NA HAJI NASSOR, PEMBA::
MADEREVA wa
vyombo vya moto kisiwani Pemba, wamewataka wanafunzi wa skuli, kutodharau honi
wanazowapigia au mingurumo maalum ya mshine, ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Walisema, wanafunzi waliowengi wamekuwa na tabia ya kudharau
honi au mivumo isiyokuwa na kawaida, wanayoifanya ili wakae pembeni, jambo
ambalo linaweza kuleta madhara.
Wakizungumza na mwandishi wa habari eneo la Ngwachani, ambapo
dereva mmoja aliyekataa kutaja jina lake, alipoteremka kwenye gari,
kuwaeilimisha wanafunzi waliodharau honi aliyowapigia mara tatu.
Alisema, alilazimika kuweka gari pembeni, na kuwapa maneno
makali kundi la wanafunzi, baada ya kuwapigia honi na mivumo mikali ya mashine,
bila ya kujali.
Dereva huyo alieleza kuwa, alikuwa amebeba mzingo akitokea
bandarini Mkoani, na alipofika karibu na njia ya Tangaani, aliwapigia honi
wanafunzi, ili wakae pembeni, ingawa hawakutii.
‘’Mbele yangu kuna gari mbili za abiria zinafukuzana
zikitokezea mjini Chake chake, na upande wangu kuna kundi la wanafunzi kama 15,
niliwapigia honi chaajabu, hakuna hata mmoja aliyegeuka nyuma,’’alisema.
Kwa upande wake dereva Ali Omar Ali wa gari ya Chake
chake-Mkoani, alisema wanafunzi wenye tabia hiyo, hasa ni wa skuli zenye
sekondari na zaidi wale wa kike, ndio ambao wameuwa wakidharau honi.
‘’Wale skuli za msingi ukiwapigia honi au gari ukiibadilisha
mvumo wanakaa pembeni haraka, lakini hawa wakubwa ni wajeuri na wakati mwengine,
inatubidi sisi tuwakwepe wao,’’alieleza.
Kwa upande wake dereva wa gari ya abiria, Hussein Kassim Omar
alisema, kisheria wanafunzi wanapotembea iwe kwenda ama kurudi skuli,
wavielekee vyombo vya moto na siku kuvipa mgongo.
Mwanafunzi mmoja Nassor Haji Ali, alisema kinachojitokeza ni
kutokana na kukosekana kwa miundumbinu rafiki, ya watembea kwa miguu kwenye
barabara Chake chake- Mkoani.
Nae mwanafunzi Aisha Khamis Adam, alisema sio kweli kuwa wao
wamekuwa wakidharau honi, bali wakati mwengine madereva, wanakuwa wanawapigia
karibu yao, pasi na dharura.
‘’Lakini madereva wengine hutupigia honi sisi wanafunzi wa
kike, kama ishara ya kuanza kwa mahusiano ya kimapenzi na mmoja kati yetu, na
hasa wanaemjua,’’alieleza.
Hata mwanafunzi Mwajuma Daudi Mohamed, alisema wamekuwa
wakiziheshimu mno honi na mivumo ya gari, isiyo ya kawaida, ingawa shida ni
madereva kutopunguza mwendo wanapowaona wanafunzi.
‘’Kama madereva wanafukuzana huko wanakotokea, hata wakikuta
kundi la wanafunzi, hawapunguzi mwendo, sasa hili ni tatizo kwao na sio sisi,’’alieleza.
Hivi karibuni Mkuu wa usalama barabarani mkoa wa kusini Pemba kutoka
Jeshi la Polisi, Shawali Abdallah, alisema wameshazimaliza skuli zote za msingi
na sekondari, kuwaelimisha wanafunzi, matumizi sahihi ya barabara.
‘’Tumeshapita skuli zote za mjini na vijijini, kwa zile ambazo
wanafunzi wanapita kwenye barabara kuu, kuwa wanapokwenda ama kurudi gari, wawe
wamezipa uso gari, hii inaweza kuwa rahisi chombo kikipata hitilafu, kukimbia,’’alieleza.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma
Saad Khamis, amewakumbusha madereva, kuendelea kuheshimu sheria za usalama
barabarani.
Katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2020 kikosi cha Usalama barabarani, kilifanikiwa kukamata makosa madogo ya Usalama barabarani 2,152,533 ikilinganishwa na makosa 2,311,538 yaliyokamatwa kwa mwaka 2019.
Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, mkoa wa Mjini Magharibi
uliongoza kwa matukio ya aina hiyo 7,031 na Mikoa iliyokuwa na idadi ndogo ya
matukio ilikuwa ni Kaskazini Pemba 1,512 na Kusini Unguja 2,154.
Matukio ya usalama barabara kwa 2019, yaliripotiwa 104, yakisababisha
majeruhi 290 na mwaka 2020, kulikuwa na watu 124 waliofariki, na majerehi 2092.
Ingawa pia ripoti hiyo ya Jeshi la Polisi Tanzania, ya mwaka
202o, iliripoti ajali 1,133 za piki piki, zilizosababisha vifo 744, sawa na
majeruhi 948 kwa Tanzania yote.
mwisho
Comments
Post a Comment