Na
Sabiha Keis ,Zanzibar
WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo
ya Makaazi Rahma Kassim Ali amesema asilimia 80% ya migogoro ya ardhi katika
maeneo mbali mbali ya Zanzibar yanasababishwa na baadhi ya madalali kwenda kinyume
na taratibu za kisheria zilizowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari uliyofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo Maisara jana, Alisema asilimia kubwa ya migogoro ya
ardhi inachangiwa na madalali kwa kuuza viwanja bila kufuata taratibu za kisheria
zilizowekwa katika uuzaji na ununuzi hali ambayo inasababisha migogoro ya ardhi
kuendele kujitokeza nchini.
Alisema kutokana hali hiyo wizara
yake inajipanga kuandaa utaratibu maalum wa kuweza kudhibiti tatizo hilo ambalo
linarudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo. Lakini kuanzia sasa mtu
akijulikana anauza kiwanja kinyume na utaratibu sheria itachuka mkondo wake.
"Napenda kuwasihi
wananchi wanapotaka kununua ardhi katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kufika
katika taasisi husika iliyowekwa kisheria ili kuepusha migogoro ya ardhi
kuongezeka Zanzibar"Alisema Waziri Rahma.
Aidha ametoa wito kwa
wananchi wa Zanzibar pamoja na wageni ambao wanania ya kuekeza kufika taasisi
husika na kuacha kuwatumia madalali katika hatua za ununuzi wa ardhi kwani umiliki
wa ardhi unahitaji hatua mbali mbali za kisheria zikamilike ndipo mnunuzi
atakuwa salama katika uwekezaji wake.
Sambamba na hayo Waziri huyo aliwataka
wananchi ambao wamepewa viwanja na SMZ kwaajili ya matumizi mbali mbali kuayaendeleza
maeneo hayo ili kuzidhibiti kwa lengo la kuepusha uvamizi na kusababisha
migogoro ardhi kuendelea kujitokeza kila siku.
Alieleza kwamba Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar imetoa agizo la muda wa miezi sita kwa mwananchi aliyepewa
ardhi kuendeleza matumizi ya ardhi katika eneo alilopewa mara tu anapopata
umiliki rasmi huku raia wa kigeni wamepewa muda wa mwaka mmoja kinyume na hilo
eneo hilo litarudi Serikalini.
"Niwatake wananchi
pamoja na raia wa kigeni kuhakikisha wanayaendeleza maeneo kwa mujibu wa sheria
iliyowekwa na wasipo yaendeleza kwa muda uliowekwa maeneo hayo yatarudi
Serikalini" Alisisitiza Waziri Rahma.
Wakati huo huo alifahamisha
kua katika kukabiliana na changamoto ya upangaji miji hivi karibuni Wizara ya
Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar ilitiliana saini na kampuni ya
Properties lnternational kutoka Tanzania bara kwa lengo la kushirikiana katika
suala zima la upangaji miji na vijiji ambapo kwa hatua ya awali kazi hiyo
itahusisha maeneo ya akiba yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mkutano huo kwa waandishi wa
habari umekuja mara baada ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar kufanya
ziara katika maeneo mbali mbali pamoja na kufanya tathmini ya ongezeko la
migogoro ya ardhi nchini.
Mwisho.
Comments
Post a Comment