comments
Post a Comment