WATUMISHI WA UMMA: 'MUSIANZISHE MIJDALA YA KUKEBEHI, KUDHARAU MWELEKEO WA SERIKALI' : MDHAMINI THABITI
NA HAJI NASSOR, PEMBA:
OFISA Mdhamini Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa,
Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Thabit Othman Abdalla, amewataka
watumishi wa umma kisiwani Pemba, kutoungana na watu wengine, katika kukebehi
na kudharau mipangano, sera na mikakati ya serikali, kwani kufanya hivyo ni ukiukwaji
wa maadili ya kazi.
Alisema, kila mtumishi wa umma
anapofanyakazi katika kitengo na idara yoyote ile, ajue kuwa anamwakilishi
kiongozi wa nchi, hivyo lazima asikubali kuwa sehemu ya kuongoza mijadala ya
kukibehi mwelekeo wa serikali.
Ofisa Mdhamini huyo aliyasema
hayo Januari 15, 2023, ukumbi wa mikutano Baraza la mji wa Chake chake, wakati akiyafunga
mafunzo ya siku tatu, kama sehemu ya uthibitishwaji wa kazi, kwa watumishi
wapya wa umma, yalioendeshwa na Chuo cha Utawala wa Umma ‘IPA’.
Alisema, wapo baadhi ya watumishi
wa umma kwa kule kutokujua nafasi zao, wamekuwa wakiungana au wakati mwengine
kuanzisha mijadala ya kudhoofisha mikakati ya serikali.
Alieleza kuwa, kiutumishi hilo ni
kosa, kwani kuajiriwa kwake katika kitengo anachofanyakazi, anamwakilishi
kiongozi wa nchi, kama muajiri mkuu.
‘’Wapo watumishi wengine kwa
mfano, wanakebi suala la kupanda vyakula na sera ya uchumi wa buluu, au kusema
serikali haijafanya lolote, haya na mengine yanayofanana na hayo, hayafai kwa
mutumishi umma,’’alisema.
Kati hatua nyingine Ofisa
Mdhamini huyo, amewataka watumishi hao wakawe watumishi bora wenye kutunza sira
za ofisi, matumizi sahihi ya lugha na kufanyakazi, kwa moyo wa kiuzalendo.
Hata hivyo alisema, anaamini kwa
elimu walioyoipata kwa siku hizo tatu, watakuwa mfano wa kuigwa na wenzao kwa
kule kuzifuata kwa vitendo sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Akizungumza kabla ya kufungwa kwa
mafunzo hayo, Mkuu wa ‘IPA’ tawi la Pemba Juma Haji Juma, alisema mafunzo hayo
yamewafungulia milango watumishi hao.
‘’Moja ya faida kubwa ya mafunzo
haya, mtaweza kuthibitishwa kazi, ruhusa za likizo au kwenda masomoni sasa
mtakuwa na haki, na hasa baada ya ofisi zenu kuridhishwa na baadhi ya
mambo,’’alieleza.
Hata hivyo Mkuu huyo wa ‘IPA’
tawi la Pemba, aliwasisitiza watumishi hao, kama wanataka kufika mbali
kiutumishi, waziheshimu na kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo.
‘’Mafunzo haya mjue kuwa, ni
sehemu ya utekelezaji wa sheria na kanuni ya utumishi wa umma ya Zanzibar ya mwaka
2014, hivyo muone thamani yake, katika kazi zenu,’’alieleza.
Mapema akiwasilisha mada ya
sheria ya Utumishi wa Umma Zanzibar ya mwaka 2014, mwanasheria Suleiman Omar
Makame, alisema sheria hiyo ni nzuri, ikiwa itatekelezwa kama ilivyoandikwa.
‘Kwa mfano, sheria imetoa amri ya likizo kila mwaka, na fedha zake kila baada ya miaka mitatu, lakini hata namna ya upandishwaji madaraja na haki ya matibabu kwa mtumishi wa umma,’’alieleza.
Baadhi ya watumishi hao akiwemo
Abass Omar Abass wa wizara ya Habari, alisema sheria ni nzuri, ikiwa muajiri atayatekeza
ipasavyo haki za muajiriwa.
Nae Wahida Kombo Khamis kutoka
Baraza la mji Chake chake, alipendekeza mafunzo hayo, yashirikishe na maafisa
utumishi, ili kupata ufafanuzi zaidi.
Katika mafunzo ya siku tatu, mada
10 zilijadiliwa ikiwa ni Mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar ‘ZSSF’, sheria ya ZAECA,
uzalendo na umuhimu wake kwa taifa, sheria ya Utumishi ya umma na kanuni zake
pamoja na sheria ya Afya na usalama kazini.
Mwisho
Comments
Post a Comment