NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
AFISA
Mdhamini wizara ya nchi, afisi ya rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Utawala
bora Pemba, Halima Khamis Ali, amesema kampeni ya kitaifa ya Rais ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan ya msaada wa kisheria, inalenga
kutoa ulinzi na upatikanaji haki, kwa wanawake, watoto na wale wa makundi
maalum.
Afisa Mdhamini huyo aliyasema
hayo Machi 28, 2023, ukumbi wa wizara hiyo Gombani Chake chake Pemba, kwenye
mkutano maalum wa kuutambulisha mkakati wa kampeni hiyo, kwa wadau wa haki
jinai wakiwemo wasaidizi wa sheria kisiwani humo.
Alisema, kampeni hiyo iliyopewa
jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutokana na maono yake ya kwa
makundi hayo na mengine, ya upatikanaji wa msaada wa kisheria, kampeni hiyo
inakuja kuondoa changamoto hizo.
Alieleza kuwa, kampeni hiyo
inagusa kila taasisi katika utekelezaji wake, ikiwemo wasaidizi wa sheria,
Jeshi la Polisi, Tume ya haki za bindamu, vyombo vya sheria, Ofisi za ustawi,
wizara husika ya katiba na sheria, vyombo vya sheria pamoja na jamii kwa
ujumla.
‘’Kampeni hii inataka kuona,
zile changamoto za upatikanaji wa msaada wa kisheria na kisha haki kwa
wahusika, zinapatikana na hasa kwa wanawake, watoto na wale wenzetu wa makundi
maalum,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Afisa
Mdhamini huyo alisema eneo jingine katika kampeni hiyo, ni upatikanaji wa
wasaidizi wa sheria wapya 5,000 kutoa elimu ya kisheria, kuzisomesha sera na
sheria za upatikanaji wa msaada wa kisheria.
Aidha alisema, kila mdau kama
ataitekeleza ipasavyo kampeni hiyo, majibu ya maono ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan, yatafikiwa.
Kwa upande wake Afisa Sheria
kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Ali Haji Hassan, alisema
ujio wa kampeni hiyo, ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati, wa utoaji wa
msaada wa kisheria Tanzania.
Alieleza kuwa, kampeni ambayo
ni kwa ajili ya Tanzania bara na Zanzibar, imekuja ili kuimarisha upatikanaji
wa msaada wa kisheria, kwa wananchi hasa wasiokuwa na uwezo.
‘’Tunaelewa kuwa zipo sheria
kama ile ya Msaada wa Kisheria Tanzania
bara, nambari 1 ya Mwaka 2017, Kanuni zake za mwaka 2018 na sheria nambari 13
ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019 kwa upande wa Zanzibar,
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ile ya Zanzibar ya
mwaka 1984, ambazo ndio msingi mkuu wa utoaji wa msaada wa
kisheria,’’alieleza.
Akiwasilisha mpango wa mkakati
wa kampeni hiyo, Afisa Sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria
Zanzibar Yussfa Abdalla Said, alisema kila mmoja kwa nafasi yake ni mtekelezaji
wa kampeni hiyo.
Alifahamisha kuwa, utekelezaji
wa kampeni hiyo unatarajia kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa
jamii, hususan haki za wanawake na watoto.
Alieleza kuwa jengine ni kuimarisha
huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili
wa kijinsia pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa huduma za
kisheria.
‘’Kuongeza uelewa kwa
wananchi kuhusu elimu ya sheria kwa umma, masuala ya haki na wajibu na misingi
ya utawala bora, na kuwa na huduma endelevu za msaada wa kisheria katika ngazi
zote za kijamii,’’alifafanua Afisa huyo.
Wakichangia, baada ya
uwasilishwaji wa kampeni hiyo, washiriki akiwemo, Mkurugenzi wa Jumuiya ya
Wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani Nassor Hakim Haji, alisema kampeni hiyo,
inaweza kufungua ufahamu kwa Jeshi la Polisi.
‘’Hadi leo bado baadhi ya
vituo vya Jeshi la Polisi, wanawazuia watuhumiwa zaidi ya muda wa kisheria,
inakuwa kila siku uende kuuliza sababu hizo, sasa kampeni hii
itawazindua,’’alieleza.
Nae mjumbe kutoka Jumuiya ya
Maimamu Zanzibar ‘JUMAZA’ Nassor Abdalla Mauli, alisema kampeni hiyo ni nzuri,
ikiwa jamii na wadau, wataweka kando siasa zao.
Msadizi wa sheria Jimbo la
Chake chake Mashavu Juma Mabrouk na Mratibu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora Pemba, Suleiman Salim walisema kazi iliyobakia ni wananchi, kuelimishwa
juu ya mpango huo.
Wakati huo huo Afisa sheria
wa Idara hiyo Pemba, Bakar Omar Ali, alisema wanasiasa ni sehemu ya utekelezaji
wa mpango huo, ingawa hakuwashirikisha moja kwa moja.
‘’Ni kweli wanasiasa ni
jukwaa muhimu katika kampeni hii, lakini wanaweza kushiriki, ingawa sio moja
kwa moja, kama walivyo wadau wengine,’’alifafanua.
Kampeni hiyo ya kitaifa ya
msaada wa kisheria ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu
Hassan, ilizinduliwa Machi 1, mwaka huu na ikitarajiwa kumalizika Machi 2026.
Kampeni ya Huduma
ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inalenga kulinda na kukuza haki ya
upatikanaji haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini.
Kampeni
hii inatarajia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika
mazingira magumu.
Vilevile, itachangia kuimarisha amani na
utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa.
Utekelezaji
wa kampeni hii, unatarajia kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa
jamii hususan haki za wanawake na watoto.
Aidha kampeni
hii inatarajiwa kuimarisha huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa
waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia.
Jengine
ni kuwa, maono ya mabadiliko ya huduma ya
msaada wa kisheria umetokana na azma ya Dk. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania
ya kuimarisha mfumo wa kutatua changamoto
zinazowakumba wananchi bila kusubiria wananchi kuwasilisha changamoto zao
wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa.
Ambapo
kampeni hiyo ya msaada wa kisheria itaongozwa na kauli mbiu isemayo Msaada
wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo”
Mwisho
Taarifa imetulia hongera sana mr Haji
ReplyDelete